Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wajue Watu wa Timor Mashariki

Wajue Watu wa Timor Mashariki

Wajue Watu wa Timor Mashariki

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

TIMOR MASHARIKI, au Timor-Leste, ni nchi ndogo inayopatikana kwenye sehemu ndogo ya mashariki ya kisiwa cha Timor. Neno la Kimaleya “Timor” na neno la Kireno Leste yote yana maana ileile yaani, “mashariki.” Watu wanaozungumza Kiswahili huiita nchi hiyo Timor Mashariki. Jina hilo linafaa kwani nchi hiyo inapatikana kwenye ncha ya mashariki zaidi ya visiwa vya Indonesia.

Nchi ya Timor Mashariki ina ukubwa wa kilomita 14,800 za mraba, kwa hiyo eneo hilo ni karibu nusu tu ya ukubwa wa Burundi. Hata ingawa kisiwa hicho ni kidogo, kina mchanganyiko wa mazingira ya asili ya Asia na ya Australia. Huko kuna misitu minene na vilevile nyanda kavu za vichaka vya mikaratusi na nyasi kavu. Pia, kuna mchanganyiko wa wanyama kutoka Australia na Asia. Kwa mfano, aina fulani ya wanyama wasiokuwa na kondo na walio na kifuko cha kubebea watoto wa Australia na ndege, wanaishi pamoja na tumbili wa Asia na mamba wa maji ya chumvi. Vipi kuhusu watu wa Timor Mashariki? Je, ungependa kuwafahamu?

Kumbukumbu za Ukoloni

Huenda wasafiri Wareno walifika Timor Mashariki karibu mwaka wa 1514. Wakati huo misitu ya misandali ilikuwa imeenea kwenye milima. Biashara ya miti ya misandali ilikuwa na faida kubwa na hiyo ilikuwa sababu ya kutosha kuwafanya Wareno waanzishe kituo cha biashara. Pia, Kanisa Katoliki lilipendezwa na eneo hilo na wakataka kutuma wamishonari wawageuze wenyeji kuwa Wakatoliki. Sababu hizo mbili ziliwachochea Wareno kuanza kutawala kisiwa hicho mnamo 1556.

Hata hivyo, kisiwa cha Timor Mashariki hakikutiliwa maanani sana na wakoloni. Waholanzi walipoanza kumiliki upande wa magharibi wa kisiwa hicho mnamo 1656, Wareno wakajisogeza upande wa mashariki. Hatimaye mwaka wa 1975, baada ya utawala wa kikoloni wa miaka 400, Wareno waliondoka.

Mwaka huohuo, vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka. Kwa miaka 24 iliyofuata wenyeji wapatao 200,000 waliuawa katika vita hivyo, yaani asilimia 33 hivi ya watu wa Timor Mashariki. Ghafula ujeuri uliongezeka katika nchi nzima mwaka wa 1999, ukisababisha asilimia 85 ya nyumba na huduma za msingi kuharibiwa. Mamia ya maelfu ya watu walikimbilia milimani. Mwishowe Umoja wa Mataifa uliingilia kati na kukomesha uharibifu na kutuliza hali.

Tangu wakati huo, wenyeji wa Timor Mashariki wamejitahidi kuboresha maisha yao yaliyovurugika. Mnamo Mei (Mwezi wa 5) 2002, Timor Mashariki au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor Mashariki, ilitambuliwa rasmi na ikawa taifa jipya duniani.

Nchi Yenye Tamaduni Nyingi

Nchi ya Timor Mashariki ina tamaduni na lugha nyingi kwa sababu ya biashara ambayo imefanywa huko kwa karne nyingi, wahamiaji wenye asili ya Asia na Australia, na wakoloni kutoka Ulaya. Ingawa Kireno ndiyo lugha ya biashara na taifa, asilimia 80 ya watu huzungumza lugha rasmi iitwayo Tetum, lugha ambayo ina maneno mengi ya Kireno. Makabila mbalimbali nchini humo huzungumza angalau lugha nyingine 22.

Vijijini kuna wafalme wa kikabila wanaoongoza mambo. Wanasimamia sherehe, mgawanyo wa ardhi, na mambo mengine ya kitamaduni, wakati chifu wa kuchaguliwa ndiye anayesimamia mambo ya kiserikali.

Dini nchini humo ni mchanganyiko wa ibada ya maumbile na Ukatoliki. Kila sehemu ya maisha yao inaongozwa na ibada ya mababu, uchawi, na kuwasiliana na pepo. Watu ambao kwa kawaida wanaenda kanisani, pia huenda kwa waganga wa kienyeji wanaoitwa matan doʹok, ili watabiri wakati ujao, wawaponye magonjwa, au ili wayafukuze mapepo mabaya.

Watu Wadadisi na Wakarimu

Kiasili watu wa Timor Mashariki, ni wacheshi, wadadisi, na wakarimu. “Tunapenda kujifunza, kuzungumza, kuingiliana, na hata kuchangamana na wageni,” anasema Rais Kay Rala Xanana Gusmão.

Huenda mgeni anayekaribishwa kula mlo wa jioni na familia ya Kitimori atakula kwanza na kichwa cha familia. Mke na watoto wake watawaandalia chakula kisha wao watakula baadaye jioni. Ni vema kuchukua kwanza kiasi kidogo cha chakula. Mgeni atamfurahisha sana mpishi kwa kuomba aongeze tena chakula.

Milo ya Watimori inatia ndani wali, mahindi, au mihogo, nayo huliwa na mboga za majani. Saboko, ni kati ya vyakula vinavyopendwa sana, ni mchanganyiko wa dagaa, mchuzi wa ukwaju, na viungo vingine, vyote hufungwa kwenye jani la mchikichi. Si rahisi kununua nyama huko kwani bei yake ni ghali sana.

Familia Zenye Watoto Wengi

Timor Mashariki ni taifa la vijana. Karibu nusu ya watu nchini humo ni vijana, na familia nyingi zina kati ya watoto 10 na 12 wanaoishi katika nyumba moja.

Mara nyingi watoto wanapoenda shuleni wanatembea wakiwa wameshikana mikono, wavulana kwa wavulana na wasichana kwa wasichana, wakicheka na kuimba. Zaidi ya silabasi ya kawaida ya masomo, wanafunzi hufundishwa tabia njema na kanuni zinazofaa katika maisha.

Watoto Watimori hawachezi peke yao kimyakimya, badala yake watoto wote majirani wanajiunga katika mchezo huo! Mchezo unaopendwa sana unaitwa dudu karreta, yaani mchezo wa kusukuma gari. Gari hilo la kuwaziwa ni rimu ya baiskeli. Watoto hukimbia mitaani wakicheka na kuiendesha rimu hiyo wakitumia kijiti.

Hata hivyo, watoto Watimori hawachezi tu. Kwa mfano, wanaweza kupewa kazi ya kutwanga mahindi wakitumia mchi mzito wa chuma. Lakini wanapoendelea kufanya kazi wao hutabasamu kana kwamba hawajui wamezaliwa katika mojawapo ya mataifa kumi maskini zaidi duniani.

Matatizo ya Taifa Jipya

Umaskini uliopindukia umesababisha maisha ya Watimori wengi kuwa magumu sana. Asilimia 40 ya watu wanatumia kiasi cha dola 1.50, kiasi cha chini kinachohitajika ili kununua chakula na mahitaji mengine ya nyumbani. Huduma za msingi zimeharibika. Ripoti moja ya serikali inasema hivi: “Nchini kote, watu watatu kati ya wanne hawana umeme, watu watatu kati ya watano wanaishi kwenye mazingira mabaya na asilimia 50 hawana maji safi ya kunywa.”

Chini ya hali hizi magonjwa ni mengi. Utapiamlo, malaria, kifua kikuu, na magonjwa mengine yanasababisha watu waishi kwa wastani miaka 50 tu. Karibu mtoto 1 kati ya 10 anakufa kabla ya kufikia miaka mitano. Inakadiriwa kwamba mnamo 2004, ni madaktari 50 waliokuwa wakihudumia karibu watu 800,000.

Mataifa mengi yameanza kushirikiana na Umoja wa Mataifa kusaidia nchi ya Timor Mashariki iliyoharibiwa. Wingi wa mafuta na gesi kwenye Bahari ya Timor pia unaleta matumaini ya kwamba hali ya uchumi itabadilika. Hata hivyo, utajiri mkubwa zaidi wa Timor Mashariki ni watu wake wanyenyekevu na imara. Mwanamke mmoja wa Timor alimwambia hivi mwandishi wa Amkeni!: “Ingawa sisi ni maskini, hilo halimaanishi eti hatuna furaha!”

“Habari Njema za Jambo Bora”

Hivi karibuni Mashahidi wa Yehova wamewapelekea wenyeji wa Timor Mashariki “habari njema za jambo bora.” (Isaya 52:7; Waroma 10:14, 15) Mnamo 2005 kutaniko pekee la Mashahidi nchini humo lilitumia saa 30,000 kuwaambia watu juu ya ahadi nzuri za Biblia kuhusu dunia paradiso inayokuja.—Zaburi 37:10, 11; 2 Petro 3:13.

Kujifunza kweli za Biblia kumewaweka huru wenyeji fulani kutokana na nira ya ushirikina. Kwa mfano, Jacob, mwanamume mwenye watoto watano, alikuwa amejihusisha sana na tamaduni zenye ushirikina. Mara nyingi alikuwa akitoa dhabihu za wanyama kwa ajili ya roho za wafu. Desturi hiyo ilizidisha shida za kiuchumi za familia yake. Kutoa dhabihu ya kuku kunagharimu karibu mshahara wa siku moja, na kutoa dhabihu ya mbuzi au nguruwe kunagharimu mshahara wa majuma kadhaa.

Baada ya muda mke wa Jacob aitwaye Fransiska, alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Alimsomea Jacob Maandiko yanayoonyesha kwamba wafu hawajui lolote na hawawezi kuwadhuru walio hai. (Mhubiri 9:5, 10; Ezekieli 18:4) Jacob akakubali kile ambacho Biblia inasema na wakaacha kutolea roho waovu dhabihu. Hilo lilifanya watu wa ukoo wawatenge na kuwaambia kwamba mapepo yamekasirishwa na yatawaua. Hata hivyo, Jacob na Fransiska walisimama imara na kusema: “Yehova atatulinda.”

Jacob alianza kujifunza Biblia na kuhudhuria mikutano ya Kikristo pamoja na familia yake. Hilo lilimsaidia kufanya mabadiliko mengine maishani. Ingawa kwa miaka mingi alikuwa anavuta pakiti moja ya sigara kwa siku, aliacha kuvuta. Pia alijifunza kusoma na kuandika. Wakati huohuo Fransiska aliacha kutafuna miraa. Mwishowe, mnamo 2005, Jacob na Fransiska walibatizwa na kuwa Mashahidi wa Yehova. Sasa, wanatumia pesa zao kwa hekima ili kuwasomesha watoto na kulipia gharama zinazohitajika za matibabu.

Kwa kweli, kama vile Yesu alivyotabiri, habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa “mpaka sehemu ya mbali zaidi ya dunia,” kutia ndani watu wadadisi, wakarimu, na wema wa kisiwa kidogo cha Timor Mashariki.—Matendo 1:8; Mathayo 24:14.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

“Kuleta Kigurudumu cha Uzi na Uzi”

“Kuleta kigurudumu cha uzi na uzi” ni msemo wa Watimori uliotumiwa mtoto wa kike anapozaliwa. Unafafanua kazi ya wanawake Watimori ya ufumaji wa tais, kitambaa maridadi. Tais hutumiwa kutengeneza mavazi yenye madoido ya sherehe, mablanketi, na mavazi yanayorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Wanawake wenye umri mkubwa huwafundisha wanawake wachanga kukuza, kuchuma, kusokota, kutia rangi, na kufuma pamba ili kutengeneza nguo zenye nakshi na rangi zenye kupendeza. Ikitegemea mtindo unaofumwa, vazi moja linaweza kuchukua kipindi cha mwaka mzima au zaidi kumalizika. Kwa kuwa kila eneo lina mitindo yake ya kitamaduni, mtaalamu anaweza kujua mara moja mahali ambapo tais ilitengenezwa.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

PAPUA NEW GUINEA

INDONESIA

TIMOR MASHARIKI

AUSTRALIA

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nyumba ya kitamaduni yenye umbo la pia

[Picha katika ukurasa wa 16]

“Dudu karreta”—mchezo unaopendwa na watoto

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Jacob na familia yake