Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watoto Watishwa

Watoto Watishwa

Watoto Watishwa

Inapofika jioni, utaona maelfu ya watoto wakitembea miguu mitupu kwenye barabara zilizo kaskazini mwa Uganda. Wao huondoka vijijini mwao kabla ya giza kuingia wakielekea kwenye miji kama vile Gulu, Kitgum, na Lira. Wanapofika huko, wanatawanyika na kuelekea kwenye majengo, vituo vya basi, bustani, na nyua. Kunapopambazuka, unawaona tena barabarani wakirudi nyumbani. Kwa nini kila siku wao hufunga safari hiyo isiyo ya kawaida?

WATU fulani huwaita wasafiri wa usiku. Lakini watoto hao hawaendi kufanya kazi usiku. Wao huondoka nyumbani jioni kwa sababu giza linapoingia, sehemu za mashambani wanakoishi huwa hatari.

Kwa miaka 20 hivi, waasi wamekuwa wakivamia sehemu hizo za mashambani na kuwateka nyara watoto. Kila mwaka wao huteka mamia ya wavulana na wasichana kutoka nyumbani na kupotelea msituni. Mara nyingi watoto hao hutekwa nyara usiku nao hutumiwa na waasi hao kama askari, wabebaji wa mizigo, na wasichana wa kufanya ngono nao. Mateka hao wasipotii, huenda wakakatwa pua au midomo. Wale ambao hujaribu kutoroka hukamatwa na kuuawa kikatili.

Kuna wahasiriwa wengine wachanga wa ugaidi. Huko Sierra Leone, vijana ambao ni vilema walikuwa wachanga sana wakati wanaume wenye mapanga walipokata miguu na mikono yao. Wavulana na wasichana huko Afghanistan hucheza na mabomu ya ardhini yanayofanana na vipepeo nao hupoteza vidole na macho yao vitu hivyo vya kuchezea vyenye kuvutia vinapolipuka.

Vijana fulani huathiriwa kwa njia tofauti kunapotokea shambulizi la kigaidi. Kwa mfano, katika shambulizi la kigaidi lililofanywa 1995 huko Oklahoma City, Marekani, kati ya watu 168 waliouawa kulikuwa na watoto 19 na baadhi yao walikuwa vitoto. Kama tu upepo wenye nguvu unavyozima mishumaa, bomu hilo lilikomesha mara moja uhai wa vitoto hivyo. Shambulizi hilo la kigaidi liliwapokonya watoto hao maisha yao, likawazuia wasicheze, wasicheke wala kupakatwa na mama na baba zao.

Hayo ni matukio ya hivi karibuni, lakini kama tutakavyoona, wanadamu wamekumbwa na vitendo vya kigaidi kwa miaka mingi.

[Sanduku katika ukurasa wa 3]

KUJITAYARISHIA KIFO CHA MTOTO

“Leo asubuhi nilipomwamsha mwanangu mwenye umri wa miaka 11, aliniuliza, ‘Je, tayari magaidi wameshambulia leo?’” Ndivyo alivyoandika mwandishi David Grossman kuhusu jeuri inayoendelea katika nchi anamoishi. Aliendelea kusema hivi: “Mwanangu anaogopa.”

Katika miaka ya karibuni, watoto wengi sana wamekufa katika mashambulizi ya kigaidi hivi kwamba wazazi wengi hujitayarisha iwapo mtoto wao anaweza kuuawa kijeuri. “Sitasahau kamwe jinsi wapenzi wawili walivyonieleza kuhusu mipango yao ya wakati ujao,” akaandika Grossman. “Walisema watafunga ndoa na kupata watoto watatu. Si wawili, bali watatu. Ili iwapo mmoja atakufa, wawili watabaki.”

Hawakusema jambo watakalofanya iwapo watoto wawili wangekufa, au wote watatu. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Manukuu haya yametoka katika kitabu Death as a Way of Life, cha David Grossman.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

© Sven Torfinn/ Panos Pictures