Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia Iliyojaa Umwagaji wa Damu

Historia Iliyojaa Umwagaji wa Damu

MIAKA michache tu iliyopita, ilionekana kwamba ugaidi ulitukia tu katika sehemu chache kama vile Ireland Kaskazini, eneo la Basque huko kaskazini mwa Hispania, na sehemu nyingine za Mashariki ya Kati. Sasa, hasa tangu Septemba 11, 2001, wakati majengo ya Twin Towers yalipoharibiwa huko New York, ugaidi umeongezeka haraka ulimwenguni pote. Umetukia kwenye kisiwa maridadi cha Bali; Madrid, Hispania; London, Uingereza; Sri Lanka; Thailand, na hata Nepal. Hata hivyo, ugaidi si jambo geni. Neno “ugaidi” linamaanisha nini?

Ugaidi umefafanuliwa kuwa “matumizi au vitisho vya kutumia nguvu kiharamu au jeuri inayofanywa na mtu ama kikundi dhidi ya watu au mali kwa lengo la kutisha au kulazimisha jamii ama serikali, kwa sababu ya kutekelezwa kwa mawazo yao au kwa sababu za kisiasa.” (The American Heritage Dictionary of the English Language) Hata hivyo, mwandishi Jessica Stern anasema: “Mtu anayechunguza ugaidi hupata kwamba neno hilo lina ufafanuzi mwingi . . . Lakini ni mambo mawili tu ambayo hutofautisha ugaidi na jeuri ya aina nyingine.” Ni mambo gani hayo? “Kwanza, ugaidi hulenga raia. . . . Pili, magaidi hutumia jeuri kutimiza kusudi kubwa: kuwafanya walengwa waogope huwa muhimu kuliko madhara yanayotokana na ugaidi. Kutokeza woga kimakusudi kwa njia hiyo ndiko hutofautisha ugaidi na mauaji au mashambulizi ya kawaida.”

Ugaidi Ulianza Zamani

Katika Yudea ya karne ya kwanza, kikundi fulani cha Wayahudi washupavu kilipigania uhuru kutoka kwa Waroma. Baadhi ya wafuasi wake sugu waliitwa Wasikarii, au wanaume wenye kutumia visu, jina linalotokana na panga fupi walizoficha ndani ya nguo zao. Wakichangamana na umati uliokuja kwenye sherehe huko Yerusalemu, Wasikarii walikata koo za adui zao au kuwadunga kisu mgongoni. *

Mnamo 66 W.K., kikundi hicho shupavu kilitwaa ngome ya Masada karibu na Bahari ya Chumvi. Walichinja kikosi cha askari Waroma na kufanya ngome hiyo ya mlimani kuwa kituo chao. Kwa miaka mingi, walitumia kituo hicho kuwashambulia na kuwasumbua wanajeshi Waroma. Mnamo 73 W.K., Kikosi cha Kumi cha Roma kikiongozwa na Gavana Flavio Silva kiliteka tena Masada lakini hakikushinda washupavu hao. Mwanahistoria mmoja aliyeishi wakati huo anadai kwamba badala ya kusalimu amri ya Roma, washupavu 960 kati yao walijiua isipokuwa tu wanawake wawili na watoto watano.

Watu fulani huona uasi huo wa washupavu hao kuwa mwanzo wa ugaidi. Vyovyote vile, tangu wakati huo, ugaidi umeathiri sana ulimwengu.

Ugaidi Umetumiwa na Jumuiya ya Wakristo

Kuanzia mwaka wa 1095 na kuendelea kwa karne mbili, majeshi yaliyopigana “vita vitakatifu” yalipitapita kwa ukawaida kati ya Ulaya na Mashariki ya Kati. Majeshi ya Waislamu kutoka Asia na Afrika Kaskazini yalipigana nao. Wote walitaka kumiliki Yerusalemu, na kila upande ulijaribu kuushinda ule mwingine. Katika vita vingi walivyopigana, hao “wapiganaji watakatifu” walichinjana kikatili. Pia waliwakatakata watu wasio na hatia kwa mapanga na mashoka. William wa Tyre, kasisi aliyeishi karne ya 12, alieleza hivi kuhusu jinsi “wapiganaji watakatifu” walivyovamia Yerusalemu mnamo 1099:

“Wote waliandamana barabarani wakiwa wamebeba mapanga na mikuki. Walikatakata na kuua kila mtu waliyekutana naye, wanaume, wanawake, na watoto, bila kuacha yeyote. . . . Waliua watu wengi sana hivi kwamba maiti zilitapakaa barabarani na ilibidi watu wapite juu ya miili hiyo. . . . Kulikuwa na umwagaji mwingi sana wa damu hivi kwamba mitaro ilijaa damu na barabara zote za mji zilijaa maiti.” *

Katika karne zilizofuata, magaidi walianza kutumia vitu vinavyolipuka na bunduki zinazoweza kuua kikatili.

Mamilioni Wafa

Wanahistoria huona Juni 28, 1914, kuwa siku iliyobadili historia ya Ulaya. Kijana mmoja, ambaye watu fulani humwona kuwa shujaa alimpiga risasi Mwana-mfalme wa Austria, Francis Ferdinand. Tukio hilo liliwatumbukiza wanadamu kwenye Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Kabla ya hivyo Vita Vikuu kwisha, watu milioni 20 walikuwa wamekufa.

Juni 28, 1914, ulimwengu uliingia vitani

Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilifuatwa na Vita vya Pili vya Ulimwengu ambavyo vilikuwa na kambi za mateso, raia waliuawa kwa mabomu, na matendo ya kulipiza kisasi kwa kuua watu wasio na hatia. Baada ya vita hivyo, mauaji yaliendelea. Zaidi ya watu milioni moja waliuawa katika vita huko Kambodia miaka ya 1970. Na bado Wanyarwanda hawajasahau mauaji ya watu zaidi ya 800,000 katika miaka ya 1990.

Tangu mwaka wa 1914 hadi wakati wetu, wanadamu wameteseka sana kwa sababu ya matendo ya ugaidi katika nchi nyingi. Hata hivyo, watu fulani leo hutenda kana kwamba hawajajifunza chochote kutokana na historia. Kwa kawaida, mashambulizi ya kigaidi yameua mamia, yakalemaza maelfu, na kuwapokonya mamilioni amani ya akili na usalama. Mabomu hulipuka kwenye masoko, vijiji huteketezwa kabisa, wanawake hulalwa kinguvu, watoto hutekwa nyara, na watu hufa. Licha ya sheria na shutuma za ulimwenguni pote, matendo haya ya kinyama hayakomi. Je, kuna tumaini lolote kwamba ugaidi utakwisha?

^ fu. 5 Kama inavyotajwa katika Matendo 21:38, kamanda mmoja wa jeshi la Roma alimshtaki isivyo haki mtume Paulo kuwa kiongozi wa wanaume 4,000 “wenye kutumia visu.”

^ fu. 10 Yesu aliwafundisha wanafunzi wake ‘wawapende adui zao,’ badala ya kuwachukia na kuwaua.—Mathayo 5:43-45.