Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Nyumba?

Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Nyumba?

Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Nyumba?

JOSEPHINE mwenye umri wa miaka 36 anaishi na wavulana wake watatu wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 11 kwenye kitongoji cha jiji fulani la Afrika. Ili kujiruzuku, yeye huokota plastiki na kuziuza kwenye kiwanda fulani. Yeye hupata dola mbili hivi kwa siku kwa kazi hiyo inayochosha sana. Katika jiji hilo, pesa hizo hazitoshi kuilisha familia yake au kuwalipia karo ya shule.

Jioni, yeye hurudi mahali anapopaita nyumbani. Kuta za nyumba yake zimejengwa kwa miti myembamba na kukandikwa kwa udongo na matofali yaliyochomwa. Paa yake imetengenezwa kwa mabati yenye kutu pamoja na mikebe na plastiki. Vipande vya mawe, mbao, na vyuma vimewekwa juu ya paa ili lisipeperushwe na upepo mkali. “Mlango” na “dirisha” la nyumba yake limetengenezwa kwa magunia yaliyochakaa, ambayo hayawezi kutoa ulinzi wowote dhidi ya hali mbaya ya hewa wala wavamizi.

Hata hivyo, nyumba hiyo duni si mali yake. Kila wakati Josephine na watoto wake huishi kwa woga kwamba watafukuzwa. Ardhi ambayo nyumba yao duni imejengwa imetengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara iliyo karibu. Kwa kusikitisha, kuna hali kama hizo katika nchi nyingi ulimwenguni.

Nyumba Yenye Sumu

Robin Shell, ofisa mwenye cheo cha juu katika shirika moja la kimataifa la kusaidia watu kujenga nyumba anasema kwamba kwa sababu ya kuishi katika “nyumba duni, . . . watoto huaibikia nyumba yao, . . . kila wakati washiriki wa familia huwa wagonjwa, na . . . hawajui ni lini afisa wa serikali au mwenye nyumba atakuja kubomoa [nyumba yao].”

Kuishi katika hali hizo huwafanya wazazi wawe na wasiwasi daima kuhusu afya na usalama wa watoto wao. Badala ya kufanya kazi ili kuboresha hali yao, mara nyingi wao hutumia wakati na nguvu nyingi wakijitahidi kupata mahitaji ya lazima ya watoto wao, kama vile chakula, mapumziko, na makao.

Mtu asiyefahamu hali hiyo anaweza kukata kauli kwamba maskini wanaweza kuboresha hali yao iwapo wangejitahidi zaidi. Lakini suluhisho si tu kuwaambia watu wajitahidi zaidi. Kuna mambo mengi mazito yanayohusika katika tatizo la nyumba ambayo yanapita uwezo wa mwanadamu yeyote. Watafiti wanataja visababishi vikuu kuwa ongezeko la idadi ya watu, watu wengi kuhamia mijini, misiba ya asili, misukosuko ya kisiasa, na umaskini usiokoma. Mambo hayo ni kama vidole vitano vinavyowanyonga watu wengi maskini.

Mikazo Inayosababishwa na Ongezeko la Watu

Kwa ujumla, inakadiriwa kwamba kila mwaka ulimwenguni pote watu wengine milioni 68 hadi milioni 80 huhitaji makao. Kulingana na Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, idadi ya watu ulimwenguni ilipita bilioni 6.1 mnamo 2001 na inatarajiwa kufika kati ya bilioni 7.9 na bilioni 10.9 kufikia 2050. Jambo linaloshtua hata zaidi ni kwamba inatabiriwa kuwa asilimia 98 ya ongezeko hilo katika miaka 20 ijayo litatokea katika nchi zinazositawi. Makadirio hayo yanaonyesha kwamba kutakuwa na tatizo kubwa sana la nyumba. Hata hivyo, tatizo hilo linakuwa baya hata zaidi kwa sababu katika nchi nyingi, maeneo yanayokua haraka zaidi ni majiji ambayo tayari yamesongamana.

Watu Wengi Wanahamia Mijini

Mara nyingi, watu huona kwamba majiji makubwa kama vile, New York, London, na Tokyo huwakilisha ukuzi wa kiuchumi wa nchi. Kwa sababu hiyo, kila mwaka maelfu ya watu wa mashambani hufurika katika majiji wakitafuta hali bora za maisha, hasa elimu na kazi.

Kwa mfano, uchumi wa China unakua haraka. Kwa sababu hiyo, ripoti moja inakadiria kwamba katika miongo kadhaa ijayo, zaidi ya nyumba mpya milioni 200 zitahitajika katika majiji makubwa pekee. Idadi hiyo ni karibu maradufu ya nyumba zote zilizoko Marekani leo. Ni mradi gani wa ujenzi unaoweza kutosheleza mahitaji hayo?

Kulingana na Benki ya Dunia, “kila mwaka, familia milioni 12 hadi 15 hivi, zinazohamia miji ya nchi zinazositawi, zinahitaji idadi kama hiyo ya nyumba.” Kwa kuwa hakuna nyumba za kutosha ambazo familia hizo maskini zinaweza kugharimia, zinalazimika kuishi mahali popote penye makao, mara nyingi mahali ambapo hakuna mtu yeyote angependa kuishi.

Misiba ya Asili na ya Kisiasa

Umaskini umewafanya watu waishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko, maporomoko ya ardhi, na matetemeko ya nchi. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba huko Caracas, Venezuela, watu zaidi ya nusu milioni “huishi katika makao ya maskwota yaliyo kwenye miteremko mikali ambayo huathiriwa daima na maporomoko ya ardhi.” Pia, kumbuka aksidenti iliyotokea katika kiwanda fulani huko Bhopal, India, mwaka wa 1984 na kuua maelfu ya watu na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa nini watu wengi hivyo walikufa au kujeruhiwa? Ni kwa sababu kitongoji kimoja duni kilikuwa kimepanuka na kufikia meta tano tu kutoka kwenye mpaka wa kiwanda hicho.

Pia misiba ya kisiasa, kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, imechangia sana matatizo ya nyumba. Ripoti moja iliyochapishwa mwaka wa 2002 na kikundi kimoja kinachotetea haki za binadamu ilisema kwamba kati ya mwaka wa 1984 na 1999 huenda watu wapatao milioni 1.5 walilazimika kuhama vijiji vyao huko kusini-mashariki mwa Uturuki kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wanakijiji wengi walilazimika kutafuta makao mahali popote ambapo wangeweza, mara nyingi wakisongamana na watu wa jamaa na majirani wao katika makao ya muda, nyumba za kukodisha, majengo ya shambani, au nyumba ambazo hazijakamilika. Inasemekana kwamba familia kadhaa ziliishi katika mazizi, watu 13 au zaidi wakiishi katika chumba kimoja, wakitumia choo kimoja, na mfereji mmoja uliokuwa katika ua. Mmoja wa wakimbizi hao alisema: “Hatungependa kuendelea kuishi hivi. Tunaishi katika makao ya wanyama.”

Kutokuwepo kwa Maendeleo ya Kiuchumi

Mwishowe, kuna uhusiano mkubwa kati ya nyumba na hali ya kiuchumi ya maskini. Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia iliyotajwa awali, ilisemekana kuwa mnamo 1988 pekee, kulikuwa na maskini milioni 330 kati ya watu walioishi katika majiji ya nchi zinazositawi, hali ambayo haikutarajiwa kubadilika sana katika miaka iliyofuata. Ikiwa watu ni maskini sana hivi kwamba hawawezi kugharimia mahitaji ya lazima kama vile chakula na mavazi, watawezaje kulipa kodi au kujenga nyumba nzuri?

Kiwango cha juu cha riba na inflesheni hufanya familia nyingi zisiweze kupata mkopo kutoka kwenye benki, na gharama za matumizi zinazoongezeka hufanya iwe vigumu kwa wengi kuboresha hali yao ya kiuchumi. Asilimia 20 hivi ya watu katika nchi fulani hawana kazi na hivyo ni vigumu kwao kupata mahitaji ya lazima.

Sababu hizo na nyingine zimewalazimisha mamia ya mamilioni ya watu katika sehemu zote ulimwenguni waishi katika nyumba za hali ya chini. Watu huishi ndani ya mabasi makuukuu, kontena za kusafirishia vitu, na katoni. Wengine huishi chini ya ngazi, katika nyumba zilizojengwa kwa karatasi za plastiki, au vipande vya mbao. Hata wengine huishi katika viwanda vilivyoacha kutumiwa.

Ni Jitihada Gani Zinazofanywa?

Tayari jitihada nyingi zinafanywa na mashirika mengi, serikali, na watu wengi wanaojali ili kushughulikia tatizo hilo. Nchini Japani, mashirika kadhaa yameanzishwa ili kusaidia kujenga nyumba za bei nafuu. Mradi mmoja wa ujenzi ulioanzishwa nchini Afrika Kusini mwaka wa 1994, umesaidia kujenga nyumba zaidi ya milioni moja zenye vyumba vinne. Nchini Kenya, mradi fulani wa ujenzi unakusudia kujenga nyumba 150,000 katika maeneo ya jijini na kujenga mara mbili ya idadi hiyo katika maeneo ya mashambani kila mwaka. Nchi nyingine kama vile Madagaska zimeelekeza jitihada zao kutafuta mbinu za kujenga nyumba zisizo za gharama kubwa.

Mashirika ya kimataifa kama vile mradi wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia makao (UN-HABITAT), yamebuniwa ili kuonyesha kwamba ulimwengu umeazimia “kuzuia na kutatua matatizo yanayosababishwa na ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini.” Mashirika yasiyojipatia faida na yasiyo ya kiserikali pia yanajaribu kusaidia. Shirika moja lisilojipatia faida limesaidia zaidi ya familia 150,000 katika nchi mbalimbali kuboresha nyumba zao za hali ya chini. Linakadiria kwamba kufikia mwaka wa 2005, litakuwa limesaidia watu milioni moja kupata nyumba sahili, nzuri, na ya bei nafuu.

Mengi ya mashirika hayo yako tayari kutoa habari zitakazowasaidia watu wanaoishi katika nyumba za hali ya chini wakabiliane ifaavyo na hali zao au hata kuziboresha. Bila shaka, ikiwa unahitaji msaada unaweza kunufaika na mipango hiyo. Pia kuna mambo mengi ya msingi ambayo unaweza kufanya ili kujisaidia.—Ona sanduku “Nyumba na Afya Yako,” kwenye ukurasa wa 7.

Bila kujali kama unaweza kuboresha hali yako, hakuna tumaini kwamba mtu fulani au shirika fulani la kibinadamu linaweza kuondoa na kumaliza mambo yanayosababisha tatizo la nyumba ulimwenguni pote. Jamii ya kimataifa inaendelea kushindwa kukabiliana na uhitaji wa haraka na unaoongezeka wa maendeleo ya kiuchumi na kutoa msaada wa kibinadamu. Kila mwaka mamilioni ya watoto wanazaliwa katika hali hiyo ya umaskini inayozidi kuzorota. Je, kuna tumaini lolote halisi la kutatua tatizo hilo kabisa?

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

NYUMBA NA AFYA YAKO

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, kwa ujumla, ili kuwa na afya nzuri, nyumba inapaswa angalau kuwa na vitu vifuatavyo:

▪ Paa nzuri ili kuzuia mvua

▪ Kuta na milango mizuri ili kujikinga dhidi ya hali mbaya ya hewa na kuwazuia wanyama wasiingie

▪ Wavu wa waya kwenye madirisha na milango ili kuwazuia wadudu, hasa mbu

▪ Paa zilizorefushwa kuzunguka nyumba ili kuzuia jua lisiharibu kuta za nyumba

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

NYUMBA ZA KIENYEJI KATIKA MAENEO YA MASHAMBANI AFRIKA

Nyumba za kienyeji zimekuwapo kwa miaka mingi. Zilikuwa na ukubwa na maumbo mbalimbali. Jamii fulani, kama vile Wakikuyu na Wajaluo wa Kenya, walipendelea kujenga kuta za mviringo na paa zilizoezekwa kwa nyasi zenye umbo la pia. Jamii nyingine, kutia ndani Wamasai wa Kenya na Tanzania, walijenga nyumba zenye umbo kama la mstatili. Katika maeneo ya pwani ya Mashariki ya Afrika, nyumba fulani zilikuwa na paa iliyoezekwa kwa nyasi ambayo iligusa ardhi na iliyofanana na mzinga wa nyuki.

Kwa kuwa vifaa vya kujenga nyumba hizo vilipatikana kwa urahisi, hakukuwa na matatizo mengi ya nyumba. Udongo wa kujenga ungepatikana kwa kuuchanganya tu na maji. Misitu mingi iliyokuwepo karibu ilifanya iwe rahisi kupata mbao, nyasi, matete, na majani ya mianzi. Kwa hiyo, haidhuru familia ilikuwa tajiri au maskini kadiri gani, ingeweza kuwa na nyumba yake yenyewe.

Bila shaka, nyumba kama hizo zilikuwa na matatizo fulani. Kwa kuwa paa nyingi zilitengenezwa kwa vifaa ambavyo vingeweza kushika moto, kulikuwa na hatari kubwa ya kutokeza moto. Pia, mvamizi angeweza kuingia ndani ya nyumba kwa urahisi kwa kutoboa tu shimo katika ukuta wa udongo. Basi, haishangazi kwamba katika maeneo mengi leo, nyumba zinazoweza kudumu zinachukua mahali pa nyumba za kienyeji za Afrika.

[Hisani]

Chanzo: African Traditional Architecture

Huts: Courtesy Bomas of Kenya Ltd - A Cultural, Conference, and Entertainment Center

[Picha katika ukurasa wa 5]

ULAYA

[Hisani]

© Tim Dirven/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 6]

AFRIKA

[Picha katika ukurasa wa 6]

AMERIKA KUSINI

[Picha katika ukurasa wa 7]

AMERIKA KUSINI

[Picha katika ukurasa wa 7]

ASIA

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 6]

© Teun Voeten/Panos Pictures; J.R. Ripper/BrazilPhotos

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]

JORGE UZON/AFP/Getty Images; © Frits Meyst/Panos Pictures