Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Jinsi Tunavyokumbuka . . . Vitunguu Saumu!”

“Jinsi Tunavyokumbuka . . . Vitunguu Saumu!”

“Jinsi Tunavyokumbuka . . . Vitunguu Saumu!”

Na mwandishi wa Amkeni! katika Jamhuri ya Dominika

IKIWA ungekuwa mbali na nyumbani na una njaa, ungependa kula chakula gani? Huenda ukakumbuka matunda na mboga zinazokuzwa nchini kwenu, au labda ungefikiria mchuzi wenye ladha nzuri wa nyama au samaki ambao mama yako alikuwa akitayarisha. Lakini je, kitunguu saumu kingefanya udondokwe na mate?

Miaka 3,500 hivi iliyopita, Waisraeli walipokuwa wakivuka nyika ya Sinai walisema hivi: “Jinsi tunavyokumbuka samaki tuliokuwa tukila bure huko Misri, matango na matikiti-maji na vitunguu vya majani na vitunguu na vitunguu saumu!” (Hesabu 11:4, 5) Naam, walitamani vitunguu saumu. Wayahudi walipenda sana vitunguu saumu hivi kwamba kulingana na hekaya fulani, walijiita walaji wa vitunguu saumu.

Ni nini kilichofanya Waisraeli wapende kula vitunguu saumu? Walipokuwa Misri kwa miaka 215, walikula sana vitunguu saumu. Uthibitisho wa akiolojia unaonyesha kwamba muda mrefu kabla ya Yakobo na familia yake kuwasili Misri, Wamisri walikuwa wakikuza kitunguu saumu. Mwanahistoria Mgiriki Herodoto anaripoti kwamba serikali ya Misri ilinunua kiasi kikubwa cha vitunguu, figili, na vitunguu saumu ili kuwalisha watumwa wake waliokuwa wakijenga piramidi. Inaonekana kwamba chakula hicho kilichokuwa na kitunguu saumu kingi, kiliwaongezea nguvu wafanyakazi hao. Wamisri walipomzika Farao Tutankhameni, waliweka vitu vingi vyenye thamani kwenye kaburi lake, kutia ndani vitunguu saumu. Bila shaka, kitunguu saumu hakingeweza kuwasaidia wafu, lakini kimewasaidia sana walio hai.

Dawa Yenye Nguvu

Kwa muda mrefu madaktari wametumia kitunguu saumu kutibu wagonjwa wao. Karne nyingi zilizopita matabibu Wagiriki Hipokrati na Dioskoride walikipendekeza kwa ajili ya kutibu matatizo ya kumeng’enya chakula, ukoma, kansa, vidonda, maambukizo, na matatizo ya moyo. Katika karne ya 19, mwanakemia Mfaransa Louis Pasteur alichunguza kitunguu saumu na kusema kwamba kinaweza kutumiwa kusafisha vidonda. Katika karne ya 20, Albert Schweitzer, mmishonari na daktari maarufu alitumia kitunguu saumu kutibu kuharisha kunakosababishwa na maambukizo ya amiba na magonjwa mengine barani Afrika. Walipoishiwa na dawa za kisasa wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, madaktari Warusi walitumia kitunguu saumu kutibu wanajeshi waliojeruhiwa. Kwa hiyo, kitunguu saumu kiliitwa penisilini ya Warusi. Hivi karibuni, wanasayansi wamechunguza jinsi kitunguu saumu husaidia mfumo wa kuzungusha damu.

Kwa hiyo, kitunguu saumu kinafaa kama chakula na dawa, nacho kina harufu na ladha ya kipekee. Kitunguu saumu kilikuzwa wapi mara ya kwanza? Wataalamu fulani wa mimea wanaamini kilitoka Asia ya kati na kuenea sehemu zote ulimwenguni. Na tuchunguze sehemu fulani maridadi ya mabara ya Amerika ambako kitunguu saumu kinakuzwa kwa wingi.

Kukuza Kitunguu Saumu Huko Constanza

Bonde la Constanza, katika Jamhuri ya Dominika, lina halijoto ya kadiri. Bonde hilo lililozungukwa na milima lina udongo wenye rutuba na mvua nyingi. Constanza ni mahali panapofaa kukuza kitunguu saumu.

Mnamo Septemba au Oktoba, wakulima wa Constanza hulima na kutayarisha mashamba yao, wakiacha mitaro mikubwa iliyotenganishwa na matuta ya udongo yenye upana wa meta moja hivi. Kwenye kila tuta, wao huchimba mitaro mitatu au minne midogo ambapo wanapanda kitunguu saumu. Wakati huohuo, wafanyakazi hutenganisha vidole vya kitunguu saumu kizima. Baada ya kuvilowesha katika maji kwa dakika 30, wafanyakazi hao huvipanda katika mitaro midogo iliyochimbwa. Kitunguu saumu hukua wakati wa majira ya baridi ya kadiri huko Dominika.

Mavuno huanza Machi au Aprili. Wafanyakazi hung’oa vitunguu saumu vilivyokomaa na kuviacha mashambani kwa siku tano au sita. Kisha wao huvikusanya, hukata mizizi na sehemu za juu, na kuweka vitunguu saumu vilivyosafishwa katika kontena zinazoitwa cribas. Wao huanika kontena hizo juani kwa siku moja ili vitunguu saumu vikauke. Baada ya hapo, viko tayari kuuzwa.

Kitunguu Saumu Kidogo, Harufu Kali

Unapokula mchuzi au saladi yenye ladha nzuri, mara moja pua lako hukuambia ikiwa chakula hicho kina kitunguu saumu. Hata hivyo, kwa nini kitunguu saumu hakinuki kabla hakijakatwa? Kitunguu saumu kina kemikali zenye nguvu ambazo huwa zimetenganishwa hadi kinapomenywa, kukatwa, au kupondwa. Unapokata-kata kitunguu saumu, kimeng’enya kinachoitwa alliinase huungana na kemikali inayoitwa alliin. Mara moja mchanganyiko huo hutokeza allicin, kemikali ambayo hutokeza harufu na ladha ya kitunguu saumu.

Unapouma kipande cha kitunguu saumu, ni kana kwamba allicin hulipuka mdomoni mwako. Iwe unapendezwa na harufu hiyo au la, baada ya muda harufu hiyo itajaa kila mahali. Je, unaweza kupunguza harufu ya kitunguu saumu inayotoka mdomoni mwako? Huenda ukajaribu kutafuna kitimiri au karafuu ili kuficha harufu hiyo.

Lakini kumbuka kwamba harufu ya kitunguu saumu katika pumzi yako hutoka hasa kwenye mapafu yako. Unapokula kitunguu saumu, mfumo wako wa kumeng’enya chakula hukisafirisha kwenye damu ambayo hukipeleka kwenye mapafu yako. Unapotoa pumzi, harufu yake kali hutoka. Kwa hiyo kusafisha mdomo na kutafuna kitimiri hakuondoi harufu ya kitunguu saumu. Je, kuna suluhisho la tatizo hilo? La. Lakini ukimfanya kila mtu ale kitunguu saumu, basi hawatatambua kwamba wewe unatoa harufu hiyo!

Katika nchi nyingi watu hawawezi kula chakula ambacho hakina kitunguu saumu. Na hata katika sehemu ambako kitunguu saumu hutumiwa kwa kiasi kidogo, walaji wengi wanaamini kwamba licha ya harufu yake, kitunguu saumu kina manufaa mengi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kukausha kitunguu saumu kilichovunwa

[Picha katika ukurasa wa 23]

Bonde la Constanza

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kwa nini kitunguu saumu hutoa harufu tu baada ya kupondwa?