Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtu Aliyeonyesha Kwamba Dunia Huzunguka

Mtu Aliyeonyesha Kwamba Dunia Huzunguka

Mtu Aliyeonyesha Kwamba Dunia Huzunguka

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Poland

“Kuna ‘waropokaji’ fulani wanaojitwalia jukumu la kuchambua kitabu changu, ingawa hawajui chochote kuhusu hesabu. Hata hawaoni aibu kupotosha maana ya sehemu fulani ya Maandiko Matakatifu ili kutimiza makusudi yao. Wakikosoa na kushambulia kitabu changu; hawanihangaishi hata kidogo nami nayadharau maoni yao na kuyaona kuwa ya kijinga.”

MANENO hayo ya Nikolao Kopeniko yalimlenga Papa Paulo wa 3. Kopeniko aliandika maneno hayo katika dibaji ya kitabu chake kipya On the Revolutions of the Heavenly Spheres, kilichochapishwa mwaka wa 1543. Kuhusu maoni yaliyokuwamo katika kitabu hicho, Christoph Clavius, kasisi Myeswiti wa karne ya 16 alisema: “Nadharia ya Kopeniko ina madai mengi yenye kasoro ambayo hayajathibitishwa.” Martin Luther, Mwanatheolojia Mjerumani alisema hivi: “Mpumbavu huyu atavuruga sayansi yote ya astronomia.”

Nikolao Kopeniko ni nani? Kwa nini maoni yake yalizua ubishi mwingi? Naye ameathirije maoni ya watu leo?

Kijana Aliyekuwa na Hamu ya Kupata Ujuzi

Alizaliwa Februari 19, 1473, huko Toruń nchini Poland, na kuitwa Mikołaj Kopernik. Baadaye alipoanza kuandika vitabu vyake, akaanza kutumia muundo wa Kilatini wa jina lake, yaani, Nikolao Kopeniko. Baba yake, ambaye alikuwa mfanya-biashara huko Toruń alikuwa na watoto wanne; na Nikolao ndiye aliyekuwa kitinda-mimba. Nikolao alipokuwa na umri wa miaka 11, baba yake alikufa. Mjomba wake, Lucas Watzenrode, alimtunza Nikolao na nduguze. Alimsaidia Nikolao kupata elimu, naye alimtia moyo awe kasisi.

Nikolao alianza masomo yake katika mji wa nyumbani kwao lakini baadaye akaendelea na masomo yake huko Chełmno, ambako alijifunza Kilatini na kusoma vitabu vya waandishi wa kale. Alipokuwa na umri wa miaka 18, alihamia Kraków, lililokuwa jiji kuu la Poland. Akiwa huko alijiunga na chuo kikuu, na kusomea astronomia, somo alilopenda. Nikolao alipomaliza masomo yake huko Kraków, mjomba wake ambaye wakati huo alikuwa askofu wa Warmia alimwomba ahamie Frombork, jiji lililokuwa kwenye Bahari ya Baltiki. Watzenrode alitaka mpwa wake awe padri wa dayosisi hiyo.

Hata hivyo, Nikolao aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo alitaka kuendelea na masomo yake naye alimsihi mjomba wake amruhusu asomee sheria za kanisa, tiba, na hesabu katika vyuo vikuu vya Bologna na Padua huko Italia. Akiwa huko Nikolao alishirikiana na mwastronomia Domenico Maria de Novara na mwanafalsafa Pietro Pomponazzi. Mwanahistoria Stanisław Brzostkiewicz anasema kwamba mafundisho ya Pomponazzi “yalipanua maarifa ya kijana huyo mwastronomia.”

Wakati wake wa mapumziko, Kopeniko alisoma sana vitabu vya waastronomia wa kale hivi kwamba alipotambua kwamba baadhi ya vitabu vya Kigiriki havikuwa vimetafsiriwa katika Kilatini alijifunza Kigiriki ili asome maandishi ya awali. Kufikia mwishoni mwa masomo yake, Nikolao alikuwa mwanahisabati, daktari, na pia alikuwa na shahada ya sheria za kanisa. Isitoshe, alikuwa mtaalamu wa lugha ya Kigiriki, akiwa mtu wa kwanza kutafsiri hati fulani ya Kigiriki moja kwa moja hadi Kipolandi.

Atunga Nadharia ya Kimapinduzi

Kopeniko aliporudi Poland, mjomba wake ambaye alikuwa askofu alimpa wadhifa ulioheshimika sana kwa kumteua awe katibu, mshauri na daktari wake binafsi. Kwa makumi ya miaka iliyofuata, Nikolao alikuwa na nyadhifa mbalimbali kanisani na serikalini. Licha ya kazi nyingi aliyokuwa nayo, aliendelea kujifunza kuhusu nyota na sayari na kukusanya uthibitisho wa nadharia yake ya kimapinduzi, iliyodai kwamba dunia sio kitovu cha ulimwengu na kwamba badala yake dunia inazunguka jua.

Nadharia hiyo ilipinga maoni ya Aristotle, mwanafalsafa aliyeheshimiwa sana, nayo haikupatana na nadharia za mwanahisabati Mgiriki Ptolemy. Isitoshe nadharia ya Kopeniko ilikanusha dhana iliyoaminiwa kuwa ya “kweli” kwamba jua huchomoza mashariki, husafiri angani na hatimaye kutua magharibi, huku dunia ikiwa imesimama tuli.

Kopeniko hakuwa wa kwanza kudai kwamba dunia inazunguka jua. Mwastronomia Mgiriki Aristarchus wa Samos alikuwa na maoni hayohayo katika karne ya tatu K.W.K. Wafuasi wa Pythagoras walifundisha kwamba dunia na jua zilikuwa mwendoni zikizunguka moto fulani. Hata hivyo, Ptolemy aliandika kwamba ikiwa dunia inazunguka, “wanyama na vitu vingine vingening’inia hewani, na Dunia ingeanguka ghafula kutoka mbinguni.” Aliongeza kwamba “hata kuwazia tu mambo hayo huyafanya yaonekane kuwa ya kipuuzi.”

Ptolemy aliunga mkono dhana ya Aristotle kwamba dunia imesimama tuli ikiwa kitovu cha ulimwengu nayo imezungukwa na matabaka kadha wa kadha ambamo jua, sayari, na nyota nyingine huwa. Alikata kauli kwamba matabaka hayo yasiyoonekana ndiyo yaliyowezesha sayari na nyota kuzunguka. Kupitia hesabu, Ptolemy alikadiria mizunguko ya sayari angani usiku kwa usahihi kiasi.

Hata hivyo, upungufu katika nadharia ya Ptolemy ndio uliomchochea Kopeniko kutafuta kujua kiini cha mizunguko isiyoeleweka ya sayari. Ili kufafanua nadharia yake, Kopeniko alijenga upya vifaa viliyotumiwa na waastronomia wa kale. Ingawa vifaa hivyo ni duni kwa kulinganishwa na vifaa vya leo, bado vilimwezesha kukadiria umbali kati ya sayari mbalimbali na jua. Alitumia miaka kadhaa akijaribu kukadiria tarehe hususa ambazo waliomtangulia waliona matukio fulani muhimu ya kiastronomia. Akiwa na habari hizo, Kopeniko alianza kutayarisha mswada uliozua ubishi, ambao ulibadili maoni ya watu kwamba dunia ndicho kitovu cha ulimwengu.

Ubishi Kuhusu Mswada Huo

Kopeniko alitumia miaka ya mwisho-mwisho ya maisha yake akiboresha na kuongezea habari na fomyula za hesabu zilizounga mkono nadharia yake. Zaidi ya asilimia 95 ya mswada wake ilikuwa na habari nyingi za kisayansi zilizounga mkono nadharia yake. Mswada wa kwanza uliokuwa umeandikwa kwa mkono ungalipo leo hii, nao uko katika Chuo Kikuu cha Jagiellonian, huko Kraków, Poland. Mswada huo hauna kichwa. Kwa hiyo, mwastronomia Fred Hoyle aandika hivi: “Kwa kweli hatujui jinsi Kopeniko alivyotaka kitabu chake kiitwe.”

Hata kabla ya kitabu chake kuchapishwa, habari zilizomo zilikuwa zimevutia watu kadhaa. Kopeniko alikuwa amechapisha muhtasari mfupi wa dhana zake katika kitabu kilichoitwa Commentariolus. Kwa hiyo, ripoti za utafiti wake zikafika Ujerumani na Roma. Mnamo mwaka wa 1533, tayari Papa Clement wa 7 alikuwa amesikia kuhusu nadharia ya Kopeniko. Na katika mwaka wa 1536, Kadinali Schönberg alimwandikia Kopeniko, akimsihi achapishe dhana zake zote. Georg Joachim Rhäticus, profesa katika Chuo Kikuu cha Wittenberg, Ujerumani, alivutiwa sana na kitabu cha Kopeniko hivi kwamba akamtembelea mwastronomia huyo na kukaa naye kwa miaka miwili. Mwaka wa 1542, Rhäticus alichukua nakala ya mswada huo na kwenda nayo Ujerumani, ambako alimkabidhi mchapishaji anayeitwa Petreius na kasisi msoma-prufu anayeitwa Andreas Osiander.

Osiander alikiita kitabu hicho De revolutionibus orbium coelestium (Mizunguko ya Matabaka ya Mbinguni). Kwa kuongeza maneno “matabaka ya mbinguni,” Osiander alidokeza kwamba kitabu hicho kiliathiriwa na dhana za Aristotle. Pia, Osiander aliandika dibaji ambayo haikuwa na jina lake, na kueleza kwamba nadharia zilizokuwa katika kitabu hicho hazikutokana na imani na si lazima ziwe za kweli. Kopeniko hakupokea nakala ya kitabu hicho kilichochapishwa, kikiwa na mabadiliko ambayo hakuwa ameyaidhinisha, mpaka saa chache kabla ya kifo chake mwaka wa 1543.

Mizunguko—Kitabu cha Kimapinduzi

Mwanzoni, mabadiliko ya Osiander yalikiepusha kitabu hicho na uchambuzi. Baadaye, Galileo, aliyekuwa mwastronomia na mwanafizikia Mwitaliano, aliandika hivi: “Kitabu hicho kilipochapishwa, kilikubaliwa na Kanisa takatifu na watu wamesoma na kujifunza kitabu hicho pasipo kipingamizi chochote dhidi ya mafundisho yake. Sasa, hata hivyo, ingawa mambo yanayoonekana yamethibitisha kwamba dhana hizo zina msingi, kuna watu ambao wangemvunjia heshima mwandishi wa kitabu hicho kabla hata ya kukisoma.”

Walutheri ndio waliokuwa wa kwanza kukiita kitabu hicho, “upuuzi mtupu.” Ingawa mwanzoni Kanisa Katoliki halikutoa maoni yake kuhusu kitabu hicho, liliamua kwamba kitabu hicho kinapingana na mafundisho yake rasmi na katika mwaka wa 1616 kitabu hicho cha Kopeniko kikaongezwa katika orodha ya vitabu vilivyokuwa vimepigwa marufuku. Kilibaki katika orodha hiyo hadi mwaka wa 1828. Katika dibaji ya kitabu kilichotafsiriwa katika Kiingereza, Charles Glenn Wallis aeleza hivi: “Mgawanyiko kati ya Wakatoliki na Waprotestanti ulifanya vikundi vyote viwili vihofu kashfa ambayo ingewafanya wafuasi wa Kanisa wakose kuiheshimu Biblia, na hivyo waliyafuata Maandiko neno kwa neno bila kuzingatia maana yake na kushutumu maelezo yoyote yaliyoonekana kana kwamba yanapinga jinsi walivyoielewa Biblia.” * Galileo aliandika hivi kuhusu kupingana kwa nadharia ya Kopeniko na mafundisho ya Biblia: “[Kopeniko] hakuipuuza Biblia lakini alijua vizuri kwamba ikiwa mafundisho yake yangethibitishwa, hayangepingana na Maandiko ikiwa yangeeleweka vizuri.”

Leo, Kopeniko anatambuliwa na wengi kuwa mwanzilishi wa astronomia ya kisasa. Ni kweli kwamba maelezo yake kuhusu ulimwengu yalirekebishwa na kuboreshwa na wanasayansi wa baadaye kama vile Galileo, Kepler, na Newton. Hata hivyo, mtaalamu wa astronomia na fizikia, Owen Gingerich, anasema hivi: “Kopeniko ndiye aliyetuonyesha jinsi dhana za kisayansi zinavyoweza kubadilika haraka.” Kwa kufanya utafiti, kuchunguza, na kupiga hesabu, Kopeniko alipindua dhana zilizokuwa na kasoro za kidini na za kisayansi ambazo zilikuwa zimetia mizizi. Alibadili maoni ya watu kwa kuonyesha kwamba dunia wala si jua ndiyo iliyokuwa ikizunguka.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 23 Kwa mfano, simulizi la Yoshua 10:13, linalozungumzia kusimama kwa jua, lilitumiwa kudai kwamba jua ndilo huzunguka wala si dunia.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Kitabu On the Revolutions of the Heavenly Spheres

Kopeniko aligawanya kitabu chake katika sehemu sita. Baadhi ya mambo makuu ya kitabu chake yameorodheshwa hapa.

● Dunia yetu ni mmojawapo wa “wasafiri” wengi ambao safari yao inaongozwa na ‘jua ambalo limeketi kwenye kiti chake cha ufalme.’

● Sayari zinazunguka jua kuelekea upande mmoja. Dunia ni mojawapo ya sayari hizo, ikizunguka katika mhimili wake wenyewe mara moja kwa siku na kulizunguka jua mara moja kila mwaka.

● Zikiwa zimepangwa kwa kutegemea umbali kutoka kwa jua, Zebaki ndiyo iliyo karibu zaidi, ikifuatiwa na Zuhura, kisha Dunia na mwezi wake, halafu Mihiri, Sumbula, na hatimaye Sarateni.

[Hisani]

Title page of Copernicus’ work: Zbiory i archiwum fot. Muzeum Okrȩgowego w Toruniu

[Picha katika ukurasa wa 14]

Darubini iliyotumiwa na Kopeniko

[Hisani]

Zbiory i archiwum fot. Muzeum Okrȩgowego w Toruniu

[Picha katika ukurasa wa 15]

Vifaa katika chumba cha Kopeniko cha utafiti katika kituo chake cha kutazama angani kilicho Frombork, Poland

[Hisani]

Zdjecie: Muzeum M. Kopernika we Fromborku; J. Semków

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mfumo unaoonyesha kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu

[Hisani]

© 1998 Visual Language

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mfumo unaoonyesha kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu

[Hisani]

© 1998 Visual Language

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mfumo wa jua kama unavyofahamika leo