Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Barafu Inayoyeyuka Inasaidia Akiolojia

Barafu inayoyeyuka inafichua mabaki ya vitu vya kale yanayowapendeza sana wanahistoria, lasema gazeti Der Spiegel la Ujerumani. Mwaka wa 1999 katika Milima ya Rocky huko Kanada, barafu iliyoyeyuka ilifichua mwili wa mwanamume mmoja Mhindi, aliyekufa miaka 550 iliyopita. Hata hivyo, mabaki mengi ya vitu vya kale yamepatikana katika Milima ya Alps. Kwa mfano, mwili wa mwanamume mmoja anayedhaniwa kuwa alimwacha mpenzi wake na mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa wakiteseka mwaka wa 1949, umepatikana hivi majuzi. Alikuwa ameanguka ndani ya shimo, na pete za uchumba zilikuwa mkobani mwake. Kulingana na Harald Stadler, mkuu wa akiolojia ya barafu katika Chuo Kikuu cha Innsbruck huko Austria, mradi wa mwanahistoria yeyote ni kupata vitu vinavyohusiana na Hannibal, yule kamanda maarufu wa Carthage aliyepitia Milima ya Alps na tembo 37. Anasema: “Mfupa wa tembo utawavutia wengi.”

Vijana Wanaocheza Kamari

Kulingana na Kituo cha Kimataifa Kinachoshughulikia Vijana Wanaocheza Kamari kwenye Chuo Kikuu cha McGill, “zaidi ya nusu ya vijana wa Kanada wenye umri wa miaka 12 hadi 17 hucheza kamari ili kujifurahisha, asilimia 10 hadi 15 wanakabili hatari ya kuwa wachezaji sugu wa kamari na asilimia 4 hadi 6 huonwa kuwa wachezaji sugu,” laripoti gazeti National Post la Toronto. Mara nyingi vijana hao huanza kutamani kucheza wakiwa wachanga sana wanapopewa zawadi za tiketi za bahati nasibu au kutumia Intaneti kucheza kamari. Hivyo, kulingana na watafiti, vijana wengi wa Kanada sasa wanacheza kamari zaidi ya wanavyojihusisha katika mazoea mengine sugu, kama vile kuvuta sigara au kutumia dawa za kulevya. Wakuu wa elimu wanatumaini kwamba miradi ya kuwazuia vijana kucheza kamari katika shule za sekondari za Kanada zitafaulu kudhibiti tatizo hilo.

Ufaransa Ilikumbwa na Joto Kali

Halijoto huko Ufaransa zilifikia kiwango cha juu zaidi siku 12 za kwanza za mwezi wa Agosti 2003. Tangu halijoto zilipoanza kurekodiwa mwaka wa 1873, Paris haijawahi kuwa na joto kali hivyo wakati wa kiangazi. “Kulingana na [shirika la utabiri wa hali ya hewa la Ufaransa], kipindi hicho cha joto jingi kilikuwa kikali zaidi na kilidumu kwa muda mrefu kuliko vipindi vingine vya joto vilivyowahi kutukia huko,” lasema gazeti la mambo ya asili Terre sauvage. Katika miezi miwili tu, mto mmoja wa barafu katika Milima ya Pyrenees, kwenye mpaka wa kusini wa Ufaransa, ulipungua kwa meta 50 hivi. Kulingana na mtaalamu wa mito ya barafu, Pierre René, “kwa muda wa miaka 150, ukubwa wa mito ya barafu kwenye Milima ya Pyrenees umepungua kutoka kilometa 25-30 za mraba hadi kilometa 5 za mraba.” Je, hilo linaonyesha kuna ongezeko la joto duniani? Wataalamu wana maoni yanayotofautiana. Hata hivyo, wataalamu fulani wa hali ya hewa wanasema kwamba huenda vipindi vya joto kali vikaongezeka katika miaka inayokuja, na hilo ni jambo linalosababisha wasiwasi kwa sababu inakadiriwa kwamba katika majira ya kiangazi yaliyopita joto kali lilisababisha vifo 15,000 hivi huko Ufaransa.

Wanaume Wanaoshuka Moyo

“Mojawapo ya mambo ya kusikitisha zaidi kuhusu kushuka moyo ni kwamba watu hudhania kimakosa kuwa ni ‘ugonjwa unaowakumba wanawake’ hasa, na kwamba ‘wanaume halisi’ hawawezi kuupata,” lasema gazeti The Star la Johannesburg. “Wataalamu wanasema kwamba ugonjwa huo hauonekani wazi katika wanaume kwa sababu wao hawaendi hospitalini mara nyingi kama wanawake, hivyo hawapati nafasi ya kueleza matatizo yao” na “hisia zao.” Hivyo, madaktari wanafahamu zaidi dalili za wanawake walioshuka moyo. Jarida JAMA linaeleza kwamba “dalili za wanawake walioshuka moyo ni tofauti sana na za wanaume.” Ni nini baadhi ya dalili za wanaume walioshuka moyo? Hasira, uchovu, kuchokozeka haraka, jeuri, kushindwa kufanya kazi vizuri, na kujitenga na wapendwa na marafiki. Jarida Reader’s Digest la Afrika Kusini linasema: “Haimaanishi kwamba nyakati zote wanaume walioshuka moyo huwa na huzuni.”

Makasisi wa Katoliki na Ujuzi wa Biblia

“Makasisi wanaijua Biblia vizuri kadiri gani?” Swali hilo liliulizwa na Andrea Fontana, ambaye ni kasisi na msimamizi wa Ofisi ya Dayosisi ya Katekisimu huko Turin. Akiandika katika gazeti la Kikatoliki la Italia linaloitwa Avvenire, Fontana alisema kwamba alifikiria swali hilo wakati “muumini mmoja alipomwuliza ikiwa dayosisi hiyo ilikuwa ikitoa mafunzo ya Biblia.” Katika kanisa ambalo muumini huyo alihudhuria, “Maandiko Matakatifu hayakutajwa kamwe.” Kwa kujibu Fontana aliandika: “Kusema kweli, inasikitisha kwamba baada ya [makasisi] kuhudhuria seminari zao, ni wachache wanaoendelea kujifunza Biblia. . . . Waumini wengi hupata nafasi ya kusikiliza habari fulani kutoka kwa Biblia wakati wa mahubiri ya Jumapili tu.” Muumini huyo alisema kwamba “alishirikiana na Mashahidi wa Yehova ili ajifunze mengi zaidi.”

Matatizo ya Kunenepa Kupita Kiasi

Idadi ya watu wanene kupita kiasi inaongezeka nchini Marekani. Kulingana na makadirio kutoka katika Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, katika mwaka wa 1991 asilimia 12.5 ya watu wazima wa Marekani walikuwa wamenenepa kupita kiasi, lakini kufikia mwaka wa 2003 idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kufikia asilimia 20. Ongezeko hilo limeathiri biashara kadhaa. Gazeti The New York Times linasema: “Kama vile mashirika ya ndege yalivyoonywa mnamo Mei [2003] kwamba uzito wa abiria umeongezeka kuliko ilivyokuwa na hivyo kuombwa kubadili viwango vya uzito vinavyohitajiwa, mashirika yanayotoa huduma za mazishi yamebadilisha vifaa vyao ili kutengeneza majeneza yanayowatoshea Wamarekani wanene.” Ijapokuwa jeneza la kawaida huwa na upana wa sentimeta 61, sasa majeneza yenye upana wa sentimeta 124 yanapatikana na yametengenezwa ili kustahimili uzito. Hata ukubwa wa “vifuniko vya makaburi, makaburi, majeneza na hata sepetu za mashine zinazotumiwa kuchimba makaburi” umeongezwa. “Watu wanaendelea kunenepa na wanakufa wakiwa wanene, na mashirika yanalazimika kubadilika kulingana na hali hiyo,” anasema Allen Steadham, mkurugenzi mkuu wa kikundi cha kuwatetea watu wanene.

“Bahari ya Chumvi Inaendelea Kupungua”

Shirika la Associated Press linaripoti kwamba “Bahari ya Chumvi inaendelea kupungua na ni mradi mkubwa tu wa uhandisi unaoweza kuiokoa.” Kwa kuwa bahari hiyo ina chumvi nyingi, viumbe wa baharini hawawezi kuishi humo. Bahari ya Chumvi ndilo eneo la maji lililo chini zaidi duniani, likiwa meta 400 chini ya usawa wa bahari. “Kwa maelfu ya miaka, kiasi cha maji [yanayoingia na kuchukua mahali pa maji yanayobadilika kuwa mvuke] kilidumishwa na chanzo cha pekee cha maji ya Bahari ya Chumvi, yaani, Mto Yordani,” yasema makala hiyo. “Hata hivyo, katika miongo ya karibuni, Israeli na Jordan zimekuwa zikitumia maji ya Mto Yordani kumwagilia maji mashamba makubwa yaliyo karibu na mto huo mwembamba unaogawanya nchi hizo mbili, na hivyo kuzuia maji yasiongezeke katika Bahari ya Chumvi.” Uchunguzi mmoja wa Israeli unasema kwamba, hatua yoyote isipochukuliwa, kiwango cha maji kitaendelea kupungua kwa meta moja kila mwaka na kuathiri sana maeneo ya karibu, kutia ndani wanyama wa pori na mimea. Tayari ukame wa miaka mitano unaathiri Bahari ya Chumvi.