Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wadudu Wasumbufu Wanaosafisha Maji

Wadudu Wasumbufu Wanaosafisha Maji

Wadudu Wasumbufu Wanaosafisha Maji

Katikati ya miaka ya 1980 koa anayetoshana na ukucha anayeitwa kome-milia alifika bila kukusudia katika Maziwa Makuu ya Amerika Kaskazini kutoka Ulaya ndani ya maji yanayoimarisha meli. Gazeti la Kanada, Maclean’s lasema kwamba koa “wanawakilisha viumbe wavamizi wa majini.” Kwa nini?

Kome wa kike anaweza kutaga mayai 500,000 kwa mwaka. Isitoshe, makundi haya makubwa ya kome hujishikiza kwenye sehemu yoyote ngumu. Kome wapatao 700,000 wanaweza kukaa katika eneo la meta moja ya mraba. Kwa hiyo, wanaziba mifereji au mabomba yanayoingiza maji katika mitambo ya maji na vituo vya kuzalisha umeme. Pia huwatia hasara wenye mashua na wenye bandari.

Hata hivyo, viumbe hao wenye sifa mbaya wana faida. Huenda kome-milia wakatumiwa kulinda afya yetu hivi karibuni. Wanasayansi wa mazingira, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakichunguza maumbile na utendaji wa viumbe hao, wanajua kwamba kome-milia ni msafishaji wa maji anayeweza kustahimili mengi. Mtaalamu wa vimelea Thaddeus K. Graczyk, wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Baltimore, na mwanasayansi mtafiti wa shirika la Mazingira ya Kanada, Yves de Lafontaine, wa Montreal, wameshirikiana katika uchunguzi wa koa. Gazeti Maclean’s laripoti kwamba kome-milia anaweza kumeza “vitu vinavyoelea kama vile tributyltin, kemikali yenye sumu inayopatikana katika rangi inayopakwa meli, kimelea hatari kinachoitwa Cryptosporidium na bakteria inayoitwa E. coli.”

Kimelea cha Cryptosporidium kinatoshana na chembe nyekundu ya damu ya binadamu na si rahisi kukitoa katika maji ya kunywa. Dawa nyingi za kuua viini kama vile klorini na ozoni haziwezi kukiua. “Hata hivyo kome-milia wanaweza kuchuja kwa urahisi chembe zenye ukubwa huo,” lasema gazeti Maclean’s. Watafiti wanasema kwamba “katika miezi ya joto, kila kome aliyekomaa anaweza kuchuja lita moja ya maji kwa siku na kuondoa mwani, chembe za madini, vichafuzi, viini na bakteria nyingine zinazoweza kuhatarisha uhai.” Wanakadiria kwamba kundi linaloweza kupatikana katika eneo la meta moja ya mraba linaweza kumeza vimelea milioni 13 kwa muda wa saa mbili hivi.

Kwa kweli, mambo ambayo wanasayansi wanajifunza kuhusu uwezo wa kusafisha wa koa huyu ni ushuhuda wa ajabu wa kwamba uumbaji wote wa Mungu ni mkamilifu.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

Fingers holding zebra mussel: U.S. Geological Survey; all other mussels: © Rob and Ann Simpson/Visuals Unlimited; Cryptosporidium: H.D.A. Lindquist, U.S. EPA