Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kamari Hupendwa Ulimwenguni Pote

Kamari Hupendwa Ulimwenguni Pote

Kamari Hupendwa Ulimwenguni Pote

JOHN, aliyelelewa huko Scotland, alitamani sana kushinda zawadi katika mchezo wa bahati nasibu. Anasema hivi: ‘Nilinunua tiketi ya kushinda bahati nasibu kila juma. Tiketi hiyo haikuwa pesa nyingi, lakini ilinipa tumaini la kupata kila kitu ambacho nilikuwa nikitamani.’

Kazushige, anayeishi Japani, alipenda sana mashindano ya mbio za farasi. Anasema hivi: “Nilifurahia sana kucheza kamari pamoja na rafiki zangu kwenye uwanja wa mbio za farasi, na nyakati nyingine nilishinda pesa nyingi.”

Linda, anayeishi Australia, anasema hivi: ‘Nilipenda sana kucheza kamari aina ya bingo. Kila juma zoea hilo lilinigharimu dola 30 za Marekani, lakini nilisisimuka sana niliposhinda zawadi.’

John, Kazushige, na Linda, waliiona kamari kuwa tafrija isiyodhuru sana. Mamilioni ya watu kotekote duniani wana maoni hayohayo. Mahojiano yaliyofanywa mwaka wa 1999 yalionyesha kwamba thuluthi mbili za Wamarekani waliona kucheza kamari kuwa zoea linalofaa. Wamarekani walitumia dola bilioni 50 hivi za Marekani katika michezo halali ya kamari mwaka wa 1998. Hizo ni pesa nyingi kuliko kiasi walichotumia kununua tiketi za sinema, kutazama michezo, na burudani mbalimbali, na kununua kaseti za muziki na michezo ya video.

Kulingana na uchunguzi wa hivi majuzi, zaidi ya asilimia 80 ya Waaustralia walicheza kamari angalau mara moja katika kipindi cha mwaka mmoja, na asilimia 40 walicheza kamari kila juma katika kipindi hicho. Watu wazima katika nchi hiyo, hutumia dola 400 za Marekani kwa wastani kila mwaka katika michezo ya kamari. Kiasi hicho ni maradufu ya kiasi ambacho Watu wa Ulaya na Wamarekani hutumia. Kwa hiyo, Waaustralia ni miongoni mwa watu wanaopenda kucheza kamari zaidi ulimwenguni.

Wajapani wengi wameshindwa kudhibiti zoea la kucheza pachinko, nao hutumia mabilioni ya pesa kila mwaka katika mchezo huo wa kamari. Wabrazili hutumia dola bilioni 4 za Marekani katika michezo ya kamari kila mwaka, na kiasi kikubwa cha pesa hizo hutumiwa kununua tiketi za kushinda bahati nasibu. Hata hivyo, si Wabrazili pekee wanaopenda michezo ya bahati nasibu. Hivi majuzi, gazeti la Public Gaming International lilikadiria kwamba kuna “michezo 306 ya bahati nasibu katika nchi 102.” Naam, ulimwenguni pote watu hupenda kucheza kamari. Jambo ambalo kwa maoni ya watu fulani ni lenye faida kubwa.

Sharon Sharp, aliye mwakilishi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchezaji wa Kamari wa Umma, anasema kwamba kuanzia mwaka wa 1964 hadi 1999 huko Marekani, ‘serikali ilipata faida ya dola bilioni 125 hivi kutokana na michezo ya bahati nasibu, na sehemu kubwa ya faida hiyo imekuwa ikiingia tangu mwaka wa 1993.’ Kiasi kikubwa cha fedha hizo kilikusudiwa kutumiwa hasa kwa ajili ya elimu, mbuga za taifa, na majengo ya michezo. Pia, kampuni za kamari huajiri watu wengi. Kwa mfano, huko Australia kuna zaidi ya kampuni 7,000 za kamari ambazo zimewaajiri wafanyakazi wapatao 100,000.

Kwa hiyo, wale wanaotetea uchezaji wa kamari husema kwamba mbali na kuwatumbuiza watu, kampuni halali za kamari huwaajiri watu, huiletea serikali faida, nazo huboresha uchumi unaoshuka.

Kwa hiyo, watu wengi hujiuliza, ‘Kuna ubaya gani kucheza kamari?’ Huenda ukabadili maoni yako kuhusu kucheza kamari baada ya kupata jibu katika makala zinazofuata.

[Picha katika ukurasa wa 3]

John

[Picha katika ukurasa wa 3]

Kazushige

[Picha katika ukurasa wa 3]

Linda