Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?

Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?

Kuna Ubaya Gani Kucheza Kamari?

“Waaustralia 290,000 hivi wana tatizo la kucheza kamari, na jambo hilo husababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 3 za Marekani kila mwaka. Hiyo ni hasara kubwa kwa watu wenye tatizo hilo na vilevile kwa wale watu wapatao milioni 1.5 wanaoathiriwa moja kwa moja kwa sababu ya kufilisika, talaka, kujiua, na wakati wa kazi unaopotea bure.”—J. Howard, waziri mkuu wa Australia, mwaka wa 1999.

JOHN, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, ana tatizo la kucheza kamari. * Alihamia Australia na akamwoa Linda aliyekuwa pia mchezaji kamari. Tamaa ya John ya kucheza kamari ilizidi. Anasema hivi: “Niliacha kununua tiketi za kushinda bahati nasibu na kuanza kucheza kamari kwenye uwanja wa mbio za farasi na katika nyumba za kamari. Muda si muda, nilikuwa nikicheza kamari karibu kila siku. Nyakati nyingine nilipoteza mshahara wote na nilikosa fedha za kulipa mkopo wa nyumba na za kulisha familia. Hata niliposhinda fedha nyingi, niliendelea kucheza kamari. Nilisisimuka sana niliposhinda na hiyo ndiyo iliyonifanya nisiweze kuacha kucheza.”

Watu wengi wana tatizo kama la John. Ni kana kwamba jamii nzimanzima zimeshikwa na kichaa cha kucheza kamari. Gazeti la USA Today lilisema kwamba kati ya mwaka wa 1976 na 1997, kiasi kilichotumiwa katika michezo halali ya kamari huko Marekani kiliongezeka kwa asilimia 3,200. Hilo lilikuwa ongezeko kubwa sana.

Gazeti la The Globe and Mail la Kanada linasema kwamba “hapo awali kucheza kamari kulionwa kuwa jambo baya. Leo, zoea hilo huonwa na watu wengi kuwa tafrija isiyo na ubaya wowote.” Likitaja sababu moja inayowafanya watu wabadili maoni, gazeti hilo linasema: “Maoni ya watu yamebadilika moja kwa moja kwa sababu ya kampeni inayodhaminiwa na serikali ya Kanada ya kuwachochea watu wacheze kamari. Huenda kampeni hiyo iligharimu serikali ya Kanada pesa nyingi na kuchukua muda mrefu kuliko kampeni nyingine yoyote katika historia ya nchi hiyo.” Jitihada za kuendeleza kamari zimewaathiri watu kwa njia gani?

Watu Wengi Wana Tatizo la Kucheza Kamari

Kadirio lililofanywa na Idara ya Mazoea Sugu ya Chuo cha Tiba cha Harvard lilionyesha kwamba mwaka wa 1996 kulikuwa na “Wamarekani milioni 7.5 waliokuwa na tatizo la kucheza kamari na wachezaji sugu,” na vilevile “vijana Wamarekani milioni 7.9 walikuwa na matatizo hayohayo.” Kadirio hilo lilitiwa ndani ya ripoti iliyotayarishwa na Tume ya Kitaifa Inayochunguza Athari za Kamari (NGISC) na kusomwa mbele ya Bunge la Marekani. Ripoti hiyo ilionyesha kwamba huenda ikawa idadi ya watu walio na tatizo la kucheza kamari huko Marekani ni kubwa kuliko ilivyokadiriwa.

Serikali ya Marekani hutumia mabilioni ya dola kila mwaka ili kuwasaidia watu ambao wamepoteza kazi zao, wale ambao wamekuwa wagonjwa, na wale wanaohitaji usaidizi wa kifedha kwa sababu ya kucheza kamari, na ili kuwasaidia wachezaji sugu kuacha zoea hilo. Hata hivyo, mbali na gharama hiyo kubwa ya kifedha, tatizo kubwa zaidi ni magumu na mateso ambayo watu wenye tatizo la kucheza kamari huwaletea watu wa familia, marafiki, na wafanyakazi wenzao. Magumu hayo husababishwa na wizi, udanganyifu, kujiua, ujeuri nyumbani, na kuwatenda watoto vibaya. Uchunguzi mmoja huko Australia ulionyesha kwamba kwa kila mtu mmoja aliye na tatizo la kucheza kamari, watu kumi huathiriwa moja kwa moja. Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti huko Marekani inasema kwamba “asilimia 50 ya wenzi wa ndoa na asilimia 10 ya watoto hupigwa na mchezaji sugu wa kamari.”

Zoea Linaloambukizwa

Inaonekana kwamba watoto walio na wazazi wenye tatizo la kucheza kamari wanaweza kuambukizwa zoea hilo. Ripoti ya tume ya NGISC inasema hivi: ‘Yaelekea kwamba watoto wa watu wenye tatizo la kucheza kamari mara nyingi huwa na tabia mbaya kama vile kuvuta sigara, ulevi, na kutumia dawa za kulevya. Na kuna uwezekano mkubwa kwamba wao pia watakuwa na tatizo la kucheza kamari au watakuwa wachezaji sugu.’ Ripoti hiyo inaongeza kwamba ‘yaelekea kuna uwezekano mkubwa kwa vijana wanaocheza kamari kushindwa kudhibiti zoea hilo au kuwa wachezaji sugu hatimaye kuliko vile ilivyo kwa watu wazima wanaocheza kamari.’

Dakt. Howard J. Shaffer, msimamizi wa Idara ya Mazoea Sugu ya Chuo cha Tiba cha Harvard, anasema hivi: ‘Imethibitishwa kwamba idadi ya vijana wanaocheza michezo haramu ya kamari inaongezeka kwa kiwango kilekile au hata inazidi ile ya vijana wanaocheza michezo ya kamari iliyohalalishwa.’ Alisema hivi kuhusu uwezekano wa wachezaji sugu wa kamari kutumia Internet kwa njia mbaya: “Kama vile kokeini kali aina ya crack ilivyo hatari kuliko kokeini ya kawaida, ndivyo michezo ya kamari kwenye Internet itakavyokuwa na matokeo mabaya kuliko michezo ya kawaida ya kamari.”

Kucheza kamari huonwa mara nyingi kuwa tafrija isiyodhuru. Lakini zoea la kucheza kamari linaweza kuwatawala vijana sawa na dawa za kulevya, nalo linaweza kuwaingiza katika uhalifu. Uchunguzi mmoja uliofanywa Uingereza ulionyesha kwamba “asilimia 46 [ya vijana waliocheza kamari] waliiba kutoka kwa familia yao” ili waweze kuendelea kucheza.

Hata hivyo, shirika moja maarufu la michezo ya kamari linatetea uchezaji wa kamari kwa kusema hivi: “Wamarekani wengi wanaopenda kucheza kamari hawaathiriwi hata kidogo.” Huenda ukaona kwamba kucheza kamari hakuathiri hali yako ya kiuchumi wala afya yako. Lakini, vipi hali yako ya kiroho? Je, kuna sababu nzuri za kuepuka kucheza kamari? Makala inayofuata itajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Ona sanduku “Je, Nina Tatizo la Kucheza Kamari?” kwenye ukurasa wa 4 na 5.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Je, Nina Tatizo la Kucheza Kamari?

Kulingana na Shirika la Madaktari wa Akili la Marekani, dalili zinazotajwa kwenye ukurasa wa 5 zinaweza kukusaidia kutambua zoea sugu la kucheza kamari. Wataalamu wengi hukubali kwamba mtu mwenye dalili kadhaa ana tatizo la kucheza kamari na mtu aliye na mojawapo ya dalili hizo anaelekea kuwa na zoea hilo.

Kufikiria kamari daima Unafikiri daima kuhusu kucheza kamari, unarudia akilini michezo iliyotangulia, unapanga kucheza tena, au unafikiria njia za kupata fedha ambazo unahitaji kucheza.

Kutosisimuka Unahitaji kutumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha unapocheza ili usisimuke.

Athari za Kujaribu Kuacha Unaudhika au unakasirika haraka unapojaribu kupunguza muda wa kucheza au kuacha kucheza.

Kuepa matatizo Unacheza kamari ili kuepa matatizo au kutuliza hisia za kushindwa, hatia, wasiwasi, au kushuka moyo.

Kulipia hasara Baada ya kupoteza pesa katika kamari, unarudi siku nyingine ili kulipia hasara, yaani, kupata tena pesa ulizopoteza.

Kusema uwongo Unawadanganya watu wa familia yako, madaktari, au watu wengine ili wasijue muda unaotumia kucheza kamari.

Kushindwa kudhibiti zoea Umejaribu tena na tena kuacha lakini umeshindwa, umeshindwa kudhibiti zoea la kucheza kamari au kupunguza muda unaotumia kucheza kamari.

Matendo ya uhalifu Umefanya matendo ya uhalifu, kama vile ulaghai, wizi, au udanganyifu ili upate fedha za kutumia katika michezo ya kamari.

Kupoteza marafiki wa karibu Umehatarisha au kuharibu uhusiano mzuri pamoja na rafiki wa karibu, au umepoteza nafasi fulani ya kupata elimu au kazi, kwa sababu ya kucheza kamari.

Kukopa Umeomba mkopo ili kulipia madeni yaliyosababishwa na kucheza kamari.

[Hisani]

Chanzo: National Opinion Research Center at the University of Chicago, Gemini Research, na The Lewin Group.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Ujumbe wa Matangazo ya Michezo ya Bahati Nasibu

Watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Duke, nchini Marekani, walisema hivi katika ripoti moja ambayo walituma kwa Tume ya Kitaifa Inayochunguza Athari za Kamari: “Matangazo yanayowatia watu moyo kununua tiketi za michezo ya bahati nasibu . . . yanaweza kuonwa kuwa elimu ya maadili. Elimu hiyo inafundisha kwamba kucheza kamari si hatari na hata ni jambo jema.” Matangazo ya michezo ya bahati nasibu huwaathiri watu jinsi gani? Ripoti hiyo inasema hivi: ‘Hatutii chumvi tunaposema kwamba matangazo ya bahati nasibu huwadanganya watu yanapoahidi kwamba ufanisi maishani hutokana na kuchagua nambari bora. Huenda “elimu” hiyo inayopotosha, ambayo inaendelezwa na makampuni ya michezo ya bahati nasibu, hatimaye itapunguza mapato ya serikali kwa kufanya uchumi ushuke. Matangazo ya kuwachochea watu kucheza kamari yatafanya uchumi ushuke hasa ikiwa yatawafanya watu washindwe kufanya kazi, washindwe kuweka akiba ya fedha, na washindwe kutumia fedha kwa ajili ya elimu au kujifunza kazi. Kwa vyovyote vile, hatutaki kuwafundisha watoto wetu kwamba mafanikio maishani hutegemea kuchagua nambari bora katika mchezo fulani wa kamari.’

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Inawezekana Kucheza Kamari Nyumbani

Sasa, badala ya kujenga nyumba za michezo ya kamari, mashirika ya michezo ya kamari yanatumia pesa chache zaidi kuwawezesha watu kucheza kamari nyumbani kwao kwenye vituo vya Internet. Katikati ya miaka ya 1990 kulikuwa na vituo 25 hivi vya kucheza kamari kwenye Internet. Mnamo mwaka wa 2001 kulikuwa na vituo zaidi ya 1,200, na mapato yanayotokana na kucheza kamari kwenye Internet yamekuwa yakiongezeka maradufu kila mwaka. Vituo vya kucheza kamari kwenye Internet vilichuma faida ya dola milioni 300 za Marekani mwaka wa 1997. Mapato ya mwaka wa 1998 yalikuwa dola milioni 650. Ripoti moja ya shirika la habari la Reuters inasema kwamba katika mwaka wa 2000 vituo vya kucheza kamari kwenye Internet vilichuma dola bilioni 2.2, na mapato “yanatarajiwa kuongezeka hadi dola bilioni 6.4” kufikia mwaka wa 2003.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Familia za watu walio na tatizo la kucheza kamari zinaweza kukosa pesa za kununua chakula

[Picha katika ukurasa wa 7]

Idadi ya vijana wanaocheza kamari inaongezeka kwa haraka

[Picha katika ukurasa wa 8]

Kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wa watu walio na tatizo la kucheza kamari watakuwa na tatizo hilohilo