Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Huchukua Muda Mrefu Sana Kukomaa!

Huchukua Muda Mrefu Sana Kukomaa!

Huchukua Muda Mrefu Sana Kukomaa!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA

KWA nini watalii husafiri kwa gari kwa muda wa saa mbili au tatu kutoka kwenye jiji la La Paz lililoko kwenye milima ya Andes na kuvuka nyanda kame ya Altiplano hadi kwenye eneo lisilo na watu la Comanche? Kwa nini wataalamu wa mimea kutoka sehemu zote ulimwenguni hutembelea mlima huo uliozingirwa na milima mikubwa?

Wao hufanya hivyo ili waone mmea mkubwa zaidi na wenye kustaajabisha zaidi kati ya mimea yote ya milima ya Andes. Mmea huo unaitwa Puya raimondii. Ukitembelea eneo hilo kati ya miezi ya Septemba na Desemba, huenda ukaona maua yenye kupendeza sana. Watu fulani husema kwamba maua hayo huchanuka baada ya miaka mia moja.

Mmea wa Puya raimondii hukua tu katika sehemu chache za Milima ya Andes. Kwa kuwa mmea huo hauna zile nyuzinyuzi ngumu za miti na vichaka, wataalamu wa mimea huuainisha kuwa mmea unaotokeza mbegu. Hata hivyo, mmea huo ni mkubwa sana! Mmea huo mkubwa huwa mrefu sana na una majani membamba yenye miiba mingi. Ukichunguza majani hayo, utaona kwamba ndege wengi wadogo hunaswa hapo. Nafasi nyembamba zilizopo kati ya majani huwa na mizoga mikavu ya ndege walionaswa. Huenda ndege hao walinaswa walipokuwa wakimtoroka mwewe, kisha wakadungwa na miiba hiyo hatari.

Huenda ukapendezwa hasa na maua ya mmea huo. Japo kuna mimea mingi ya aina hiyo katika sehemu hiyo, kwa kawaida utapata kwamba mmea mmoja au miwili tu ndiyo imechanua.

Inapendeza sana kuona mmea huo mkubwa ukiwa umechanua. Mmea huo una jani lenye miiba ambalo ni refu kuliko mengineyo yote ulimwenguni. Maelfu ya maua ya rangi ya manjano huchanuka kwenye jani hilo kufikia kimo cha meta kumi—juu zaidi kuliko jengo la orofa tatu! Mmea huo mrefu huvutia sana huku ukiwa umeshikamana na miamba.

Lakini, jambo la kuhuzunisha ni kwamba mmea wa Puya raimondii uko katika hatari ya kutoweka kabisa. Haijulikani ni kwa nini watu hupenda kuteketeza mmea huo. Inakisiwa kuwa wanafanya hivyo ili kufurahia kuona moto mkubwa ukiwaka, kupata joto wakati wa baridi, au kwa sababu wanahofu kwamba kondoo watanaswa na kufa katika majani yake yenye miiba. Hata hivyo, mmea huo umeendelea kusitawi licha ya moto, baridi kali, pepo, jua kali, na ukosefu wa udongo. Hilo linawezekanaje?

Mmea wa Puya raimondii ni mojawapo ya aina 2,000 hivi za mimea ya bromeliad ambayo husitawi mahala ambako mimea mingine haisitawi. Aina zote hizo isipokuwa aina moja hupatikana katika mabara ya Amerika. Sawa na mmea wa puya, mimea mingi kati ya aina hizo huwa na mizizi. Kusudi kuu la mizizi ni kuimarisha mimea hiyo. Majani ya mimea hiyo huwa na magamba madogo ambayo huiwezesha kufyonza mvuke kutoka hewani badala ya kutoka ardhini. Pia, kunapokuwa na umande au mvua, mmea huo huhifadhi maji katikati, kwa ajili yake na vilevile viumbe wengine wadogo. Lakini kati ya mimea yote ya bromeliad, mmea wa Puya raimondii ndio mkubwa zaidi.

Mmea huo, unaoitwa pia “malkia wa Andes,” unavutia watu hasa kwa sababu unachukua muda mrefu sana kukomaa na kuchanua. Mtaalamu mmoja wa mimea anayeheshimiwa alihesabu makovu kwenye majani ya mmea wa puya uliokuwa umenyauka na akakadiria kwamba ulikuwa umedumu kwa miaka 150. Wengine hudai kwamba mimea hiyo hudumu kwa miaka 70 tu. Wenyeji wa huku huamini kwamba mimea hiyo huchukua miaka 100 kuchanua. Inaripotiwa kwamba puya wa kwanza kupandwa ulichanua baada ya miaka 28 tu huko California, mnamo mwaka wa 1986. Hata watu waseme nini kuhusu mimea ile inayomea katika milima mirefu ya Andes, ukweli ni kwamba mimea hiyo huchukua muda mrefu sana kukomaa.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Mmea wa “Puya raimondii” huwezaje kumea katika kiasi kidogo cha udongo?

[Picha katika ukurasa wa 23]

Maua mengi sana ya mmea wa “Puya raimondii” huwavutia ndege wengi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mmea wa “Puya raimondii” uliokuwa karibu kuteketea kabisa