Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jangada—Mashua za Kipekee za Brazili

Jangada—Mashua za Kipekee za Brazili

Jangada—Mashua za Kipekee za Brazili

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

KWA karne nyingi, wavuvi wajasiri wanaoitwa jangadeiro wamesafiri kwenye pwani ya kaskazini-mashariki ya Brazili wakitumia mashua zao sahili za jangada zenye kupendeza. Acha nieleze mambo niliyojifunza kuhusu mashua hizo za kipekee.

Ukiona mashua hizo kwa mara ya kwanza, huenda ukafikiri ni vyombo vilivyotengenezwa haraka-haraka na watu waliovunjikiwa meli. Lakini usipumbazike. Mashua hizo zaweza kwenda kwa mwendo wa kilometa 12 kwa saa na hutumiwa katika mashindano ya mashua. Ingawa mashua hizo zina muundo sahili, zaweza kukaa baharini kwa siku kadhaa na zaweza kufika umbali wa kilometa 60 toka ufukoni, huku zikielea karibu na meli zinazovuka Bahari ya Atlantiki. *

Mashua ya jangada ilitumiwa kwa mara ya kwanza huko Brazili kama chombo cha wavuvi mwishoni mwa karne ya 17, wakati wakoloni Wareno walipoweka matanga ya pembe-tatu kwenye mashua ndogo za wenyeji. Yasemekana kuwa Wareno ndio waliotunga jina jangada, linalomaanisha “kuunganisha.” Kabla ya kufika Brazili, walikuwa wametembelea India, ambako walisikia neno hilo la Kitamil.

Tangu wakati huo, mashua hizo zimebadilika kwa kiasi fulani. Hapo awali, viunzi vya mashua hizo vilitengenezwa kwa vigogo vitano hadi vinane vya mbao nyepesi za balsa, kama vile piúva, navyo viliunganishwa kwa kamba pasipo kutumia bolti wala msumari. Siku hizi, viunzi vingi vya jangada hutengenezwa kwa mbao zinazotumiwa kutengeneza mashua nyingine, hivyo vinadumu kwa muda mrefu. Mashua za siku hizi pia zina sanduku la mbao la kuhifadhia samaki, lililotengenezwa kwa zinki na plastiki maalumu. Ukubwa wa mashua hizo ni uleule—zina urefu wa meta 5 hadi 8 na upana unaweza kufikia meta 1.8.

Katika miaka ya karibuni, kutokea kwa mashua za kisasa za uvuvi kumewalazimu jangadeiro wengi kutafuta kazi nyingine, kama vile kuwatembeza watalii kwa kutumia jangada. Bado kuna vijiji vichache vya kitamaduni vya wavuvi kwenye pwani ya kaskazini-mashariki mwa Brazili. Watu hao huishi maisha sahili. Katika vijiji vingi kama hivyo, wakati ambapo wanaume wako baharini, wanawake hushona mapambo ili kuongeza pato la familia.

Ninapanda jangada kwa mara ya kwanza kwenye kijiji cha wavuvi huko kwenye ufuko wa Mucuripe.

Ninakuwa Jangadeiro kwa Siku Moja

Ni saa 10:00 alfajiri, nami niko ufukoni. Najulishwa kwa watu wengine wanne ambao tutasafiri nao. Nahodha wetu anaitwa Assis. Baada ya kupandisha tanga, tunasukuma mashua hiyo toka mahala ilipoegeshwa kwenye mbao za mti fulani unaofanana na mtende na kuiingiza baharini. Punde baadaye, mashua hiyo yalowa maji na yaonekana itazama. Lakini kumbe nimepumbazika. Kwa kawaida, mashua za jangada haziwezi kuzama. Mabaharia hao waniambia kwamba nyakati nyingine mashua hizo hupinduka juu-chini na ni mabaharia wenye ujuzi walio waogeleaji stadi tu wanaoweza kuzipindua tena. Vyovyote iwavyo, mawimbi yanapiga-piga sitaha huku tunaposonga mbele baharini.

Nahodha wetu yuko nyuma, ambako anaongoza mashua kwa tanga na usukani. Mvuvi mwingine yuko mbele mashuani. Wale mabaharia wengine wawili, ambao wameshikilia milingoti imara, wanaegemea ili kusawazisha jangada. Kwa kuwa mimi ni mtazamaji tu, ninaamua kwamba ni heri nijishikilie kabisa kwenye milingoti hiyo. Kwa kawaida watu huwa wagonjwa wanaposafiri baharini kwa mara ya kwanza, lakini ninajaribu sana kuvumilia hali hiyo.

Tunawasili mahala tulipokuwa tukienda baada ya kusafiri kwa muda wa saa mbili hivi. Mabaharia wanaondoa tanga upesi na kutia nanga—jiwe lililowekwa ndani ya kiunzi cha mbao—kisha tunaanza kuvua samaki. Wavuvi hao hutumia kamba ya kuvua badala ya fito. Ndiyo sababu mikono yao ni migumu na imejaa makovu. Mbali na kuvua samaki, nyakati nyingine wao huvua kamba-miti wakitumia mtego unaoitwa manzuá, ambao umetengenezwa kwa mwanzi na kamba ya nailoni. Wavuvi wengine huvaa kofia za nyasi zenye ukingo mpana, na wengine huvaa kofia za kitambaa ili kujikinga na jua.

Maisha ya jangadeiro ni magumu kwani wao hufanya kazi katika jua kali, chumvi, na kutoa jasho sana. Idadi ya vijana wanaotaka kujifunza kazi hiyo inapungua. Kwa karne nyingi, akina baba wamekuwa wakiwakabidhi wana wao kazi hiyo.

Wakati wa alasiri, tunaanza safari ya kurudi huku tukisafiri karibu na jangada zingine. Mashua hizo zenye matanga meupe zinapasua mawimbi yenye nguvu huku zikisafiri kati ya bahari nyangavu ya kijani na anga la bluu. Hiyo ni mandhari yenye kupendeza sana ambayo imewavutia watu kutunga mashairi na nyimbo nyingi.

Tunapofika ufukoni, tunasukuma jangada hiyo kwenye gati lake juu ya mchanga. Ingawa kwa kawaida jangada huwa na uzito wa kilogramu 300, mashua hiyo yaonekana kuwa nzito sana kwa kuwa tumechoka. Wavuvi hao wanamuuzia mfanyabiashara samaki. Kisha mfanyabiashara huyo atawauzia watu samaki hao. Safari yetu ilikuwa fupi, na tulivua samaki wachache. Lakini jangada inaweza kubeba kilogramu 1,000 za samaki. Ninawashukuru mabaharia hao na ninarudi nyumbani. Ingawa nimechoka, nimeridhika. Nikiwa ninapumzika kitandani usiku, ninahisi ni kana kwamba ninapelekwa huku na huku katika jangada, mashua sahili na ya kipekee ya Brazili.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Mnamo mwaka 1941, wavuvi wanne walisafiri kilometa 3,000 kwa jangada kutoka kwenye jiji la Fortaleza hadi Rio de Janeiro. Kisa hicho kilielezwa katika filamu yenye kichwa It’s All True, iliyotayarishwa na Orson Welles.

[Picha katika ukurasa wa 25]

“Jangada” za kale zilizotengenezwa kwa vigogo, hazitumiwi sasa

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kwa kawaida “jangada” huwa na uzito wa kilogramu 300 hivi