Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Biashara Iliyoanza Kale

Biashara Iliyoanza Kale

Biashara Iliyoanza Kale

Karakana ya John ya useremala ilikuwa karakana iliyojengwa vyema na yenye vifaa vingi zaidi katika eneo lao. Aliionea fahari na shangwe. Lakini moto ulizuka usiku mmoja. Baada ya muda wa saa chache, karakana yake nzuri iliteketea kabisa.

HAPO awali, John alifikiria kukata bima ya moto kwa kutumia kiasi fulani cha fedha za ujenzi wa karakana yake. Hata hivyo, akasababu hivi: ‘Mimi ni mwangalifu sana. Na moto usipozuka kamwe, basi nitakuwa nimepoteza fedha kwa kukata bima.’ Lakini moto ulizuka. Endapo John angekuwa ameikatia bima karakana yake, yamkini angeweza kuijenga upya. Lakini hangeweza kuijenga bila bima.

Bima Ni Nini?

Si lazima bima iwe biashara ambayo mtu anatarajia kurudishiwa fedha zake. Wala si kamari. Mcheza-kamari hujasiria hatari, ilhali bima huandaa ulinzi dhidi ya hatari zilizopo. Bima ni njia ya kushiriki hatari na wengine.

Tangu nyakati za kale, jamii zimekuwa zikichanga baadhi ya rasilimali zake ili kuwasaidia watu wanaopata hasara. Miaka 3,500 hivi iliyopita, Musa aliagiza taifa la Israeli litoe fungu la mazao yake pindi kwa pindi kwa ajili ya “mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe.”—Kumbukumbu la Torati 14:28, 29.

Mwanzo wa Bima

Bima imekuwapo kwa maelfu ya miaka. Sheria za Hammurabi zilitaja bima fulani ya malipo, sheria hizo zilitia ndani sheria za Babiloni ambazo yadhaniwa zilitangulia Sheria ya Musa. Ili kugharimia safari zao za kibiashara nyakati za kale, wamiliki wa meli waliomba mikopo kutoka kwa wawekezaji. Iwapo meli ingezama, wamiliki hawakuwa na wajibu wa kulipa mikopo hiyo. Kwa kuwa meli nyingi zilirejea salama salimini, faida iliyolipwa na wamiliki wengi wa meli hizo ilitosha kuwapa faida wakopeshaji.

Mojawapo ya kampuni mashuhuri zaidi za bima ulimwenguni, Lloyd’s of London, iliibuka baadaye kutokana na shughuli hizohizo za baharini. Kufikia mwaka wa 1688, Edward Lloyd alikuwa akiendesha mkahawa ambamo wafanyabiashara wa London na wafanyakazi wa benki walikutana ili kufanya biashara za ziada. Humo wadhamini waliowapa mabaharia kandarasi za bima waliandika majina yao chini ya kiasi fulani hususa cha fidia ambacho walikuwa tayari kutoa baada ya kupokea malipo fulani ya bima. Hao watoaji-bima wakaanza kuitwa watoaji wa hati za bima (underwriters). Hatimaye, kampuni ya Lloyd’s ikawa shirika rasmi la bima mnamo mwaka wa 1769, na muda si muda ikasitawi na kuwa kampuni kubwa zaidi ya bima ya hatari za baharini.

Shughuli za Bima Leo

Watu wanapokata bima leo, wangali wanashiriki hatari yao na wengine. Makampuni ya kisasa ya bima huchunguza takwimu zinazoonyesha hasara zilizotokea awali—kwa mfano, hasara za mioto kuteketeza karakana—ili kujaribu kukisia hasara ambayo wateja wao watakabili wakati ujao. Kampuni ya bima hutumia fedha zinazolipwa na wateja wengi ili kulipa fidia kwa wateja wanaopata hasara.

Je, wahitaji bima? Ikiwa ndivyo, ni bima ipi inayofaa hali zako? Uwe na bima au la, ni tahadhari zipi zinazoweza kukusaidia kukabiliana kwa mafanikio na hatari maishani?

[Picha katika ukurasa wa 3]

Mojawapo ya kampuni mashuhuri zaidi za bima ulimwenguni ilianzia kwenye mkahawa

[Hisani]

Courtesy of Lloyd’s of London