Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Bohari la Mbegu

Gazeti la National Post la Kanada laripoti kwamba “wanasayansi wanatabiri kwamba asilimia 25 ya mimea yote duniani huenda ikatoweka katika miaka 50 ijayo.” Ili kulinda mimea iliyo katika hatari ya kutoweka, bustani ya Royal Botanical Gardens huko Kew, Uingereza imeanzisha Hifadhi ya Mbegu za Milenia (MSB). Gazeti hilo laeleza kwamba “mradi wa MSB ni kukusanya na kuhifadhi zaidi ya jamii 25,000 za mimea—zaidi ya asilimia 10 ya mimea yote inayoota mbegu.” Wasimamizi wa mradi huo wanatumaini kutumia mbegu hizo kupanda tena mimea katika maeneo yaliyofanywa ukiwa, kupunguza uwezekano wa kutokea kwa ukame, na kukuza mimea inayotumiwa katika dawa za kienyeji na zile za kawaida. Msimamizi wa mradi huo wa kuhifadhi mbegu, Roger Smith alisema hivi: “Mimea inayotangulia kutoweka ni ile iliyo muhimu zaidi kwa wanadamu na wanyama.”

Mshtuko wa Moyo Usio na Maumivu

Watu wengi wanatambua dalili ya kawaida ya mshtuko wa moyo—kubanwa kifuani. Hata hivyo, ni watu wachache sana wanaofahamu kwamba “thuluthi ya wagonjwa wote hawahisi maumivu yoyote kifuani wanapopatwa na mshtuko wa moyo,” laripoti gazeti la Time. Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika jarida la The Journal of the American Medical Association, jambo hilo laonyesha ni kwa nini “watu wanaopatwa na mshtuko wa moyo bila kuhisi maumivu kifuani kwa kawaida huahirisha kwenda hospitalini—kwa wastani wa saa mbili.” Hata hivyo, ni hatari kusita kupata matibabu ambayo huenda yakaokoa uhai. Utazamie dalili zipi? “Huenda dalili nyingine kuu itakuwa kukosa pumzi,” lasema gazeti la Time. Dalili nyinginezo zatia ndani kichefuchefu, kutokwa na jasho jingi, na “‘kiungulia’ chochote chenye kuongezeka unapotembea au kufanya kazi ngumu,” yasema makala hiyo.

Vidole vya Miguu Vyenye Kunata

Mjusi wanaweza kutimua mbio kwa urahisi kwenye dari yenye kuteleza kama kioo. Ni nini huwawezesha kufanya hivyo? Wanasayansi ambao wamekuwa wakitafuta jibu la swali hilo kwa miongo mingi, sasa wanafikiri wamepata jawabu. Kundi moja la wanasayansi na wahandisi limegundua kwamba “kani yenye uwezo wa ajabu wa kunata hutokea manyoya madogo sana yaitwayo setae yaliyo kwenye miguu ya mjusi yagusapo sehemu fulani,” laripoti gazeti la Science News. “Kila setae huwa na manyoya mengine madogo zaidi yanayoitwa spatulae. Mjusi anapokanyaga sehemu fulani, takriban spatulae bilioni moja hivi zilizo kwenye wayo wake husongamana sana hivi kwamba kani baina ya molekuli . . . huenda ikatokea.” Wachunguzi pia wameona kwamba mjusi anapokanyaga sehemu kwa vidole vyake, “hufinya setae kwenye eneo hilo kisha kuzitandaza.” Jambo hilo huongeza “uweza wa kunata wa kila setae mara 10 zaidi ya ingalivyokuwa iwapo angalifinya tu bila kutandaza,” lasema gazeti hilo.

Uamuzi Wakasirisha Kanisa Othodoksi la Ugiriki

Ripoti moja kutoka kituo cha Newsroom.org. yasema kwamba kuondolewa kwa jina la dini ya raia Wagiriki katika “vitambulisho vya kitaifa kumelikasirisha sana Kanisa Othodoksi la Ugiriki.” Uamuzi huo ulitolewa kufuatia ripoti moja ya 1998 ya Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu la Helsinki “iliyodai kwamba Ugiriki huonea dini nyingine zisizo za Othodoksi na kwamba dai la kisheria la kuonyesha dini ya mtu kwenye kitambulisho chake cha kitaifa huongoza kwenye ubaguzi wakati wa kuajiriwa kazi na anavyotendewa na polisi.” Serikali ya Ugiriki inasema kwamba badiliko hilo “litafanya vitambulisho hivyo vipatane na viwango vya Muungano wa Ulaya na pia sheria ya nchi hiyo ya mwaka wa 1997 ya kulinda siri,” yasema makala hiyo. Hata hivyo, kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Ugiriki amewataja watu wanaotaka jina la dini liondolewe kwenye vitambulisho kuwa wanaongozwa na “kani za uovu.”

China Yapambana na Dhoruba za Vumbi

Katika miaka ya hivi karibuni, dhoruba za vumbi kutoka Mongolia ya Kati zimesambaa eneo lote la kaskazini mwa China na kuharibu mimea na mifugo ya thamani ya mamilioni ya dola, laripoti gazeti la China Today. Mwaka wa 2000, baadhi ya dhoruba hizo zilisambaa hadi mji mkuu, Beijing. Katika mwaka wa 1998, dhoruba ya vumbi iliharibu zaidi ya ekari 82,000 za nafaka na kuua mifugo 110,000. Utumizi mbaya wa ardhi na mwanadamu ulitajwa kuwa kisababishi kikuu cha hali hiyo. Maeneo makubwa yamefyekwa na kuachwa ukiwa. Kwa kielelezo, katika mwaka wa 1984, watu katika Jimbo Linalojitawala la Ningsia Hui, lililo kaskazini mwa China, walianza kufukua mizizi ya urukususu ili kuitumia kama dawa ya kienyeji ya Kichina. “Katika muda usiozidi miaka 10, nyika ya [ekari 1,500,000] iliharibiwa na mashamba ya [ekari 32,940] yaligeuka kuwa jangwa” lasema gazeti la China Today. Maeneo mengine yamegeuka kuwa jangwa kutokana na kulishwa wanyama kupita kiasi na matumizi mabaya ya maji yaliyomo. Ili kupambana na tatizo hilo na kuzuia kuenea kwa jangwa, jitihada kubwa inafanywa ya kupanda miti na nyasi.

Wizi wa Vitambulisho

Ripoti moja katika gazeti la Mexico City, El Economista yaonya juu ya walaghai wanaoiba kitambulisho chako na kukitumia kuibia wakopeshaji. Baada ya kupata habari ya kibinafsi kwa kuiba barua au kibeti chako, walaghai hao huagiza kadi mpya ya mkopo kwa jina lako na kuomba itumwe kwa anwani zao. Halafu wanatumia vitambulisho vyako kununua vitu au kukodi nyumba kupitia simu au Internet. Wanaoibiwa vitambulisho vyao waweza kuchukua miaka, na labda miongo ili kurekebisha hasara iliyosababishwa, lasema gazeti hilo. Waweza kujikingaje na wizi wa vitambulisho? Gazeti la El Economista lashauri hivi: Usibebe hati muhimu isipokuwa tu uwe unanuia kuzitumia, weka rekodi ya matumizi yote ya kadi zako za mkopo na utumie rekodi hiyo kuchunguza taarifa za malipo, rarua risiti zote kabla ya kuzitupa, usitume habari ya kibinafsi kupitia kwa kompyuta, andika orodha ya namba za kadi zote za mkopo ulizo nazo, tarehe ya mwisho, na namba ya simu ya wenye kutoa kadi ili uweze kuripoti kadi ipoteapo au ikiibiwa.

Pambano Dhidi ya Bakteria Halina Msingi

“Wanunuzi Waamerika wanapambana isivyofaa na bakteria nyumbani,” laripoti gazeti la USA Today. Kwa mujibu wa gazeti hilo, daktari na mtaalamu wa mikrobiolojia Stuart Levy katika Chuo Kikuu cha Tufts, asema kwamba “kuenea kwa bidhaa za kuua bakteria . . . kunatisha kutokeza bakteria sugu ambao hawawezi kuuawa na sabuni au viua vijasumu.” Kutumia bidhaa za kufisha bakteria ili kuua viini kwenye mazingira ya nyumbani ni “sawa na kutumia rungu kuua nzi,” asema Levy. Kwa upande mwingine, bidhaa za usafi wa nyumbani kama vile dawa ya klorini, hidrojeni peroksaidi, maji moto na sabuni huondoa uchafu bila kufanya bakteria kuwa sugu dhidi ya bidhaa hizo. “Bakteria ni rafiki zetu,” asema Levy. “Tuwe na amani nao.”

Waingereza Ni Watazamaji Bingwa wa Televisheni

“Takriban robo ya Waingereza hutazama televisheni kwa muda unaolingana na ule wanaotumia kazini kila juma,” laripoti gazeti la huko London, The Independent. Watafiti wanasema kwamba Mwingereza wa kawaida hutumia saa 25 kila juma kutazama televisheni, huku asilimia 21 ikitazama televisheni kwa zaidi ya saa 36. “Uchunguzi huo uligundua kwamba sio vijana pekee wanaotazama televisheni kupita kiasi, bali wanaume na wanawake na watu wazee pia hufanya vilevile,” lasema gazeti hilo. Familia moja ambayo hutazama televisheni kwa saa 30 kila juma, ilisema kwamba televisheni ni njia “inayohitajiwa ya kukwepa matatizo.” Hata hivyo, utazamaji huo wenye kupita kiasi umekuwa na athari. Katika uchunguzi wenye kuhusisha nchi 20, Uingereza “iliibuka bingwa wa kutazama televisheni,” laripoti gazeti la London, The Guardian Weekly. Ilhali “Uingereza inakaribia kuwa ya kwanza kwa kuwa na watu wengi zaidi wasiojua kusoma na kuandika.”

Masomo ya Ngono Mapema

Gazeti la Bangkok Post laripoti kwamba watoto walio katika shule ya watoto wadogo huko Bangkok, Thailand wataanza kupokea masomo ya ngono. Kulingana na Dakt. Suwanna Vorakamin wa Idara ya Mpango wa Uzazi na ya Kudhibiti Ongezeko la Watu, “walimu na wanatiba wataelimishwa kipekee jinsi ya kufundisha kisayansi masomo ya ngono,” yasema ripoti hiyo. Yeye aongeza kusema hivi: “Kuanzishwa kwa masomo ya ngono katika shule za watoto wadogo hakukusudiwi kuwachochea wajihusishe katika ngono. . . . Ujuzi watakaopokea utawasaidia kukinza tabia isiyofaa na kuepuka kupata mimba haramu watakapofikia umri wa ujana,” gazeti hilo laripoti.