Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kumlea Mtoto Porini

Kumlea Mtoto Porini

Kumlea Mtoto Porini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

KATIKA nyanda pana mno zenye mbuga za Afrika, ndama azaliwa. Adondoka kwa kishindo ardhini katika jua la mapambazuko. Kwa uanana, mama ainama chini na kumnyanyua ndama wake mwenye ngozi inayong’aa na yenye unyevunyevu aliyezaliwa karibuni, naye asimama kwa miguu yake legelege. Akina mama na dada zake wengine wakimbia karibu ili kumtazama kwa ukaribu na kumgusa na kumnusa ndama huyo mchanga sana. Ndama wa tembo mwenye uzito wa kilogramu 120 tu na mwenye kimo kinachopungua sentimeta 90, husisimua sana washiriki wengine kundini.

Katika eneo lililo maelfu ya kilometa mbali, huko Amerika, kiota kidogo sana kama kastabini, chaning’inia kwenye tawi la mti. Humo ndege wawili wavumaji aina ya bee, ambao wanalingana na wadudu warukao, hutunza makinda wawili wadogo. Huku wakiruka kwa kasi ajabu, ndege hao maridadi sana ni wazazi jasiri ambao hujaribu kuwafukuza wanyama wakubwa na hata wanadamu ambao wanakaribia sana makinda wao.

Vitoto vya wanyama hutuvutia sote. Watoto huvutiwa sana na vitoto vya mbwa. Ni nani asiyefurahia mchezo wenye kuchekesha wa mtoto wa paka, umbo lenye kuvutia la tumbili mchanga anayejishikilia kwenye manyoya ya mamaye, au kinda la bundi linalokodoa macho kutoka kwenye kiota chake kilicho salama?

Vitoto vya wanyama si hoi daima kama mtoto wa mwanadamu. Wengine wao huzaliwa wakiwa na uwezo wa kukimbia mara tu baada ya miguu yao midogo kukanyaga chini. Wengine huachwa peke yao kabisa ili kujilinda na kujitafutia mlo. Hata hivyo, ili wanyama na wadudu wengi wachanga waendelee kuishi wao hutegemea malezi, ulinzi, ulishaji, mazoezi, na utunzaji wa wazazi ambao hutokana na uhusiano wa karibu baina ya wazazi na watoto wao wachanga.

Wanyama Wasiotarajiwa Kuwa Watunzaji

Wadudu, samaki, amfibia, na wanyama-watambazi wengi hawajali masilahi ya watoto wao. Hata hivyo, kuna wanyama wengine ambao ni tofauti. Mnyama mmoja ambaye hatarajiwi kuwa mtunzaji ni mamba wa Nile mwenye kutisha. Mnyama huyo mtambazi mwenye damu baridi huandaa utunzaji wa pekee sana akiwa mzazi. Baada ya kutaga mayai katika mchanga wenye joto, wazazi hukaa karibu ili kuwalinda watoto wao. Mamba wachanga wanapokaribia kuanguliwa, wanaanza kuguna, na hivyo mama hujua ni wakati wa kuyafukua mayai. Baadaye, kwa kutumia mataya yake yenye nguvu, yeye hukusanya kwa uanana watoto wake walioanguliwa na kuwapeleka karibu na maji ili kuwasafisha na kuondoa mchanga walio nao. Mamba wa kiume pia wameonekana wakipeleka mamba wachanga majini ili kuwasafisha. Kwa siku kadhaa, watoto hao hukaa karibu na mama yao majini, huku wakimfuata kama vifaranga wa bata wanavyomfuata mama yao. Na hivyo wananufaishwa na uwezo wake mkubwa wa kuwalinda.

Jambo la kushangaza ni kwamba, samaki wengine pia wanaweza kuitwa wazazi wazuri. Samaki wengi aina ya tilapia, ambao ni samaki wa maji baridi, hutaga mayai kisha huyahifadhi salama midomoni mwao. Baada ya kuanguliwa, samaki wachanga huogelea kwa uhuru, huku wakiwa karibu na wazazi wao. Hatari inapozuka, samaki mzazi hufunua kabisa kinywa chake, na kuwaruhusu samaki wachanga kukimbia ndani na kujificha. Hatari inapotokomea, hao samaki wachanga huibuka tena na kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Chungu, nyuki, na mchwa pia huwa na mwelekeo wa pekee wa kutunza na kulinda watoto wao. Wadudu hao wanaoitwa wadudu wa kijamii, huishi kwa makundi, hujenga viota vya mayai yao, na huandalia watoto wao chakula. Nyuki wa asali ni mfano ujulikanao sana wa wadudu hao. Maelfu ya nyuki wenye shughuli nyingi hushirikiana kutunza nyuki wachanga mzingani. Hekima ya silika huwawezesha kujenga, kurekebisha, na kusafisha kiota, hata kudhibiti halijoto na unyevunyevu uliomo.

Ndege Wazazi

Ndege wengi huwa wazazi wazuri sana, wao hutumia wakati mwingi na nishati katika kuteua mahali pa kujenga kiota, hukijenga kiota, na kulea familia yao. Hondohondo mmoja wa kiume wa Afrika mwenye bidii alionekana akizuru kiota chake zaidi ya mara 1,600, na kumletea mwenzi wake vipande 24,000 vya matunda katika kipindi chote cha siku 120 cha kuatamia!

Albatrosi mwenye kuhamahama pia ni mtunzaji mwenye kutegemeka. Ndege mzazi huruka maelfu ya kilometa akitafuta chakula huku mwenziwe mwaminifu akimsubiri kiotani.

Katika majangwa ndege fulani hutumia mbinu bora ya kukata kiu cha makinda wao. Wao huruka penye kidimbwi cha maji, na kulowesha manyoya yao ya kidari na kurejea kiotani, ambamo makinda hunywa maji yaliyo kwenye manyoya yake yaliyolowa.

Kazi ya kulisha makinda wengi inapokuwa ngumu sana, jamii fulani za ndege huomba msaada wa ndege wengine ili wawe “walezi wa muda” wa makinda wao. Wasaidizi hao kwa kawaida huwa makinda waliokomaa wa ndege hao nao huwa tayari kusaidia kulisha na kulinda makinda wadogo.

Ulinzi wa Wazazi

Kuwalinda makinda pia ni kazi ya wakati wote. Mara nyingi ndege wazazi hufunika kiota chao kwa mabawa yaliyo wazi kunaponyesha, na hivyo makinda wao hupata joto na hawalowi. Kwezi ni watunza-nyumba hodari. Ili kulinda kiota chao kutokana na chawa na viroboto, ndege hao werevu hukusanya visehemu vya mimea fulani yenye sumu na kuviweka ndani na nje ya kiota. Visehemu hivyo huwa kama dawa zinazoua au zinazofukuza wadudu hatari.

Ndege mama aina ya woodcock hutumia mbinu za hali ya juu sana anapolinda kinda lake. Kunapokuwa na hatari, yeye hubeba kinda lake kwa nguvu kati ya miguu yake na mwili, hufunua mabawa yake, na kuruka mbali akiwa amebeba kinda analolipenda sana hadi mahali salama. Wazazi fulani jasiri hujisingizia wamejeruhiwa ili kukengeusha wanyama-wawindaji wasikaribie makinda wao. Kwa kupigapiga mabawa ardhini kana kwamba amejeruhiwa, mama huyo humvutia mnyama-mwindaji ili kumzuia asikaribie kiota, kisha huacha kujisingizia na kuruka mbali kwa usalama hatari inapotoweka. Ndege wenye viota ardhini waweza kutumia sauti zao kwa hila ili kufukuza wawindaji. Bundi wa Amerika Kaskazini anayeishi mashimoni hutoa mlio kama wa nyoka shimo lake linapoingiliwa. Walowezi wa mapema walikuwa na uhakika kwamba bundi hao wadogo waliishi pamoja na nyoka wanaotoa mlio wa kutatarika kwa mkia, nao waliepuka mashimo hayo!

Mamalia Walio Mama

Katika jamii ya wanyama, mamalia ndio wenye ujuzi zaidi wa kutunza watoto. Tembo mama hujitoa mhanga kutunza ndama wao, nao husitawisha uhusiano wa karibu unaoweza kudumu kwa miaka 50. Ndama humtegemea sana mama yake. Mama humkinga kutokana na jua kali kwa mwili wake mkubwa, humnyonyesha kwa uanana, na kumruhusu anyooshe mkonga wake mdogo na kula majani kutoka kwa kinywa chake. Yeye humwosha ndama wake kwa kawaida kwa kumnyunyizia maji mgongoni na kumsugua kwa mkonga wake. Familia nzima hushirikiana kumlea ndama, kwani tembo wengine wa kike kundini hutimiza fungu muhimu katika kulisha, kuzoeza, na kuwalinda ndama walio kundini.

Mamalia mwingine mkubwa, kiboko, aweza kuzaa ndama akiwa majini. Ndama hao wanaweza kunyonya vyema wakiwa ndani ya maji, kuibuka ili kupata hewa, kisha kurejea majini na kuendelea kunyonya. Kiboko mama huwa mkali sana anapolinda ndama wake aliyezaliwa karibuni.

Ngedere huwa mama wazuri pia. Baada ya kuzaa, mama humshika mtoto wake saa za kwanzakwanza huku akiwa amemkumbatia mabegani au shingoni na angalau mkono mmoja. Kwa juma la kwanza, mtoto huyo aweza kushikilia manyoya ya mama yake kisilika kwa muda mwingi. Mama aweza kuwaruhusu ngedere wengine wa kike wamshike mtoto wake, nao waweza kumtomasa, kumsafisha na kuchanua manyoya yake, kumkumbatia, na kucheza na mtoto huyo mrembo aliyezaliwa karibuni.

Kwa kweli, viumbe wengi wana “akili nyingi sana” nao hudhihirisha uwezo wa asili wa hali ya juu sana wanapowatunza watoto wao. (Mithali 30:24-28) Uwezo wao wa kutambua uhitaji au kuchanganua hali na kuimudu kwa njia ya akili hakungeweza kamwe kutokea kwa nasibu tu bila mwelekezo. Ni tokeo la ubuni wa kiakili wa mtu mwenye akili—Muumba wa vitu vyote, Yehova Mungu.—Zaburi 104:24.

[Picha katika ukurasa 15]

Makinda ya bundi

[Picha katika ukurasa 16]

“Tilapia” huhifadhi mayai yao mdomoni

[Hisani]

Courtesy LSU Agricultural Center

[Picha katika ukurasa 16]

Mamba hubeba watoto wao

[Hisani]

© Adam Britton, http://crocodilian.com

[Picha katika ukurasa 17]

Albatrosi na kinda lake

[Picha katika ukurasa 17]

Hondohondo

[Picha katika ukurasa 17]

Kwezi

[Picha katika ukurasa 17]

“Woodcock”

[Picha katika ukurasa 18]

Viboko mama huwa wakali sana wanapolinda ndama wao

[Hisani]

© Joe McDonald

[Picha katika ukurasa 18]

Nyani akina mama husafisha manyoya ya watoto wao

[Picha katika ukurasa 18]

Ngedere

[Hisani]

© Joe McDonald