Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Mtume Paulo alitumia barabara gani katika safari yake ya kwanza kwenda Roma?

Andiko la Matendo 28:13-16 linasema kwamba Paulo alisafiri kwa meli mpaka Italia. Meli hiyo ilitia nanga Puteoli (Pozzuoli la siku hizi), kwenye Ghuba ya Naples. Kisha akatumia barabara inayoitwa Via Appia kwenda Roma. Hiyo ilikuwa barabara kuu ya jiji hilo.

Barabara ya Via Appia iliitwa kwa jina la ofisa fulani Mroma (Appius Claudius Caecus), aliyeanza kuijenga mwaka wa 312 K.W.K. Barabara hiyo yenye upana wa mita 5 hadi 6, imefunikwa kwa mawe makubwa ya volkano. Barabara ya Via Appia, yenye urefu wa kilomita 583, iliunganisha Roma na bandari ya Brundisium (Brindisi ya siku hizi), upande wa kusini-mashariki. Hapo ndipo safari za kwenda Mashariki zilianzia siku za kale. Wasafiri walikatiza safari zao kwenye vituo mbalimbali vya kupumzikia vilivyopatikana baada ya kila kilomita 24 hivi. Katika vituo hivyo waliweza kununua bidhaa, kulala, au kubadilisha farasi au magari yaliyokokotwa na farasi.

Yaelekea Paulo, alipokuwa njiani kwenda Roma, alitembea kwa miguu kwa umbali wa kilomita 212 hivi kwenye barabara ya Via Appia. Alivuka eneo lenye majimaji la Pontine katika safari hiyo. Mwandikaji mmoja Mroma alilalamika kuhusu mbu wengi na harufu mbaya sana ya eneo hilo. Soko la Apio lilikuwa kaskazini ya eneo hilo, umbali wa kilomita 70 hivi kutoka Roma. Kituo cha kupumzikia cha Mikahawa Mitatu kilikuwa umbali wa kilomita 50 hivi kutoka jiji hilo. Wakristo kutoka Roma walimngojea Paulo kwenye vituo hivyo viwili. Alipowaona, ‘Paulo alimshukuru Mungu na kujipa moyo.’—Matendo 28:15.

Ni bamba la aina gani la kuandikia linalotajwa katika Luka 1:63?

Injili ya Luka inataja kwamba marafiki wa Zekaria walimuuliza kuhusu jina la mwana wake aliyekuwa amezaliwa majuzi. Zekaria “akaomba bamba na kuandika: ‘Yohana ndilo jina lake.’” (Luka 1:63) Kulingana na kitabu kimoja cha wataalamu, neno la Kigiriki linalotafsiriwa “bamba” katika andiko hilo linamaanisha “bamba dogo la mbao la kuandikia, lililopakwa nta kwenye sehemu ya juu.” Mabamba ya mbao yaliyokuwa yameunganishwa pamoja, yalipakwa nta laini ya nyuki. Mwandikaji aliandika kwenye mabamba hayo kwa kutumia kifaa fulani kilichochongoka. Baadaye maandishi yalifutwa na yale mabamba yaliweza kutumiwa tena.

Kitabu kimoja kuhusu kusoma na kuandika wakati wa Yesu (Reading and Writing in the Time of Jesus) kinasema hivi: “Michoro ambayo imepatikana Pompeii, na sanamu kutoka sehemu mbalimbali za Milki ya Roma, zinaonyesha kwamba mabamba kama hayo yalitumiwa kwa ukawaida. Yamechimbuliwa pia katika sehemu nyingi, kuanzia Misri hadi Ukuta wa Hadriani [Uingereza Kaskazini].” Yaelekea, watu kama vile wanabiashara, maofisa wa serikali, na labda hata baadhi ya Wakristo wa karne ya kwanza, walitumia mabamba kama hayo.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Via Appia

[Picha katika ukurasa wa 11]

Bamba la nta la mtoto wa shule, miaka ya 100 W.K.

[Hisani]

By permission of the British Library