Mtu Anapotaka Kuendelea Kunywa
Mtu Anapotaka Kuendelea Kunywa
ALLEN alianza kunywa pombe kupita kiasi alipokuwa na miaka 11. * Yeye na marafiki wake walicheza msituni wakiigiza watu mashuhuri waliokuwa wamewaona katika sinema. Watu waliowaigiza hawakuwa watu halisi, lakini bila shaka pombe ambayo Allen na marafiki wake walikunywa ilikuwa halisi.
Tony alikuwa na miaka 40 alipoanza hatua kwa hatua kuongeza kiasi cha pombe alichokuwa akinywa kila jioni. Hatimaye, hakujua kiasi cha pombe alichokuwa akinywa kila siku.
Allen aliomba msaada wa kuacha kunywa pombe kupita kiasi. Tony naye alikataa msaada wa watu wa familia yake na marafiki wake. Allen angali yuko hai leo; Tony alikufa miaka kadhaa iliyopita katika msiba wa barabarani uliotokea kwa sababu alikuwa amelewa.
Hata mtu anapokunywa kupita kiasi akiwa peke yake, haikosi watu wengine wataathiriwa, na mara nyingi matokeo yanakuwa yenye kuhuzunisha. * Ulevi unahusika mara nyingi mtu anapotukanwa au kupigwa, mtu anaposhambuliwa au kuuawa, na vilevile misiba inapotokea barabarani au kazini. Ulevi pia unasababisha matatizo mengi ya afya na hasara kubwa ya pesa kwa jamii kila mwaka. Isitoshe, mtu mmoja-mmoja, familia, na watoto wanaathiriwa sana kihisia.
Hata hivyo, ripoti ya Taasisi za Afya za Marekani inasema kwamba “si wote wanaokunywa pombe kwa ukawaida ambao ni walevi, wala si wote ambao wana tatizo la kunywa pombe kupita kiasi, wanaokunywa kila siku.” Wengi ambao si walevi sugu wamezoea kunywa kupita kiasi bila kutambua tatizo lao. Wengine hawanywi kwa ukawaida lakini wanakunywa pombe nyingi kupita kiasi, kila wanapokunywa.
Ukiamua kunywa pombe, ni kiasi gani kinachofaa? Unaweza kujua jinsi gani kwamba hupaswi kuendelea kunywa? Makala zinazofuata zinazungumzia habari muhimu kuhusu unywaji wa pombe.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Baadhi ya majina yamebadilishwa.
^ fu. 5 Uwezekano wa mwanamume kuwa mlevi sugu ni mara nne kuliko wa mwanamke, hata hivyo, habari hizi zinafaa wanaume kwa wanawake.