Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Marekani

Katika kipindi cha juma la Oktoba 29, 2012, visa vya uuaji, jinai, na unyang’anyi vilipungua sana katika jiji la New York City ikilinganishwa na kipindi hicho hicho cha siku tano mwaka wa 2011. Sababu ilikuwa nini? Dhoruba kali inayoitwa Kimbunga Sandy, ilikumba Pwani ya Mashariki ya Marekani na kusababisha ukosefu mkubwa wa umeme. Msemaji wa Idara ya Polisi ya New York, Paul Browne, alisema, “Baada ya msiba wa asili au msiba mkubwa kama vile [lile shambulizi la kigaidi lililotokea Septemba 11, 2001], kunakuwa na upungufu wa visa vya uhalifu wa kawaida.” Hata hivyo, kulikuwa na ongezeko la visa vya uvunjaji wa nyumba kwa sababu ya uporaji, jambo ambalo halikumshangaza Browne. Alisema, “Kulikuwa na maeneo mengi ambayo hayakuwa na umeme.”

Antaktika

Wanasayansi wana wasiwasi kwamba mazingira ya asili ya Antaktika yanahatarishwa na kuwepo kwa spishi nyingi za kigeni. Inakadiriwa kwamba kila mmoja kati ya makumi ya maelfu ya wageni wanaotembelea bara hilo kila mwaka huleta bila kukusudia wastani wa mbegu 9.5, na mara nyingi mbegu hizo huwa kwenye viatu au mikoba yao. Spishi nyingi za mimea ya kigeni tayari zimegunduliwa katika Rasi ya Antaktika Magharibi.

Uholanzi

Mwanamke mwenye umri wa miaka 83 amekuwa mtu wa kwanza kupandikizwa taya bandia ya titani iliyotengenezwa na mashine ya leza yenye uwezo wa kutokeza maumbo. Mgonjwa huyo ambaye taya yake iliharibiwa na ugonjwa unaoshambulia mifupa, sasa anaweza kula, kupumua, na kuongea kama kawaida. Mashine hiyo iliunganisha chembe za titani, tabaka kwa tabaka, ili kufanyiza taya hiyo bandia, kisha akafanyiwa upasuaji na kupandikizwa.

Ujerumani

Katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya uvutaji sigara kupigwa marufuku katika mahali pa kazi nchini Ujerumani, idadi ya watu wanaolazwa hospitalini kwa sababu ya ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu makali ya kifua ilipungua kwa asilimia 13.3 kati ya kikundi kimoja kilichofanyiwa uchunguzi; idadi ya waliopatwa na mshtuko wa moyo ilipungua kwa asilimia 8.6.