Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Televisheni

Televisheni

 Televisheni

MUDA fulani baada ya wanadamu kujifunza kupeperusha sauti kwa kutumia redio, wavumbuzi walijiuliza ikiwa pia wangeweza kupeperusha picha za moja kwa moja. Ili uelewe kwa nini jambo hilo ni gumu, fikiria jinsi televisheni inavyofanya kazi leo.

Kwanza, kamera ya video hupiga picha na kuituma kwenye kifaa fulani kilicho na uwezo wa “kusoma” picha hiyo, kama tu unavyofanya unaposoma kitu kilichochapishwa. Hata hivyo, badala ya kusoma herufi, inasoma madoa (au pikseli) katika picha. Kisha inabadili chochote inachoona kuwa mawimbi ya video yanayoweza kutumwa mahali pengine. Mawimbi hayo yanapopokewa kwenye kipokezi, yanabadilishwa kuwa picha.

Inasemekana kwamba John Logie Baird kutoka Scotland, ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuonyesha jinsi televisheni inavyofanya kazi. Baird ambaye alikuwa injinia wa vifaa vya umeme aliacha kazi yake kwa sababu ya ugonjwa na kuanza kufuatilia jambo lililokuwa limempendeza tangu alipokuwa kijana, yaani, kubuni mashini ambayo ingeweza kuonyesha picha moja kwa moja.

Kamera ya televisheni ya Baird ilitumia diski iliyokuwa na matundu 30 yaliyopangwa kwa mzunguko. Diski hiyo ilipozunguka, matundu hayo yalipita yakichunguza kila sehemu ya picha na kuruhusu mwangaza upite juu ya betri inayopata umeme kutokana na mwanga. Betri hiyo ilitoa mawimbi ya video yaliyotumwa kwenye kipokezi. Kwenye kipokezi hicho, mawimbi hayo yaliongezwa ukubwa na kutokeza mwangaza nyuma ya diski nyingine inayozunguka kutokeza picha hiyo. Changamoto kubwa ilikuwa kufanya diski hizo zizunguke kwa upatano. Baird alipokuwa akishughulikia mradi huo, alijiruzuku kwa kupiga viatu rangi.

Oktoba 2, 1925 (2/10/1925) Baird alipeperusha picha za kwanza za televisheni kutoka mwisho mmoja wa dari lake hadi ule mwingine. Mtu wa kwanza kuonekana katika televisheni alikuwa kijana aliyekuwa na wasiwasi mwingi sana ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye ofisi iliyokuwa kwenye orofa ya chini ya nyumba ya Baird. Alishurutishwa kufanya hivyo baada ya kuahidiwa kuwa angelipwa shilingi mbili na senti sita za Scotland. Mnamo 1928, Baird alipeperusha picha za kwanza za televisheni hadi ng’ambo ile nyingine ya Bahari ya Atlantiki. John Baird alipowasili huko New York, alishangaa sana alipokaribishwa kwa mbwembwe za bendi ya wapiga zumari. Sasa alikuwa mtu maarufu. Lakini je, yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kupeperusha picha moja kwa moja?