Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vijia vya Chini ya Ardhi vya Odessa

Vijia vya Chini ya Ardhi vya Odessa

 Vijia vya Chini ya Ardhi vya Odessa

UFA ulitokea kwenye ukuta uliotoka tu kupigwa plasta wa nyumba iliyokuwa ikikarabatiwa. Mwenye nyumba akalalamika akisema, “Sasa ona vijia hivyo vya chini ardhi vinafanya jengo letu liiname.”

Tatizo lolote linapotokea kwenye jiji maridadi la Odessa lililo kwenye fuo ya Bahari Nyeusi huko Ukrainia, iwe ni bomba la maji limepasuka au vijia imebonyea, itasemekana kuwa tatizo hilo limesababishwa na vijia vilivyo chini ya ardhi. Vijia hivyo vilivyo kama utando wa buibui ambavyo vinadhaniwa kuwa na urefu wa kilomita 2,500, ndivyo vijia virefu zaidi ulimwenguni vilivyo chini ya ardhi.

Tulijiuliza, ‘Vijia hivyo vilitokea jinsi gani? Vinaathiri jinsi gani maisha ya watu wanaoishi juu yake?’ Tulipata majibu tulipotembelea vijia hivyo.

Kutembelea Vijia vya Chini ya Ardhi

Safari yetu ilianzia kwenye kituo cha treni cha Odessa tukiwa pamoja na kikundi cha watalii na wanafunzi waliosisimuka. Tulipokuwa safarini, yule aliyetutembeza alitueleza kuhusu historia ya vijia hivyo.

Inaonekana kuwa vijia hivyo vilianza kuchimbwa katika miaka ya 1830, wakati ambapo jiji hilo lilihitaji vifaa vya ujenzi visivyogharimu sana na vinavyopatikana kwa urahisi. Iligunduliwa kwamba chini ya jiji hilo kulikuwa na matabaka ya mawe ya chokaa ya manjano yanayodumu ambayo si mazito. Kwa hiyo, uchimbaji wa mawe ukawa biashara kubwa katika jiji hilo lililokuwa likisitawi. Polepole walipoendelea kuchimbua mawe, vijia hivyo vya chini ya ardhi vikaanza kutokea.

Punde si punde, uchimbaji huo ulitokeza vijia vidogo chini ya ardhi ambavyo vilipitana-pitana kama utando wa buibui. Vijia hivyo vilichimbwa zaidi ya mita 35 chini ya ardhi. Nyakati nyingine vilipita-pitana moja juu ya nyingine. Walipomaliza kuchimba mawe ya chokaa katika kijia kimoja walianza kuchimba kingine. Muda si muda, utando huo wa vijia ulienea hadi sehemu nyingine za nchi.

Tulifika kwenye kijiji kidogo cha Nerubaiske kilicho kaskazini ya Odessa. Tulisimama kando ya ukuta wa mawe ya chokaa ulikuwa na lango zito la chuma lililoziba mwingilio wa mojawapo ya vijia hivyo. Yule aliyekuwa akitutembeza alituambia: “Sasa tutaingia kwenye eneo ambalo lilimilikiwa na Wasovieti wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Mtajionea jinsi maisha yalivyokuwa wakati huo.” Andriy Krasnozhon, mtaalamu wa vijia hivyo, anasema kuwa kikundi kimoja kiliishi chini ya ardhi kwa miezi 13.

 Aliyekuwa akitutembeza alisema, “Kumbuka kwamba wakati mmoja au mwingine, watu wengi zaidi walitumia sehemu mbalimbali za vijia hivi. Walitia ndani waporaji, maharamia, na wakimbizi wa kisiasa. Wote walipatwa na hali zilezile.”

Tuliingia kupitia kijia ambacho hakikuwa na nuru. “Vijia hivi havikuwa tu mahali pa kujificha bali vilikuwa pia mahali ambapo watu wangestarehe,” akaeleza. “Ndani ya chumba cha kustarehe wanaume walicheza draughts, chesi, au domino wakitumia mwangaza wa mshumaa. Vyumba ambavyo wanaume na wanawake waliishi vilichongwa kwenye mwamba wa vijia vikuu. Ndani ya kila chumba kulikuwa na kitanda kilichochongwa kwenye ukuta na kutandazwa kwa nyasi kavu. Sehemu iliyotumiwa kama hospitali ilikuwa na vitanda halisi na chumba cha upasuaji. Wanawake walipika juu ya jiko la mbao lililojengwa kwa mawe ya chokaa ya manjano, nao moshi ulipitia bomba lililotokea juu ya ardhi.”

Dari la vijia hivyo ilionekana kama sifongo kubwa ya asili, lakini unapoigusa si laini. Kulikuwa na alama za msumeno ukutani mahali ambako mawe yalikuwa yamekatwa. Kuta zilikuwa kama msasa. “Watu walipoenda nje, walibadili mavazi kwa kuwa Wajerumani wangeweza kunusa harufu ya mavazi yao,” akaeleza yule aliyekuwa akitutembeza. “Unyevunyevu ulioko chini ya ardhi ulifanya nguo ziwe na harufu fulani ya kipekee.”

Alituambia hivi pia, “Kulikuwa na mambo mengine yasiyo ya kawaida chini ya ardhi, kama vile kuishi gizani.” Alizima taa na tukabaki gizani. Kisha akasema, “Hawangeweza kutumia taa za mafuta kila wakati.” Tulipokuwa tukipapasa-papasa ukutani, akaongeza na kusema: “Kuta hizi humeza sauti, hivi kwamba ukipaaza sauti wakati umepotea huwezi kusikika.” Aliyekuwa akitutembeza alituhurumia na akawasha taa tena!

Aliendelea kusema hivi, “Walinzi walifanya kazi kwa zamu ya saa mbili peke yake kwa kuwa mtu akikaa muda mrefu gizani bila kusikia sauti yoyote, anaweza kuanza kuchanganyikiwa.” Shimo lililokuwa juu ya kijia hicho, lilituwezesha kuona vijia vingine vilivyokuwa vikipita juu yetu. Nilijiuliza: ‘Vijia hivyo vinatoka wapi na vinaelekea wapi?’ Nilihisi kana kwamba ninataka kufanya uchunguzi. “Tumefaulu kuchunguza na kuweka kwenye ramani kilomita 1,700 tu za vijia hivyo, kwa hiyo bado kuna kazi nyingi sana ya kufanya,” akatueleza.

Wavumbuzi wa karibuni wamegundua vijia vingine vya chini ya ardhi. Humo ndani walipata magazeti, taa zinazotumia mafuta za zamani sana, na pesa zilizotumiwa katika siku za maliki. Vitu hivyo—ambavyo havijatumiwa kwa miaka mingi—vilimilikiwa na wakazi wa zamani wa vijia hivyo vyenye giza vya chini ya ardhi vya Odessa.—Tumetumiwa makala hii.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

UJENZI WENYE THAMANI

Bado kuna majengo maridadi yaliyojengwa kwa kutumia mawe ya chokaa ya manjano katika jiji la Odessa. Majengo fulani yana milango inayoelekea moja kwa moja kwenye vijia vya chini ya ardhi. Majengo mapya yanaendelea kujengwa kwa kutumia mawe ya chokaa.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Vitanda vya hospitali vilivyotumiwa na Wasovieti wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Inasemekana kwamba vijia vya chini ya ardhi vya Odessa vina urefu wa kilomita 2,500