Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uhai Katika Bonde la Kifo

Uhai Katika Bonde la Kifo

Uhai Katika Bonde la Kifo

MNAMO 1848, dhahabu ilipatikana karibu na Sacramento, California, Marekani. Kufikia mwaka uliofuata, karibu watu 80,000 wanaotafuta hazina walihamia jimbo hilo wakitarajia kutajirika haraka. Desemba 25, 1849 (25/12/1849), watu waliokuwa katika kikundi kimoja kati ya magari 100 ya kukokotwa yaliyokuwa yakielekea magharibi kutoka Salt Lake City, waliingia eneo ambalo sasa linaitwa Bonde la Kifo. Walitarajia kwamba wangefupisha safari yao kwa kuvuka bonde hilo kame lililo karibu na mpaka wa California na Nevada.

Bonde hilo halikuwa na joto katika kipindi hicho cha mwaka, lakini ilikuwa hatari kulivuka. Watu hao walijipanga katika vikundi kadhaa, huku kila kimoja kikichukua njia tofauti. Kikundi kimoja, kilichotia ndani wanawake na watoto, kilijitahidi bila mafanikio kupata njia ya kutoka katika bonde hilo na kuingia kwenye milima iliyokuwa upande wa magharibi. Wakiwa wamechoka sana na kupungukiwa na chakula, walipiga kambi karibu na bubujiko katika eneo ambalo sasa linaitwa Kijito cha Furnace, halafu wakasonga mbele hadi kwenye shimo la maji lililokuja kuitwa Kisima cha Bennett. Wengine walibaki hapo huku William Manly na John Rogers, waliokuwa na umri wa miaka 20, wakienda kutafuta msaada.

Manly na Rogers walitarajia kufika Los Angeles baada ya siku chache. Hawakuwa na habari kwamba jiji hilo lilikuwa kilometa 300 hivi upande wa kaskazini magharibi. Baada ya kupiga miguu kwa majuma mawili hivi, walifika kwenye Bonde la San Fernando, lililo kaskazini mwa jiji hilo. Walinunua vitu walivyohitaji nao wakashika njia kurudi walikotoka.

Walipofika kambini baada ya siku 25, hawakumkuta yeyote. Manly alifyatua risasi, na mwanamume fulani akatoka chini ya behewa. Manly aliandika hivi baadaye: “Alirusha mikono yake hewani huku akipaaza sauti, ‘Wale wavulana wamekuja!’” Watu wale wengine wakatokea, wakiwa wamelemewa na hisia wasiweze kusema lolote. Kwa sababu ya jitihada za Manly na Rogers, wote walisalimika, ila mtu mmoja tu, aliyeondoka kambini na kujaribu kulivuka bonde hilo akiwa peke yake. Kikundi hicho cha walowezi kilipokuwa kikiondoka katika bonde hilo, inasemekana kwamba mwanamke mmoja alitazama nyuma na kusema, ‘Kwaheri, Bonde la Kifo!’ Hilo likawa jina la bonde hilo.

Mandhari na Hali Zinazotofautiana Sana

Bonde hilo lenye urefu wa kilometa 225 hivi na upana wa kati ya kilometa 8 hadi 24, ndilo eneo kame zaidi, lililo chini zaidi, na lenye joto zaidi huko Amerika ya Kaskazini. Kiwango cha joto katika Kijito cha Furnace kimefikia digrii 57 Selsiasi, huku joto la ardhi likifikia digrii 94 Selsiasi. Imebaki digrii 6 tu joto hilo lifikie kiwango cha maji kuchemka! *

Kwa wastani kiwango cha mvua hakifiki sentimeta 5 kwa mwaka, na miaka mingine mvua hainyeshi kamwe. Eneo lililo chini zaidi katika maeneo yote ya Kizio cha Magharibi, yaani, meta 86 chini ya usawa wa bahari, liko karibu na kidimbwi chenye maji ya chumvi huko Badwater. Mlima Whitney wenye urefu wa meta 4,418—ambao mbali na Alaska ndio eneo lililo juu zaidi huko Marekani—uko kilometa 140 hivi kutoka hapo.

Kufikia 1850, dhahabu kidogo ilikuwa imepatikana katika bonde hilo huko Salt Spring. Wavumbuzi wa eneo hilo walipata pia fedha, shaba, na risasi. Kotekote katika bonde hilo, miji yenye majina ya kuvutia kama vile Bullfrog, Greenwater, Rhyolite, na Skidoo, iliinuka kwa sababu ya uchimbuaji. Lakini hazina hizo zilipoisha, miji hiyo iliyokuwa imeinuka ghafula ikaachwa ukiwa. Hata hivyo, mnamo 1880, borax, ambayo ni kemikali nyeupe inayotumiwa kutengeneza sabuni na bidhaa nyinginezo, iligunduliwa katika Bonde la Kifo, na huo ukawa mwanzo wa kipindi muhimu zaidi cha uchimbuaji katika eneo hilo. Hadi 1888, vikundi vya nyumbu 18 na farasi 2 vilitumiwa kuvuta magari mawili-mawili ya kukokotwa yenye urefu wa meta 5 yaliyojazwa borax na kufunga safari ngumu ya kilometa 270 hadi kwenye mji wa Mojave. Lakini kemikali hiyo haikusafirishwa kati ya Juni (Mwezi wa 6) na Septemba (Mwezi wa 9) kwani hakuna mtu wala mnyama ambaye angeweza kustahimili joto la msimu huo.

Bonde la Kifo lilifanywa kuwa hifadhi ya kitaifa mnamo 1933. Polepole mipaka yake ilipanuliwa hadi hifadhi hiyo ikawa na ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 3.3. Katika 1994, eneo hilo likawa Mbuga ya Kitaifa ya Bonde la Kifo, ambayo ni mojawapo ya mbuga kubwa zaidi za kitaifa nchini Marekani.

Bonde la Kifo Lina Viumbe Tele

Tunaweza kuelewa kwa nini watu hufikiri kwamba hakuna viumbe wowote huko Bonde la Kifo. Hata hivyo, mamia ya aina za wanyama huishi au hupitia eneo hilo, na wengi wao huendesha shughuli zao usiku kwa sababu mchana kunakuwa na joto kali. Mnyama mkubwa zaidi anayepatikana huko ni kondoo anayeitwa desert bighorn, ambaye mara kwa mara hutoka kwenye milima iliyo karibu na kuteremka kwenye bonde hilo. Viumbe wengine wanatia ndani wibari, popo, bobcat, mbweha, panya wanaoitwa kangaruu, simba wa milimani, nungunungu, sungura, vicheche, punda wa mwituni, mijusi, nyoka, na kobe wa jangwani. Kuna ndege kama vile kiluwiri, mwewe, kulasitara, kware, kunguru, chamchanga, tai, na mamia ya ndege wa aina nyinginezo.

Viumbe sugu zaidi miongoni mwa viumbe hao ni panya wa kangaruu. Wanaweza kuishi maisha yao yote bila kunywa hata tone moja la maji! “Maji yote wanayohitaji ili waendelee kuishi wanaweza kuyapata kutokana na wanga na mafuta ya mbegu kavu wanazokula,” anasema mtafiti mmoja. Na figo zao huchuja maji kwenye mkojo mara tano zaidi ya figo za wanadamu. Panya hao wadogo wanaochimba mashimo ardhini, huepuka joto kali la mchana kwa kuendesha shughuli zao usiku.

Zaidi ya aina elfu moja za mimea husitawi katika bonde hilo. Washoshone, yaani, Wenyeji wa Asili wa Amerika ambao wameishi hapo kwa zaidi ya miaka elfu moja, walikuwa wakila baadhi ya mimea hiyo na kuitumia kutengenezea vyombo. Wanasema kwamba kuna vyakula vingi kwenye Bonde la Kifo ikiwa tu unajua mmea unaofaa.

Jangwa Linapochanua

Mara kwa mara, maua mengi ya msituni huchanua huko Bonde la Kifo. Maua hayo huota kutokana na mbegu chungu nzima zilizo mchangani—nyingine zimekuwa mchangani kwa makumi ya miaka—zikisubiri mvua na joto la kadiri inayofaa ili ziote. “Miaka mingi hupita bila maua yoyote kuchanua,” anasema Tim Croissant, mtaalamu wa mimea wa Huduma za Mbuga za Kitaifa.

Lakini katika majira ya baridi kali ya 2004/2005, Bonde la Kifo lilipata kiwango cha juu zaidi cha mvua kuwahi kurekodiwa—zaidi ya mara tatu ya kiwango cha kawaida. Hilo lilisababisha kutokea kwa zaidi ya aina 50 za maua ya mwituni, kutia ndani larkspur, lilaki, okidi, mipopi, primrose, alizeti, na verbena. Mgeni mmoja alisema kwamba bonde hilo lilikuwa na harufu nzuri kama duka la maua. Bila shaka, maua yaliyochanua huwavutia nyuki na wadudu wengine. Hivyo Bonde la Kifo linapochanua, unaweza kusikia sauti za mabawa madogo yasiyohesabika yakipigwa-pigwa.

Ukiamua kutembelea bonde hilo lenye mandhari na hali zinazotofautiana sana, hakikisha kwamba una gari zuri na maji mengi sana. Na iwapo utalitembelea katika majira ya nyuki, usikose kubeba kamera yako. Washiriki wa familia na rafiki zako watastaajabia kuona picha za viumbe wengi wanaopatikana Bonde la Kifo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Kiwango cha sasa cha joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa ni digrii 58.0 Selsiasi, nacho kilifikiwa mnamo 1922 nchini Libya. Hata hivyo, kwa ujumla katika majira ya kiangazi, yaonekana Bonde la Kifo ndilo eneo lenye joto kali zaidi duniani.

[Blabu katika ukurasa wa 15]

Eneo kame zaidi, lililo chini zaidi, na lenye joto zaidi huko Amerika Kaskazini

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Samaki Jangwani!

Aina nne za samaki mdogo wa ajabu anayeitwa desert pupfish huishi huko katika Bonde la Kifo. Katika majira ya baridi kali, samaki hao wenye urefu wa sentimeta sita, walio na rangi ya fedha hulala bila kufanya chochote kwenye matope katika sakafu ya vidimbwi na vijito vya eneo hilo. Wao huanza tena shughuli zao na pia hujamiiana wakati jua linapopasha joto maji ya vijito na vidimbwi hivyo. Kisha samaki wa kiume hubadili rangi yao na kuwa ya buluu, nao hulinda vikali maeneo yao yasivamiwe na samaki wengine wa kiume. Lakini muda si muda, joto la majira ya kiangazi hukausha maji mengi sana na samaki hao hufa kwa wingi. Wale wanaosalimika hulazimika kuishi kwenye maji ambayo huwa na kiwango cha juu cha chumvi na yanayoweza kufikia nyuzi 44 Selsiasi.

[Hisani]

Top fish: © Neil Mishalov—www.mishalov.com; bottom fish: Donald W. Sada, Desert Research Institute

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Marekani

California

Mbuga ya Kitaifa ya Bonde la Kifo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Mules: Courtesy of The Bancroft Library/University of California, Berkeley

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Burros: ©Joseph C. Dovala/age fotostock; top panorama: © Neil Mishalov—www.mishalov.com; flowers: Photo by David McNew/Getty Images