Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mwaka uliopita ulikuwa mwaka “wenye joto jingi zaidi kurekodiwa katika Kizio cha Kaskazini” na ndio uliokuwa mwaka wa “pili wenye joto zaidi ulimwenguni.” “Miaka kumi iliyopita ilikuwa na miaka minane kati ya miaka 10 yenye joto jingi zaidi [kurekodiwa].”—SHIRIKA LA UTANGAZAJI LA UINGEREZA.

Mwaka wa 2005 ndio uliokuwa mwaka wenye “tufani nyingi” na “inasemekana . . . tufani hizo zilisababisha uharibifu mkubwa” zaidi kuwahi kurekodiwa. Tufani saba kati ya 14 zilizorekodiwa zilikuwa na upepo uliovuma kwa kilometa 177 kwa saa.—SHIRIKA LA KITAIFA LA USIMAMIZI WA BAHARI NA ANGA LA MAREKANI.

“Mnamo 1850, kulikuwa na zaidi ya miamba 150 ya barafu katika Mbuga ya Kitaifa ya Barafu huko Montana [Marekani]. Sasa kuna miamba 27 tu.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.

“Ukweli ulio wazi kuhusu sera za serikali mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa joto la dunia ni kwamba, hakuna nchi ambayo itakubali kufanya mabadiliko ili kutatua tatizo hilo ikiwa mabadiliko hayo yataathiri uchumi wa nchi hiyo.”—TONY BLAIR, WAZIRI MKUU WA UINGEREZA.

Je, Wakatoliki Wahubiri “Nyumba kwa Nyumba”?

Cláudio Hummes, askofu mkuu wa São Paulo anasema kwamba idadi ya Wabrazili ambao ni Wakatoliki imepungua kutoka asilimia 83 hadi asilimia 67 katika miaka 14 iliyopita. Askofu huyo anasema kwamba “kwa sababu mbalimbali [kanisa] limeshindwa kuwahubiria injili kikamili waumini wake waliobatizwa.” Hummes anasema hivi: “Tunapaswa kuwahubiria watu nyumba kwa nyumba, shuleni, na kwenye taasisi mbalimbali, bali si ndani ya makanisa tu.” Gazeti Folha Online linasema kwamba kazi hiyo itafanywa na waumini ambao wamezoezwa kuwa wamishonari. Upungufu wa makasisi ni mojawapo ya matatizo makubwa yanayolikumba Kanisa Katoliki huko Brazili na nchi nyingine zote za Amerika ya Latini.

Kuandikishwa Kisheria Nchini Ujerumani

Katika uamuzi uliochapishwa Februari 10, 2006, Mahakama ya Utawala huko Leipzig, Ujerumani, iliamuru kwamba Jimbo la Berlin liliandikishe kisheria Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova nchini Ujerumani. Hatua hiyo ilikomesha mapambano ya kisheria ya miaka 15. Katika muda huo, kesi hiyo ilichunguzwa katika mahakama mbalimbali nchini Ujerumani kutia ndani Mahakama ya Katiba. Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova nchini Ujerumani ni shirika la umma, kwa hiyo halihitajiwi kulipa kodi nalo linapaswa kupewa haki za kisheria sawa na dini nyingine kuu nchini humo.

Vijana wa China Ni Waraibu wa Michezo ya Intaneti

“Uraibu wa michezo ya Intaneti umeenea sana miongoni mwa vijana wa China,” linasema gazeti South China Morning Post la Hong Kong. Tatizo hilo linaonekana pia miongoni mwa vijana wa nchi mbalimbali za Mashariki, kama vile Korea Kusini, Hong Kong, na Japani. Gazeti hilo linasema: “Tamaa inayokua ya kutumia Intaneti ili kujitenga na watu inaonyesha matokeo ya kudhibiti watoto kupita kiasi. Hilo husababishwa na matazamio yanayopita kiasi ya wazazi wanaotaka watoto wafaulu na ushindani mkali uliopo ili kuingia chuo kikuu.” Inakadiriwa kwamba watoto milioni sita hivi nchini China wanahitaji kusaidiwa kushinda uraibu huo.