Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Umajimaji Gani Ulio na Thamani Kubwa Zaidi?

Ni Umajimaji Gani Ulio na Thamani Kubwa Zaidi?

Ni Umajimaji Gani Ulio na Thamani Kubwa Zaidi?

“Damu ni muhimu kwa matibabu kama vile mafuta yalivyo muhimu kwa usafiri.”—Arthur Caplan, msimamizi wa kituo cha elimu ya maadili katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania.

MAFUTA. Je, huo ndio umajimaji ulio na thamani kubwa zaidi? Kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta, huenda watu wengi leo wakafikiri hivyo. Hata hivyo, kila mmoja wetu ana lita kadhaa za umajimaji wenye thamani kubwa zaidi. Hebu wazia: Kila mwaka mabilioni ya lita za mafuta hutolewa ardhini ili kutosheleza mahitaji ya wanadamu, huku painti milioni 90 za damu zikitolewa katika miili ya wanadamu ili kuwasaidia wagonjwa. * Kiasi hicho kikubwa sana cha damu chatoshana na damu ya watu 8,000,000 hivi.

Hata hivyo, sawa na mafuta, inaonekana kwamba kuna uhaba wa damu. Wataalamu wa tiba ulimwenguni pote wanasema kwamba kuna uhaba wa damu. (Ona sanduku “Jitihada za Kufa na Kupona.”) Lakini kwa nini damu ina thamani kubwa sana?

Kiungo cha Pekee

Mara nyingi damu huonwa kuwa kiungo cha mwili kwa sababu ya utata wake. “Damu ni moja kati ya viungo vya mwili ambavyo ni vya ajabu na vya pekee,” Dakt. Bruce Lenes alimwambia mwandishi wa Amkeni! Kweli damu ni kiungo cha pekee! Kitabu kimoja kinasema kwamba damu ndicho “kiungo pekee katika mwili ambacho ni cha umajimaji.” Kitabu hichohicho kinasema kwamba damu ni “mfumo hai wa usafirishaji.” Hilo linamaanisha nini?

Mwanasayansi N. Leigh Anderson anasema kwamba, mfumo wa kuzungusha damu ni kama mifereji inayopitisha maji safi na maji machafu. Damu inaposafiri kupitia mfumo wetu wa kuzungusha damu, ambao una urefu wa kilomita 100,000, hupitishwa katika kila tishu ya mwili wetu, kutia ndani moyo, figo, maini, na mapafu. Vyote hivyo ni viungo muhimu sana vinavyosafisha na kuitegemea damu.

Damu huingiza vitu vingi vizuri kwenye chembe za mwili wako kama vile oksijeni, virutubishi, na vitu vinavyokinga mwili. Damu pia huondoa uchafu kama vile kaboni dioksidi ambayo ni sumu, sehemu za chembe zilizoharibika au kufa, na takataka nyinginezo mwilini. Kazi ambayo damu hufanya, yaani, kuondoa uchafu mwilini huonyesha sababu inayofanya iwe hatari kugusa damu ikisha toka mwilini. Hakuna yeyote anayeweza kuthibitisha kwamba uchafu wote umegunduliwa na kuondolewa katika damu kabla haijatiwa ndani ya mwili wa mwingine.

Bila shaka, damu hufanya kazi muhimu sana ili kuendeleza uhai. Hiyo ndiyo sababu wataalamu wa tiba huwatia damu mishipani watu waliopoteza damu. Huenda madaktari wengi wakasema kwamba damu ina thamani kubwa sana kwa sababu inatumiwa katika matibabu. Hata hivyo, mambo yamekuwa yakibadilika katika nyanja za kitiba. Ni kana kwamba kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kimyakimya. Leo, madaktari wengi wanasita kuwatia wagonjwa damu. Kwa nini?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Painti moja ina mililita 450 za damu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

Jitihada za Kufa na Kupona

Wataalamu wa tiba wanakadiria kwamba kila mwaka, painti milioni 200 zaidi za damu zinahitajiwa ulimwenguni pote. Asilimia 82 ya watu duniani huishi katika nchi zinazositawi, lakini kiasi cha damu inayotolewa katika maeneo hayo haifiki asilimia 40. Hospitali nyingi katika nchi hizo hulazimika kuwatibu wagonjwa bila kutumia damu. Gazeti The Nation, nchini Kenya, linaripoti kwamba kila siku, karibu nusu ya wagonjwa wanaohitaji kutiwa damu mishipani hawatibiwi au matibabu yao huahirishwa kwa sababu ya ukosefu wa damu.

Hata nchi tajiri zinakumbwa na ukosefu wa damu. Kwa kuwa watu wanaishi muda mrefu kuliko vizazi vilivyotangulia na pia kwa sababu ya maendeleo ya kitiba, idadi ya watu wanaofanyiwa upasuaji imeongezeka. Isitoshe, watu wengi zaidi na zaidi hawakubaliwi kutoa damu kwa sababu huenda mtindo wao wa maisha au kusafiri kumewafanya waambukizwe magonjwa.

Inaonekana kwamba wataalamu wa kuhifadhi damu wamekuwa na wasiwasi. Nyakati nyingine vijana ambao kwa kawaida mtindo wao wa maisha hauhatarishi afya sana ndio wanaotafutwa ili watoe damu inayoonwa kuwa salama. Kwa mfano, wanafunzi hutoa asilimia 70 ya damu nchini Zimbabwe. Vituo vya kukusanya damu huwa wazi kwa saa nyingi zaidi, na nchi fulani huwalipa ridhaa watu wanaotoa damu ili kuwachochea wafanye hivyo tena na tena. Kampeni fulani katika Jamhuri ya Cheki iliwavutia watu watoe damu kwa kuwaandalia pombe kwa wingi! Katika eneo moja huko India, wenye mamlaka waliwatembelea watu nyumbani kwao wakiwatafuta wale wanaotaka kutoa damu ili kusaidia kuongeza akiba ya damu kwa kuwa hifadhi yao ilikuwa imepungua.