Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kahawa Isiyo na Kafeini

Gazeti El País la Hispania linaripoti kwamba wanasayansi wa Brazili wamegundua aina fulani ya mmea wa kahawa unaoitwa Coffea arabica unaozaa kahawa iliyo na kiasi kidogo sana cha kafeini. Mmea huo hukuzwa sana. Kahawa hiyo ambayo kiasili ina kiasi kidogo sana cha kafeini hukuzwa huko Ethiopia, na ugunduzi huo utafaidi sana biashara ya kahawa. Asilimia 10 hivi ya watu ambao hunywa kahawa ulimwenguni hupenda kahawa isiyo na kafeini, na idadi yao inaongezeka. Tunda la kahawa huwa na miligramu 12 za kafeini kwa kila gramu moja, lakini aina hiyo iliyogunduliwa ina miligramu 0.76 kwa kila gramu moja. Gazeti El País linaripoti hivi: “Kazi ya kuondoa kafeini inayofanywa viwandani hugharimu pesa nyingi, na wanasayansi wanasema kwamba hiyo huharibu kafeini na vilevile vitu muhimu vinavyofanya kahawa iwe na ladha yake ya kupendeza.” Kwa hiyo, mmea huo uliogunduliwa utatatua matatizo hayo.

Kinachowafanya Buibui Wasianguke

Gazeti The Times la London linasema: “Wanasayansi wamevumbua kile kinachowawezesha buibui kujishikilia ukutani na darini. Buibui ana miguu minane. Mwishoni mwa kila mguu kuna nywele ndogo, na kila unywele una nywele ndogondogo. Uwezo wa kunata ulio kwenye mguu wenye nywele ndogondogo 624,000 ni wenye nguvu sana hivi kwamba buibui anaweza kubeba kitu kinachozidi uzito wake kwa mara 170 hivi, huku akijishikilia ukutani au darini. Watafiti huko Ujerumani na Uswisi walichunguza mguu wa buibui mmoja kwa kutumia darubini ya pekee. Gazeti The Times, linasema kwamba uchunguzi huo unaonyesha kuwa “inawezekana kuiga mbinu hizo ili kutengeneza gundi mpya zinazonata sana” ambazo “haziwezi kuathiriwa na mvuke.” Kiongozi wa kikundi hicho cha watafiti, Profesa Antonia Kesel anasema kwamba kwa kuiga buibui “wataalamu wa anga wanaweza kuvalia mavazi yanayowawezesha kujishikilia kwenye vyombo vya angani.”

Utekaji Nyara Nchini Mexico

Toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald liliripoti kwamba kulingana na shirika moja la usalama, nchi ya Mexico ndiyo nchi ya pili iliyo na visa vingi vya utekaji nyara katika Amerika ya Latini. Kolombia ndiyo nchi iliyo na visa vingi zaidi. “Inasemekana kwamba kulikuwa na visa 3,000 vya utekaji nyara [katika mwaka wa 2003].” Hata hivyo, visa vingi haviripotiwi kwani familia za waliotekwa hupendelea kutatua tatizo hilo kibinafsi. Pia, idadi hiyo haitii ndani visa vya watu kutekwa na kulazimishwa kutoa pesa kwenye mashine za benki kisha kuachiliwa. Kulingana na gazeti hilo, inakadiriwa kwamba visa 16 vya aina hiyo hutukia kila siku huko Mexico City, lakini huenda kukawa na visa 80 kila siku. Inahangaisha kwamba visa hivyo vimezidi kuwa na jeuri na watu wengi zaidi wanaotekwa huuawa, hata baada ya fidia kulipwa.

Ongezeko Kubwa la Watu Wenye UKIMWI

Jarida The Wall Street Journal linaripoti kwamba katika mwaka wa 2003, watu milioni tano waliambukizwa virusi vya UKIMWI, “na hiyo ni idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ugonjwa huo ulipozuka miaka 20 iliyopita.” Pia jarida hilo linasema: “Watu wengi zaidi wanaambukizwa na mamilioni ya watu hufa kila mwaka kutokana na UKIMWI licha ya jitihada nyingi za ulimwenguni pote za kupambana na ugonjwa huo katika nchi zinazoendelea.” Kulingana na habari zilizochapishwa na Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS), watu milioni 3 hivi hufa kila mwaka kutokana na UKIMWI na zaidi ya watu milioni 20 wamekufa tangu ugonjwa huo ulipogunduliwa mwaka wa 1981. Mradi huo unakadiria kwamba kwa sasa watu milioni 38 wana virusi vya UKIMWI. Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ndizo zimekumbwa zaidi na ugonjwa huo kwani watu milioni 25 huko wameambukizwa, na zinafuatwa na nchi za Asia Kusini na Asia Kusini-Mashariki ambako watu milioni 6.5 wameambukizwa ugonjwa huo. Gazeti hilo linasema kwamba “ulimwenguni pote, karibu nusu ya watu wanaoambukizwa virusi vya UKIMWI ni vijana walio kati ya umri wa miaka 15 na 24.”

Vijana Wanaosinzia

Gazeti ABC la Kihispania linaripoti hivi: “Siku hizi watu wanaona kuwa kulala ni kupoteza wakati.” Gazeti hilo linaongeza hivi: “Hata watoto wadogo hulala kwa muda mfupi sana kuliko muda unaohitajiwa ili kuwa na afya nzuri ya kiakili na ya kimwili.” Kulingana na Kituo cha Usingizi cha Hospitali ya Dexeus huko Barcelona, watoto wanaokosa kulala huwa na wasiwasi, hukasirika-kasirika, hawafanyi vizuri shuleni, huvunjika moyo, na huenda wakakua polepole. Wataalamu wanasema kwamba vijana wengi hawalali vya kutosha kwa sababu ya kutumia kompyuta, televisheni, simu za mkononi, na michezo ya video kabla tu ya kwenda kulala. Vifaa hivyo hupunguza wakati ambao watu hutumia kulala na kuwazuia wasipumzike kabla ya kulala. Mwanasaikolojia Victoria de la Fuente anasema hivi: “Watoto huambiwa kwamba kuvuta sigara hudhuru, lakini hakuna anayewaambia kwamba wanapaswa kulala vya kutosha.” Pia anasema: “Tusipochukua hatua, watoto hao watakuwa na matatizo ya kukosa usingizi watakapokuwa watu wazima.”

Miti Inayozuiwa Isiwe Mirefu Sana

Gazeti Las Vegas Review-Journal linasema hivi: “Ijapokuwa miti ya redwood ndiyo mirefu zaidi duniani kati ya vitu vyote vilivyo hai, haiwezi kupita urefu fulani hata ikiwa chini ya hali nzuri sana.” Uchunguzi uliofanywa kuhusu mti mrefu zaidi duniani (wenye urefu wa meta 110, ambao unakaribia kulingana na jengo lenye orofa 30) na miti mingine minne ya aina hiyo ulionyesha kwamba mti wa redwood hauwezi kupita urefu wa meta 130. Mvuke unapovukizwa kutoka kwenye majani, maji yaliyo kwenye mizizi huvutwa hadi juu ya mti, na kukiuka nguvu za uvutano. Watafiti wanakadiria kwamba maji hayo yanaweza kusonga kwa siku 24. Maji yanapovutwa kupitia sehemu zinazoitwa zilemu, uzito wake huongezeka sana hivi kwamba yanashindwa kufika juu, na hivyo kuzuia ukuzi wa mti. Mti wa Douglas fir, ambao ndio mti mrefu zaidi kuwahi kuwepo duniani, ulifikia urefu wa meta 126 hivi.

Simu Yenye Sala kwa Ajili ya Waislamu

Sasa kuna simu za mkononi zinazouzwa kwa ajili ya Waislamu. Kulingana na gazeti la Kijerumani Die Zeit, simu hiyo ina Kurani nzima na pia imeundwa katika njia ambayo inaweza kuwaita Waislamu kwa ajili ya swala mara tano kwa siku. Pia simu hiyo huonyesha jiji la Mecca liko upande gani kutoka majiji zaidi ya 5,000 ulimwenguni. Tarehe zinaweza kuonyeshwa kwa kutumia kalenda ya Gregory au kalenda ya Kiislamu ya Hijri. Ingawa simu hiyo huuzwa kwa bei ghali sana, kituo kimoja kikuu cha Kiislamu kimeipendekeza.

Dunia Inazidi Kuwa na Giza

Gazeti Scientific American linasema hivi: “Wanasayansi wamegundua kwamba katika miaka ya karibuni kiasi cha mwangaza wa jua unaofika duniani kimepungua. Jua linatoa mwangaza kama kawaida lakini mawingu, uchafuzi wa hewa, na gesi zenye sumu zinazuia mwangaza wake.” Tangu mwishoni mwa miaka ya 1950 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, vifaa vingi sana vya kupimia vimeonyesha kwamba kiasi cha mwangaza wa jua kilichofika duniani kilipungua kwa asilimia 10 hivi. Mwangaza huo ulipungua zaidi katika Asia, Ulaya, na Marekani. Kwa mfano, mwangaza katika mji wa Hong Kong umepungua kwa asilimia 37. Wanasayansi wanasema kwamba bado jambo hilo halijaeleweka kabisa.