Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Ukuta Mkubwa wa China Unaporomoka

“Thuluthi mbili za Ukuta Mkubwa wa China zimeharibiwa na watalii, wajenzi, na mmomonyoko,” laripoti gazeti The Guardian la London. “Ukuta huo, ambao ni kati ya vitu vya pekee vinavyohifadhiwa ulimwenguni, unaporomoka. . . . Inasemekana kwamba sehemu za ukuta huo zimeharibiwa, zimeandikwa-andikwa na kubomolewa ili zitumiwe kujenga mabanda ya nguruwe na migodi ya makaa ya mawe.” Hivi karibuni, Hazina ya Kimataifa ya Minara ya Ukumbusho ambayo inafafanua ukuta huo kuwa “mojawapo ya maeneo makubwa ya kitamaduni duniani,” iliorodhesha ukuta huo katika orodha yake ya kila mwaka ya majengo yaliyo hatarini zaidi ulimwenguni. Hata wale ambao wamekabidhiwa daraka la kutunza ukuta huo wameshiriki kuuharibu. Katika kisa kimoja, inasemekana kwamba “maafisa wa kuhifadhi ukuta huo ambao hawakuwa na pesa za kutosha na ambao hawakuwa wamezoezwa ifaavyo kufanya kazi yao” walimpa mtu mmoja ruhusa ya kubomoa sehemu yenye urefu wa meta 14 ambayo ilijengwa miaka 600 iliyopita. Ukuta huo ulipojengwa ulikuwa na urefu wa kilometa 6,400. Kwa kuwa ni mrefu sana, ni vigumu kuutunza ifaavyo.

Viumbe Wanaojificha Melini

Kikundi cha wanamazingira kinachoitwa Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni kinaonya hivi: “Maji yanayoingizwa ndani ya meli ili kuisawazisha na kuifanya iwe thabiti huwa na maelfu ya viumbe wa majini ambao wanaweza kuingia katika maeneo mengine maji hayo yanapomwagwa bandarini.” Viumbe hao ambao wanatia ndani viwavi wa baharini na mwani “wanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kama ule unaotokea wakati mafuta yanapomwagika baharini,” yasema ripoti moja ya shirika la Reuters. “Viumbe wanaoendelea kuishi hadi meli zinapofika bandarini wanaweza kusitawi sana katika maeneo mapya kwa sababu hakuna viumbe wa kuwawinda wala vimelea.” Viumbe hao wanatia ndani kome fulani waliotoka Ulaya na kuingia katika eneo la Maziwa Makuu huko Amerika Kaskazini, magugu-maji kutoka Asia ambayo yalipelekwa Australia, na viwavi wa baharini kutoka Amerika Kaskazini ambao walipelekwa kwenye Bahari Nyeusi. Inakadiriwa kwamba ulimwenguni pote, tani bilioni kumi za maji ya kusawazisha meli humwagwa kila mwaka. Andreas Tveteraas, msemaji wa Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni, alisema hivi: “Kwa sasa hakuna njia nzuri zisizogharimu pesa nyingi za kusafisha maji ya kusawazisha meli.”

Intaneti na Visa vya Kujiua

Kulingana na makala moja katika gazeti The Times la London, bado talaka, ukosefu wa kazi, matumizi ya dawa za kulevya, na ulevi huonwa kuwa visababishi vikuu vya “ongezeko kubwa la visa vya kujiua miongoni mwa vijana wa kiume” nchini Uingereza na Wales. Hata hivyo, watu wanahangaishwa sana na vituo vya Intaneti ambavyo vinawawezesha vijana kuwasiliana na kupanga kujiua. Gazeti hilo linasema hivi: “Intaneti huwavutia watu ambao wanakabili uwezekano mkubwa wa kujiua, yaani, vijana wa kiume. Asilimia 75 ya visa vya kujiua huwa vya wanaume, na asilimia 80 kati ya visa hivyo ni vya wanaume walio kati ya umri wa miaka 15 na 24.” Inaelekea kuna maelfu ya vituo vya Intaneti vya aina hiyo, navyo huitwa vituo vya kifo. Makala hiyo inaongeza hivi: “Watu wengi wanaowasiliana kupitia vituo hivyo wanahisi kwamba hawapendwi na inaelekea kwamba tayari wamefikiria kujiua, au wamekwisha jaribu kufanya hivyo, navyo vituo hivyo huwapa mashauri mengi ili wasibadili maoni yao.” Vituo fulani huwachochea watu wanaofikiria kujiua kutimiza nia yao.

Barua za Mungu

Kila mwaka, shirika la posta la Israel “hutuma mamia ya barua zilizoandikiwa Mungu,” laripoti gazeti The Economist. “Barua hizo hutoka sehemu zote za ulimwengu, wakati wote wa mwaka, lakini watu humwandikia Mungu barua hasa kabla ya sherehe za kidini kama vile Krismasi au Yom Kippur.” Barua hizo huwa za kumsifu, kumlalamikia, au kumwomba Mungu, na mara nyingi watu humwomba Mungu msamaha au msaada. Barua hizo huenda wapi? “Barua ambazo zina anwani za watu waliozituma hurudishwa kwa wenyewe,” lasema gazeti The Economist. “Zile nyingine hupelekwa kwenye Ukuta (“Unaolia”) wa Magharibi huko Jerusalem, zikiwa na anwani ya rabi mkuu, ili ziingizwe katika nyufa za ukuta huo mtakatifu. Ikionekana kuwa mwandishi wa barua si Myahudi, barua yake itapelekwa kwa wizara ya mambo ya kidini.” Hata hivyo, kulingana na makala hiyo, “barua za Mungu hupelekwa mara moja au mbili kwa mwaka.” Sasa shirika la simu la Israel “limeanzisha anwani ya faksi ya Mungu na vilevile anwani ya barua-pepe kwa ajili ya wale ambao wangependa kuwasiliana na Mungu haraka.”

Uharamia Waongezeka

Kulingana na Idara ya Kimataifa ya Mambo ya Bahari ya ICC, “mwaka uliopita, visa vya uharamia viliongezeka ulimwenguni pote na vilikuwa vya kijeuri zaidi, kwani visa 445 viliripotiwa ikilinganishwa na visa 370 katika mwaka wa 2002 . . . Idadi ya visa ambavyo maharamia walitumia bunduki viliongezeka kutoka 68 katika mwaka wa 2002 hadi 100, na idadi ya watu waliotekwa nyara iliongezeka karibu mara mbili kufikia wasafiri 359. Katika visa 311, maharamia waliingia katika meli, na meli 19 zilitekwa nyara.” Mabaharia na abiria 71 waliripotiwa kutoweka, hali watu 21 waliuawa, na hiyo ilizidi idadi ya mwaka uliotangulia kwa watu 11. Kwa mara nyingine tena visa vingi vya uvamizi wa maharamia vilitukia katika maeneo ya bahari ya Indonesia kwani kulikuwa na visa 121, na Bangladesh ndiyo iliyofuata ikiwa na visa 58, kisha Nigeria ikiwa na visa 39. Idara hiyo inasema kwamba “visa vyote vya utekaji-nyara vilivyoripotiwa vilikuwa vya aina mbili.” Aina moja ilikuwa ya “mashambulizi kama ya kijeshi yaliyofanywa na vikundi vya wanamgambo ili kupata pesa za kuendeleza miradi yao kwa kuwateka watu nyara, na aina ya pili ilihusisha mashambulizi dhidi ya mashua ndogo-ndogo.”

Uchunguzi Kuhusu Makasisi Wanaowachafua Watoto

Gazeti The New York Times linaripoti kwamba “miradi miwili ya uchunguzi iliyosubiriwa kwa muda mrefu ilifunua kwamba Kanisa Katoliki [la Marekani] lilihusika katika visa vingi vya kuwachafua watoto kingono, ambavyo vilihusisha angalau asilimia 4 ya makasisi kwa kipindi cha miaka 52, huku asilimia kubwa zaidi ikiwa ya makasisi waliotawazwa mwaka wa 1970, kwani asilimia 10 ya makasisi hao walishtakiwa kwa kuwachafua watoto. Inasemekana kuwa watoto 10,667 walichafuliwa na makasisi 4,392 tangu 1950 hadi 2002, lakini kulingana na uchunguzi huo idadi hizo si kamili,” kwani visa vingi havikuripotiwa. Uchunguzi mmoja uliofanywa kwenye chuo cha John Jay College of Criminal Justice huko New York, ulionyesha kwamba “katika zaidi ya asilimia 95 ya madayosisi na pia katika asilimia 60 hivi ya makao ya kidini, makasisi walihukumiwa kwa kuwachafua watoto kingono.” Katika uchunguzi wa pili, uliofanywa na kamati ya kitaifa ya Kikatoliki, iligunduliwa kwamba katika vyuo vya Kikatoliki kuna zoea la “kuruhusu mwenendo mpotovu.”

Inapendekezwa Kufanya Mazoezi kwa Kiasi

Gazeti FDA Consumer linaripoti kwamba “kufanya mazoezi kwa kiasi, kama vile kutembea kilometa 20 kila juma, kunaweza kuzuia kuongeza uzito na kusaidia kupunguza uzito bila kujinyima vyakula fulani.” Uchunguzi uliofanywa kwa miezi minane uliowahusu “wanaume na wanawake 182 ambao wamenenepa sana walio kati ya umri wa miaka 40-65 na ambao hawafanyi mazoezi,” ulithibitisha “kwamba kuna uhusiano ulio wazi kati ya kufanya mazoezi na kupunguza uzito.” Wahusika waligawanywa katika vikundi vinne na wakaruhusiwa kuendelea kula kama kawaida. Vikundi vitatu vilifanya mazoezi kwa viwango tofauti-tofauti. Kikundi cha nne hakikufanya mazoezi yoyote. Makala hiyo inasema hivi: “Wakati wa uchunguzi huo, kikundi cha nne kiliongeza uzito. Watu katika vile vikundi vingine walipunguza uzito sana kiunoni na mapajani kwa kulinganisha na kikundi cha nne.” Uchunguzi huo unadokeza kwamba mara nyingi uzito unaweza kupunguzwa kwa kufanya mazoezi kwa kiasi, kama vile kutembea kwa nusu saa kila siku.