Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Soko la Samaki Lililo Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Soko la Samaki Lililo Kubwa Zaidi Ulimwenguni

Soko la Samaki Lililo Kubwa Zaidi Ulimwenguni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPAN

JE, WEWE hufurahia kukurukakara za soko? Soko moja ambalo huenda ukalifurahia na ambalo huwavutia watalii wengi kutoka ulimwenguni kote ni lile soko la samaki la Tsukiji, ambalo haliko mbali na katikati ya Tokyo. Inasemekana kwamba hilo ndilo soko kubwa zaidi la samaki ulimwenguni.

Wakati unaofaa kwenda huko ni asubuhi na mapema. Shughuli za soko huanza wakati ambapo wakazi wa Tokyo wamelala. Malori huleta tani elfu mbili za samaki kila siku na wote hao hupakuliwa na kupangwa mapema kwa sababu kufikia saa 9:00 za usiku, wanunuzi huanza kuingia. Wauzaji huharakisha kupanga masanduku yao ya samaki, wakiyatia alama inayoonyesha nambari yake, uzani wa samaki, na mahali walipovuliwa. Ni rahisi kuwatambua wanunuzi. Wao huvaa buti za mpira na kofia zenye nambari ya leseni zao. Tofauti na watalii wanaokwenda polepole, wanunuzi hukimbia huku na huku wakichunguza ubora wa samaki na kuamua watawanunua kwa bei gani. Wanunuzi wa samaki aina ya tuna hubeba ndoana, tochi, na taulo. Ndoana na tochi hutumiwa kukagua tuna, na taulo ni ya kujipangusa mikono baada ya kushika samaki.

Vurumai huanza saa 11:30 alfajiri. Kelele za kengele husikika kotekote huku madalali wakiwaita wanunuzi. Ni kana kwamba madalali wako kila mahali. Lakini kuna wauzaji saba tu wa jumla ambao huendesha shughuli zao wakati uleule na baadhi yao wana madalali wawili au zaidi wanaouza bidhaa tofauti wakati uleule. Madalali hao wote hutaja kwa sauti mbalimbali nambari za sanduku, na wanunuzi wenye kibali hushindania bei wakitumia ishara za vidole. Shughuli hiyo hufanywa haraka-haraka hivi kwamba bei huamuliwa kwa sekunde chache tu. Wanunuzi fulani hujaribu kununua samaki kwa madalali wawili wakati uleule. Kila duka linaruhusiwa mnunuzi mmoja tu, kwa hiyo ni lazima wanunuzi wakimbie kutoka sehemu moja mpaka nyingine ili wapate samaki wanaotaka. Labda wanunuzi wenye hekaheka nyingi zaidi ni wale wanaonunua samaki wengi zaidi na wa aina mbalimbali ili wawauze katika maduka tofauti-tofauti.

Mara tu bei inapoamuliwa, wanunuzi husafirisha samaki haraka iwezekanavyo. Waendeshaji wa mikokoteni na malori madogo hupita kasi kwenye barabara nyembamba wakibeba samaki. Kila mahali kuna pilikapilika, kukurukakara, na kelele. Mgeni anaweza kufikiri ghasia zimezuka. Lakini mambo yote ni shwari na yanafanyika kwa utaratibu kabisa. Kwa muda wa saa chache tu, zaidi ya tani elfu moja za samaki huuzwa na kusafirishwa. Samaki wengine hupelekwa kwenye maduka madogo yaliyo kwenye sehemu nyingine ya soko ambako huuzwa asubuhi kwa maelfu ya wanunuzi.

Kama unavyoweza kuwazia, Soko la Tsukiji ni kubwa. Makampuni saba makubwa na zaidi ya wafanyabiashara elfu moja wadogo wamejiandikisha kufanya biashara hapo. Kila siku ya mwaka, wafanyabiashara hao huwahudumia wanunuzi 40,000 hivi katika soko hilo.

Wanunuzi hao ni akina nani? Wanatia ndani wanunuzi wa hoteli, mikahawa, na maduka makubwa wanaonunua samaki wengi. Pia, wanunuzi wanatia ndani watu wenye maduka madogo ya kuuza vyakula, wauzaji katika masoko ya samaki mtaani, na hata watu wanaouza mlo wa sushi kwenye maduka yao maridadi. Wanunuzi hao hung’ang’ania samaki bora. Inakadiriwa kwamba wao hununua karibu tani 600,000 za viumbe wa baharini kila mwaka, ambao hugharimu zaidi ya dola bilioni 5.

Tsukiji si soko la samaki tu. Ni soko la jumla linalouza matunda na mboga pia. Ni mojawapo ya masoko ya jumla 11 jijini Tokyo yanayosimamiwa na serikali ya jiji hilo. Masoko ya vyakula yalianza katika mwaka wa 1603. Ili kudumisha usafi na ubora, masoko hayo yalianza kusimamiwa na serikali mnamo mwaka wa 1877. Tetemeko la ardhi la mwaka wa 1923 liliharibu masoko ya Tokyo, na baadaye Soko la Tsukiji la leo likajengwa. Lilifunguliwa mwaka wa 1935.

Tangu wakati huo, soko hilo limepanuliwa sana. Ni sehemu chache tu ulimwenguni zinazouza samaki wengi na wa aina mbalimbali jinsi hiyo. Inakadiriwa kwamba aina 450 za samaki kutoka ulimwenguni kote kama vile samoni, chewa, sea bream, kibua, wayo, na heringi, na vilevile mwanamizi, sea cucumber, na samaki-gamba zinauzwa huko. Baadhi ya yale maduka madogo huuza aina moja tu ya viumbe wa baharini, kama vile pweza au uduvi.

Hata hivyo, kuna samaki mmoja aliye mkubwa kuliko wote. Ni tuna, ambaye huletwa kwa ndege kutoka sehemu za mbali kama vile Bahari ya Mediterania na Amerika Kaskazini. Hakuna samaki anayelingana naye kwa ukubwa au kwa bei. Tuna mmoja mkubwa anaweza kuuzwa kwa maelfu ya dola. Mamia ya tuna wabichi waliohifadhiwa kwenye barafu huuzwa hapa kila siku. Wanunuzi hukata tuna vipande-vipande na kuwauzia wafanyabiashara. Sehemu zenye mafuta zinazoitwa toro, zinazokatwa ubavuni, hutumiwa kutengeneza mlo wa sushi.

Si ajabu kwamba soko kubwa zaidi la samaki ulimwenguni liko nchini Japan. Nchi hiyo inazungukwa na bahari nne na Wajapani wamependa bidhaa za baharini toka zamani. Mara nyingi, samaki huwa sehemu kuu ya mlo mtamu wa Wajapani. Kila mwaka, Mjapani wa kawaida hula kilogramu 70 za samaki na viumbe wa baharini, na wengi hununuliwa katika Soko la Tsukiji. Kwa hiyo siku moja ukitembelea Tokyo, kwa nini usijiunge na watalii wengine wanaotembelea soko kubwa zaidi la samaki ulimwenguni?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Fish artwork: From the book L’Art Pour Tous, Encyclopedie de l’Art Industriel et Decoratif, Vol. 31, 1861-1906

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

James L. Stanfield/NGS Image Collection

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

© Jeff Rotman/www.JeffRotman.com

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Courtesy of Tokyo Metropolitan Central Wholesale Market