Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Dubu wa Ncha ya Kaskazini Wamo Hatarini

“Dubu wa ncha ya kaskazini wanakabili hatari kubwa ya kuangamia kwa sababu ya ongezeko la joto,” lasema gazeti la Nassauische Neue Presse la Ujerumani, kuhusu ripoti ya uchunguzi wa Shirika la Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni (WWF). Shirika hilo linasema kwamba barafu ya bahari ya Aktiki—makao na eneo la kuwinda la dubu wa ncha ya kaskazini—inapungua kwa sababu ya kuongezeka kwa joto. Wataalamu wanasema kwamba joto la wastani katika Aktiki ‘limeongezeka kwa nyuzi 5 [za Selsiasi] katika muda wa miaka 100 iliyopita.’ Isitoshe, “barafu ya baharini imepungua kwa asilimia 6 katika muda wa miaka 20 iliyopita,” na “inatazamiwa kwamba kufikia mwaka wa 2050 itakuwa imepungua kwa asilimia 60 katika majira ya joto.” Upungufu wa barafu na vipindi virefu vya joto huwazuia dubu kuwinda na hivyo hawawezi kuhifadhi mafuta yanayohitajika mwilini. Wanaoathiriwa zaidi ni dubu majike na watoto wao. Gazeti hilo lasema kwamba katika maeneo fulani “ni vigumu kwa nusu ya watoto hao kuokoka kipindi hicho cha joto kinachozidi kuwa kirefu.” Dubu hao wanakabili matatizo mengine kama vile “uwindaji, kemikali zenye sumu, na mafuta yaliyomwagika kwenye maji.”

Mikalitusi Huathiri Mawasiliano ya Simu za Mkononi

Gazeti la Sydney Morning Herald la Australia lasema kwamba “katika sehemu nyingi za [jimbo la New South Wales], mawasiliano ya simu za mkononi si mazuri yakilinganishwa na yale ya Ulaya na Marekani.” Tatizo hilo liko hasa kusini mwa jimbo hilo karibu na Mto Murray. Hata ingawa eneo hilo ni tambarare, “simu hukatika ghafula au hata haziingii kabisa.” Ripoti hiyo yasema kwamba tatizo hilo linasababishwa na “miti mingi ya [mikalitusi] inayokaribiana sana katika bonde la Mto Murray.” Roger Bamber, mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano ya simu, “anaamini kwamba umbo, ukubwa na kiwango cha mvuke unaotoka kwenye majani ya mikalitusi hufyonza mawimbi ya simu za mkononi zaidi ya majani ya miti mingine,” lasema Herald.

Kutiwa Damu Kunaweza Kudhuru Mapafu

Jarida la FDA Consumer, linalochapishwa na Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani linasema kwamba “watu ambao hutiwa bidhaa za damu, hasa bidhaa zenye plazima, wanakabili hatari ya kupata ugonjwa hatari wa mapafu unaotokana na kutiwa damu.” Ugonjwa huo unaweza kusababisha kifo usipogunduliwa na kutibiwa ifaavyo. “Ugonjwa huo unaweza kutokea wakati kingamwili za chembe nyeupe za damu iliyotolewa zinapoathiri chembe nyeupe na tishu za mapafu zinazopitisha umajimaji katika mwili wa mgonjwa. Mara nyingi damu inayotolewa na wanawake wenye watoto zaidi ya wawili au watu wengine waliowahi kutiwa damu mara kadhaa huwa na athari hiyo.” Dalili za ugonjwa huo ni kama vile “mafua, kushindwa kupumua, na kushuka kwa shinikizo la damu. Mara nyingi picha za eksirei huonyesha mapafu ya mtu aliyetiwa [damu] hiyo yakiwa meupe pepepe.”

Nyuki Wauawa kwa Sumu

Gazeti la Kifaransa Marianne linauliza, “Je, tutaweza kutumia asali yoyote kutoka Ufaransa miaka 10 ijayo?” Mamilioni ya nyuki wanauawa kwa sumu wakati wa majira ya kuchipua, na hilo limepunguza uzalishaji wa asali nchini Ufaransa kutoka tani 45,000 mwaka wa 1989 hadi 16,000 mwaka wa 2000. Katika juma moja tu, mfugaji mmoja wa nyuki alipoteza mizinga 450 yenye nyuki milioni 22! Wazalishaji wengi wa asali husema kwamba hasara hiyo inasababishwa na kemikali zinazotumiwa katika kilimo kama vile dawa za kuua wadudu, hasa dawa kali za bei nafuu ambazo huingizwa nchini kimagendo. Baadhi ya wakulima wametia kwenye kemikali hizo mafuta yaliyotumiwa ya injini au dawa ya kuondoa madoa ili ziwe na nguvu zaidi! Hatua isipochukuliwa, “kuna uwezekano kwamba asali ya Ufaransa itasahaulika kabisa,” lasema gazeti la Marianne.

Watoto Hawajui Kifo

“Je, unafikiri kwamba mtu anapokufa anaweza kufufuliwa?” Profesa Hiroshi Nakamura wa Chuo Kikuu cha Wanawake nchini Japan, aliwauliza wanafunzi 372 wa madarasa ya juu katika shule ya msingi swali hilo. Thuluthi moja ya wanafunzi hao walijibu ndiyo, na thuluthi nyingine hawakuwa na uhakika, laripoti gazeti la Sankei Shimbun la Tokyo. “Hali hiyo inatokana na michezo ya kompyuta ambapo, bingwa akifa, mchezaji humhuisha tena kwa kubonyeza tu kompyuta,” lasema gazeti hilo. Kulingana na profesa huyo, uchunguzi huo “ulionyesha kwamba hata wanafunzi wengi wa madarasa ya juu katika shule ya msingi hawajui kwa usahihi kifo ni nini.” Alidokeza kwamba wazazi wawafundishe watoto kuhusu kifo wakitumia wanyama-vipenzi na kuwaruhusu wawatembelee watu wao wa ukoo wanaokaribia kufa.

Yatangazwa Kwamba Hakuna Ugonjwa wa Polio Ulaya

Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba “hatua muhimu zaidi kuhusiana na afya ya umma katika milenia mpya” kwa watu milioni 870 wanaoishi Ulaya, ilifikiwa katika Juni 2002 ilipotangazwa kwamba eneo hilo halina ugonjwa wa polio. “Hakuna mwenyeji yeyote aliyeugua ugonjwa wa polio kwa zaidi ya miaka mitatu” katika nchi 51 za Ulaya. Matokeo hayo yalikamilisha mradi wa miaka 14 wa kukomesha polio kupitia kampeni za kitaifa za chanjo. Tayari ugonjwa huo umekomeshwa huko Amerika na Pasifiki ya Magharibi. Ugonjwa huo unaoenea haraka sana husababishwa na virusi vinavyoshambulia mfumo wa neva, na unaweza kumfanya mtu apooze au hata afe. Kwa sasa ugonjwa huo unaweza tu kuzuiwa lakini hauwezi kutibiwa.

Ukosefu Mkubwa wa Maji

Gazeti la BMJ (ambalo hapo awali liliitwa British Medical Journal) lasema, “ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, afya ya zaidi ya nusu ya watu ulimwenguni itaathiriwa sana na ukosefu wa maji kufikia mwaka wa 2032.” Ripoti ya Umoja wa Mataifa imegundua kwamba ingawa idadi ya watu wanaopata maji safi “imeongezeka kutoka bilioni 4.1 mwaka wa 1990 hadi bilioni 4.9 mwaka wa 2000, bado watu bilioni 1.1 wanaoishi katika nchi zinazoendelea hawana maji safi ya kunywa. Watu bilioni 2.4 hawana vyoo safi vya kutosha.” Kwa sababu hiyo “watu bilioni nne huugua ugonjwa wa kuhara na milioni 2.2 hufa kila mwaka,” mbali na wale wenye matatizo ya minyoo, ugonjwa wa kichocho, na ugonjwa wa macho.

Ngozi ya Kupachikwa

Ngozi ya binadamu ndiyo kiungo kikubwa sana mwilini na ndiyo kinga ya kwanza dhidi ya viini vya magonjwa, kupoteza maji, na kupungua kwa joto la mwili. Kwa hiyo, watu wanaokabili hatari kubwa zaidi ni wale wenye vidonda vilivyo wazi ambao wameungua na watu wenye ugonjwa wa sukari. Kwa kawaida wagonjwa hupachikwa ngozi ya watu waliokufa ambayo haipatikani kwa urahisi. Isitoshe, ngozi iliyopachikwa inaweza kuambukiza magonjwa au ikataliwe na mwili. Gazeti The News la Mexico City linasema kwamba sehemu fulani za utumbo mdogo wa nguruwe hupandikizwa bila matatizo kwenye miili ya wagonjwa wenye vidonda sugu. Sehemu ya utumbo wa nguruwe ambayo hutumiwa inafanana sana na ngozi ya binadamu na hupatikana kwa urahisi. Daktari-mpasuaji anayerekebisha viungo vya mwili Jorge Olivares, anayefanya majaribio ya kupachika ngozi, asema: “Wagonjwa ambao nimetibu wana makovu machache sana, na vidonda vyao hupona baada ya majuma machache. Faida za upasuaji huo ni kwamba maumivu ya wagonjwa hupungua haraka sana.”

Apotea Baharini kwa Miezi Minne

Tauaea Raioaoa, mvuvi mwenye umri wa miaka 56, alinusurika baada ya kupotea katika Bahari ya Pasifiki Kusini kwa miezi minne, yasema ripoti ya gazeti la Tahiti Les Nouvelles de Tahiti. Aliondoka Tahiti Machi 15, 2002, “kwa mashua yake ndogo ya kijani yenye urefu wa meta 8, iliyoitwa ‘Tehapiti.’ Mota ya mashua yake iliharibikia mbali na pwani ya Tahiti.” Aliokolewa mnamo Julai 10 karibu na kimojawapo cha Visiwa vya Cook, kinachoitwa Aitutaki, kilicho umbali wa kilometa 1,200, akiwa amepoteza uzito wa zaidi ya kilogramu 20. Raioaoa, mvuvi stadi na mwenye uzoefu aliishi kwa “kula samaki wabichi au waliokaushwa na kunywa maji ya mvua aliyochota kwa ndoo na kwa sanduku la barafu.”