Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kazi Yangu Si ya Kawaida Lakini Naipenda

Kazi Yangu Si ya Kawaida Lakini Naipenda

Kazi Yangu Si ya Kawaida Lakini Naipenda

SAUTI ndogo ya mashua yangu ya kipekee ndiyo tu inayosikika ninapoondoka kwenye bandari iliyotulia ya mji wa Gibsons. Kumepambazuka—ni wakati wa kuanza kazi.

Watu wengi wanaofanya kazi katika pwani ya magharibi ya Kanada, kama mimi, hufanya kazi zinazohusiana na kupanda na kukata miti. Lakini ni watu wachache tu wanaofanya kazi isiyo ya kawaida kama yangu. Mimi huokota magogo yaliyoanguka baharini. Kazi hiyo imefanywa kwa muda mrefu. Ama kweli, mababu wa baba zetu walifanya kazi hii pia. Ninafanya kazi katika eneo la Howe Sound na Mlango-Bahari wa Georgia, kati ya Kisiwa cha Vancouver na pwani ya British Columbia. Eneo hilo ni sehemu ndogo tu ya Eneo la Kuokota Magogo la Vancouver.

Makampuni ya kukata miti husafirisha magogo hasa kwa kuyaweka katikati ya vizuizi fulani baharini ili yapelekwe na maji au kwa kuyasafirisha kwa mitumbwi. Kusafirisha magogo majini au kwa mashua hakugharimu pesa nyingi. Na katika eneo hili kuna maji mengi yanayotoka kwenye Bahari ya Pasifiki. Hata hivyo, kuna mambo mengi yanayofanya kazi hiyo iwe ngumu. Maji ya kujaa na kupwa na upepo hubadilika haraka, na dhoruba hutokea ghafula. Hivyo, magogo mengi hupotea. Ndiyo sababu watu fulani hufanya kazi ya kuyaokota magogo hayo.

Kuokota Magogo Yaliyopotea

Waokotaji wa magogo huhitajika kuwa na leseni ili waokote na kuuza magogo yaliyopotea au yaliyoanguka kutoka kwenye mitumbwi. Waokotaji hao hulipia leseni hiyo kila mwaka. Wanapopewa leseni hiyo mara ya kwanza, wao hupewa pia muhuri wenye namba ya leseni yao. Magogo yanayoruhusiwa kuokotwa ni yale tu yanayopatikana yakielea au yale yaliyo ufuoni ambayo hayajafika mahali ambapo maji ya kujaa hufikia. Kwanza, sisi huyapiga muhuri magogo hayo ili yawe na namba yetu.

Pia ni muhimu kuwa na mashua inayofaa. Mashua hii ni tofauti na zile zinazotumiwa kwa ajili ya tafrija. Sisi hutumia mashua ndogo thabiti—ziwe ni zile zilizo na mota kwenye sehemu ya nyuma, au zile zinazotumiwa kuvuta mashua nyingine. Mashua hizo zina kiunzi kipana sana. Sehemu ya mbele ya mashua hizo ina vyuma ambavyo hutumiwa kusukuma magogo. Pia, sisi huwa na kamba za kutosha. Kamba hizo zina msumari mkubwa kwenye ncha moja. Kamba hizo huwa na urefu wa meta 4 au 5 hivi. Tunapopata gogo, sisi hugongomea msumari huo ndani ya gogo hilo na kufunga kamba hiyo kwenye mlingoti fulani kwenye mashua. Isitoshe, sisi hubeba vifaa vya kuzuia hatari.

Mtu anayeanza kufanya kazi hiyo kwa mara ya kwanza atagundua kwamba hiyo si kazi rahisi. Kazi huanza alfajiri na mapema mwaka mzima na inafanywa katika hali zote za hewa. Katika majira ya baridi kali, nyakati nyingine sisi hulazimika kuvunja barafu bandarini ili kupata njia.

Magogo hupatikana wapi? Hilo linategemea mambo mawili: kujaa na kupwa kwa maji, na upepo. Kabla ya kuanza kazi asubuhi, mwokotaji wa magogo mwenye ujuzi huangalia ratiba inayoonyesha wakati ambapo maji yatajaa na kupwa. Wakati mzuri zaidi ni pindi ambapo maji yanapojaa sana kwani magogo mengi husukumwa. Zaidi ya hayo, ni rahisi kuvuta magogo ufuoni wakati huo.

Ni muhimu sikuzote kuchunguza hali ya hewa. Sisi huchunguza daima jinsi pepo zinavyovuma, anga na mawingu, na rangi ya maji. Upepo unaotoka kusini-mashariki huleta mvua, huku pepo zinazovuma toka upande wa magharibi husababisha anga jangavu na mawimbi mengi. Katika majira ya baridi kali, upepo unaotoka kaskazini-mashariki, husababisha baridi kali, mawimbi mengi, theluji, na hivyo kusukuma magogo yaliyopotea.

Kugongomea misumari kwenye gogo linaloelea ni jambo la kusisimua, lakini kuvuta magogo hayo ufuoni husisimua hata zaidi. Miamba iliyofunikwa na maji inaweza kuvunja na kuharibu kiunzi cha mashua. Tunahitaji kuwa chonjo.

Tunapokusanya magogo hayo, sisi huyavuta na kuyaweka kwenye vibanda mbalimbali yakiwa yamefungwa. Yanakaa hapo hadi wakati wa kuyauza. Mara moja kwa juma, sisi hukusanya na kupeleka magogo yote tuliyookota—50 hadi 100 hivi—kwenye vituo mbalimbali ambako yanapimwa uzito na thamani yake kukadiriwa. Kisha, sisi hulipwa kulingana na thamani ya magogo hayo.

Huenda kazi hii ikaonekana kuwa yenye kufurahisha sana, lakini usikate kauli haraka hivyo! Kazi hii inahitaji ujasiri. Kuna hatari nyingi. Kupuuza hali ya hewa kwaweza kuwa hatari sana. Hata hivyo, eneo la Howe Sound lina sehemu nyingi za kujikinga na dhoruba. Kuna hatari nyingine pia: Mwokotaji wa magogo asipotahadhari na kuanguka ndani ya maji wakati wa baridi kali, maji hayo ya baridi yanaweza kumuua akikaa humo kwa dakika chache tu. Na je, unakumbuka zile kamba zenye misumari zilizotajwa awali? Msumari usipogongomewa kabisa kwenye gogo, unaweza kuruka hadi kwenye mashua. Lakini ni waokotaji wachache tu ndio wamewahi kugongwa na misumari hiyo—na hawawezi kusahau jambo hilo.

Faida kwa Mwokotaji na Mazingira

Je, wajua ni kwa nini naipenda kazi yangu? Eneo la Howe Sound linapendwa na watalii wengi, nao huenda huko kuendesha mashua zao. Na kwa kuwa kuna visiwa vingi, kuna mashua nyingi na mamia ya nyumba zinazotumiwa wakati wa likizo. Mashua hufanya kazi kutwa nzima kuwasafirisha wakazi na wageni. Kwa kuwa magogo yanayoelea majini ni hatari, kazi yetu ni muhimu sana.

Kwa kuokota magogo yaliyopotea, sisi huwaondolea hatari watu wanaotumia mashua. Magogo fulani ambayo yamekaa ndani ya maji kwa muda mrefu huanza kuzama. Nyakati nyingine, sehemu ndogo tu ya gogo ndiyo hujitokeza juu ya maji, na hiyo huwa hatari sana kwa watu wanaoendesha mashua. Hata hivyo, sisi huyaokota na kuyauza magogo hayo kwa sababu yana faida kwetu. Kwa kufanya hivyo, sisi huondosha hatari kwenye njia za majini na vilevile kusafisha mazingira.

Kazi hii hunisisimua na kunifurahisha. Kila siku ina mambo yake. Ninaposafiri kwa mashua, mandhari hubadilika-badilika. Nimeona jua likichomoza wakati wa baridi kali na kufanya theluji kwenye milima ionekane kuwa na rangi ya waridi. Wakati kama huo, mimi hufurahia ule mzizimo wa hewa baridi ya baharini.

Mara kwa mara mimi huwaona wanyama. Nimeona wanyama wengi kutia ndani fisimaji na makundi ya sili. Nimewatazama tai wakivua samaki na kulungu wakiogelea kutoka kisiwa kimoja hadi kingine karibu na pwani. Ni jambo lenye kustaajabisha kama nini kumwona pomboo akicheza-cheza karibu na mashua yangu, au makundi ya nyangumi yakiogelea na kukata mawimbi!

Babu yangu alianza kazi ya kuokota magogo katika miaka ya 1930. Aliwasaidia wanawe kupenda kazi yake ya kuokota magogo. Kisha, babangu aliwasaidia watoto wake pia kupenda na kuheshimu kazi hii. Nilipokuwa mtu mzima, niliamua kufanya kazi hii pia. Ama kwa hakika, hii si kazi ya maana zaidi maishani mwangu. Kumtumikia Mungu ndilo jambo la kwanza—na kunathawabisha hata zaidi. Lakini pia nimependelewa kufurahia kazi yangu ya kujiruzuku kwa muda mrefu—kwa miaka 50 hivi. Kila siku, mimi hutazamia kwa hamu kwenda kutafuta magogo.

Familia yangu hunisaidia pia. Katika majira ya joto, nyakati nyingine sisi sote huenda kutafuta magogo ufuoni wakati wa jioni. Tunapovuta magogo yetu bandarini huku jua likitua nyuma yetu, shakwe wakilia juu yetu, mashua yetu ikikata maji, na taa zikianza kumweka ufuoni, sote tunapata amani na kuhisi tukiwa karibu na Muumba. Ama kweli, hiyo ndiyo sababu kuu inayofanya niipende kazi yangu.—Tumetumiwa makala hii.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mwokotaji wa magogo afunga gogo lililopatikana ufuoni

[Picha katika ukurasa wa 10]

Sisi huwaona wanyama tunapotafuta magogo

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kituo cha kupokea magogo huko Howe Sound hufunguliwa hata katika majira ya baridi kali