Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Twende Kwenye Karamu Nchini Hawaii

Twende Kwenye Karamu Nchini Hawaii

Twende Kwenye Karamu Nchini Hawaii

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HAWAII

UKITAJA jina Hawaii watu wengi watafikiria mambo kama vile mashada ya maua, mchezo wa hula, na minazi inayoyumbayumba. Mamilioni ya watu kutoka kila sehemu ya dunia huja Hawaii ili kuona mambo hayo na kushiriki katika karamu ya Hawaii inayoitwa luau ambayo inajulikana ulimwenguni pote. *

Katika jioni nzuri tulivu huko Hawaii upepo mwanana unavuma huku jua likishuka na kupotea polepole kwenye upande wa Bahari ya Pasifiki. Karibuni kwenye hoteli moja inayoandaa karamu za kienyeji za Hawaii kwa ukawaida. Ninaona mmejitayarisha ifaavyo, kwa kuwa nyinyi mabwana mmevalia shati za Hawaii zenye rangi nyingi na nyinyi mabibi mmevalia nguo ndefu zenye rangi nyang’avu. Tumefika mapema, kwa hiyo twende tuone jinsi chakula kinavyotayarishwa.

Tunapoingia karamuni, msichana mmoja ambaye amevalia sketi ya majani ya mti wa ti, kisha anatukaribisha na kumpa kila mmoja wetu shada la maua na kinywaji cha matunda. Kinywaji hicho huburudisha sana baada ya kutalii sehemu mbalimbali na kuota jua kwenye pwani siku nzima. Mbele yetu kuna meza zenye vyakula vizuri kama vile majimbi, viazi vitamu, samaki anayeitwa salmoni na vyakula vingine vinavyopendwa huku kisiwani.

Tunavutiwa na tuta linalotoa mvuke lililoko kando ya mahali pa kulia. Wanaume kadhaa wenye nguvu ambao wamevalia mashuka wanaondoa kwa uangalifu udongo na majani kutoka kwenye tuta hilo na kuyaweka kando. Punde tunaona nguruwe mzima aliyeokwa akitolewa ardhini. Nguruwe huyo atakuwa chakula kikuu kwenye karamu yetu. Huenda ukajiuliza, ‘Je, tutakula nyama hiyo? Inanukia vizuri, lakini haionekani kuwa tamu wala safi.’ Lakini, usiondoke. Acha nieleze jinsi mlo huo unavyotayarishwa na utaona kwamba chakula hicho ni safi kabisa. Ninajua utapenda kuonja chakula hicho kitamu cha kale cha Hawaii ukielewa jinsi kinavyotayarishwa.

Joko la Chini ya Ardhi

Wahawaii wa kale walitumia joko la chini ya ardhi, linaloitwa imu, kupika vyakula mbalimbali. Mbali na nguruwe, walipika samaki, kuku, ndege wadogo, na vilevile viazi vitamu, majimbi, shelisheli, na vitindamlo mbalimbali katika joko hilo. Hata majani ya viazi vitamu na ya miyugwa yalitumiwa katika upishi.

Yamkini vitu vidogo vilifungwa katika majani ya mti wa ti na kuokwa katika mivuke. Mbinu hiyo ya kupika inaitwa laulau. Na upishi unaotumia joko la chini ya ardhi unaitwa “kalua.” Neno hilo linamaanisha “shimo.” Kwa hiyo, chakula kikuu cha karamu yetu kinaitwa nguruwe wa kalua. Kama tutakavyoona, vyakula vinaokwa katika mivuke katika joko hilo la chini ya ardhi.

Wahawaii wa kale walichimba shimo kubwa lililotoshea vyakula vyote. Kwa kawaida kazi ilianza mapema asubuhi ili chakula kiwe tayari kwa ajili ya mlo wa jioni. Kuni zilipangwa vizuri chini shimoni ili ziwake kwa urahisi. Vijiti vinavyoshika moto haraka na vilevile kiasi cha kuni cha kutosha viliongezwa kwa utaratibu ili moto uendelee kuwaka kwa muda wa saa tatu au nne.

Kuni zilipangwa pande zote kuzunguka kijiti kilichosimama wima. Baadaye kijiti hicho kiliondolewa na majivu yenye moto yalitumbukizwa shimoni ili kuwasha moto. Moto uliwashwa kwa kusugua vijiti viwili pamoja. Kisha, mawe laini ya volkeno yaliwekwa juu ya kuni. Mawe ya volkeno yalitumiwa kwa kuwa hayakupasuka yalipopashwa moto. Mawe madogo yaliyotumiwa yalikuwa na ukubwa wa ngumi na yale makubwa zaidi yalikuwa na mzingo wa sentimeta 69. Mawe mengi yalihitajiwa kwa sababu mawe hayo na makaa yaliyobaki ndiyo yaliyotoa moto ili vyakula viive. Mawe yalipashwa moto hadi yakawa mekundu. Kisha kuni zisizoteketea zikaondolewa.

Baada ya mawe hayo kupanguswa yasiwe na majivu, mawe kadhaa yaliwekwa ndani ya tumbo na kifua cha nguruwe aliyekuwa ametiwa chumvi ili kuhakikisha anaiva vizuri. Mara nyingi mawe madogo yaliwekwa ndani ya kuku. Kisha mawe na makaa yaliyobaki yaliwekwa vizuri chini na kandokando shimoni na kufunikwa kwa nyasi na majani ya ti au ya ndizi. Mara nyingi mashina ya ndizi yalikatwa vipande-vipande na kutupwa juu ya mawe. Jambo hilo lilizuia vyakula visiungue kwa sababu ya moto mkali na kuongeza unyevu ili vyakula viokwe katika mivuke.

Baada ya kuweka majani ya kutosha shimoni, nguruwe aliwekwa juu ya majani hayo, pamoja na vyakula vingine vya mlo huo. Vyakula hivyo vilifunikwa kwa majani mengine mengi. Kisha kitambaa kilichotengenezwa kwa maganda ya mforosadi au mikeka ilitandikwa juu ya majani hayo ili kuzuia udongo usivichafue vyakula. Mwishowe tuta lote lilifunikwa kwa udongo mwingi, ili mivuke isiweze kutoka katika joko hilo. Nyakati nyingine tuta lilinyunyiziwa maji ili lisikauke, au mpishi alipoona ni lazima, mwanzi uliingizwa tutani na maji yakaongezwa kupitia huo.

Muda uliohitajiwa ili vyakula viive ulitegemea mambo mbalimbali, kama vile kiasi na aina ya chakula kilichowekwa katika joko na idadi ya mawe yaliyotumiwa. Yamkini ilichukua muda wa saa kadhaa ili nguruwe aive vizuri, ikitegemea ukubwa wake. Baada ya vyakula kuiva vizuri, udongo uliondolewa kwa uangalifu, kisha mikeka na majani yaliondolewa ili kufukua nyama iliyoiva. Vyakula viliwekwa katika vyombo, kisha vikawekwa mezani na kuliwa vikiwa baridi. Nyama isiyoiva vizuri ilikatwa na kupikwa baadaye au ilipikwa kwa njia nyingine, kama vile kuchoma au kuchemsha.

Kwa kuwa watu wa kale hawakuwa na vyombo visivyoshika moto, walipotaka kuchemsha vyakula waliviweka katika bakuli la mbao lenye maji, na mawe yenye moto sana yakatumbukizwa ndani yake. Huenda nyama isiyoiva ilitiwa chumvi ili ihifadhiwe kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Kwa kuwa upishi ulikuwa kazi ngumu, wanaume ndio waliofanya kazi hiyo. Ni wazi kwamba joko hilo lilitumiwa tena na tena. Mara nyingi lilikuwa ndani ya jengo fulani ili liweze kutumiwa hata wakati wa mvua.

Joko la Imu la Siku Hizi

Leo, kwenye karamu zetu utaona kwamba utumizi wa joko la imu haujabadilika sana. Siku hizi wavu wa waya hutumiwa mara nyingi kushikilia nguruwe wakati anapoondolewa shimoni kwa kuwa upishi huo unafanya nyama iwe laini hivi kwamba inakatika-katika. Magunia hutumiwa badala ya mikeka au vitambaa vya maganda ya mforosadi. Lakini zaidi ya mabadiliko hayo machache, joko la imu halijabadilika, ijapokuwa utamaduni wa Hawaii umebadilika sana.

Baada ya kutoa nyama kwenye mifupa, chumvi inaweza kuongezwa kulingana na mapendezi ya mtu. Kisha nguruwe wa kalua yu tayari kuliwa. Acha karamu ianze! Unaweza kuketi chini kwenye mkeka na kutumia meza fupi au unaweza kutumia meza na viti vya kawaida. Kwa vyovyote, tunajua utafurahia karamu yetu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Inawezekana kwamba karamu ya luau ilihusiana na dini ya uwongo zamani, lakini siku hizi neno hilo linamaanisha tu karamu inayofanywa nchini Hawaii. Kwa hiyo, huenda Wakristo wengi wasione ubaya wowote kushiriki katika karamu ya aina hiyo.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Si Lazima Uchimbe Shimo

Ukitaka kuonja chakula hicho kitamu cha Hawaii, yamkini itakubidi kuja huku Hawaii na kushiriki katika karamu yetu ya kienyeji. Lakini unaweza kupika mlo unaofanana sana na nguruwe wa kalua jikoni mwako.

Hata huku Hawaii hatuna wakati wa kutosha kutumia joko la imu kila wakati tunapotaka kula nguruwe wa kalua. Kwa hiyo, tunafanya upishi huo kwa njia rahisi ili kuokoa wakati. Badala ya kupika nguruwe mzima, huenda ukaweza kutumia tu tako la nguruwe au sehemu nyingine ya nguruwe inayoweza kuokwa. Hata unaweza kupika kuku au batamzinga ukitaka nyama isiyo na mafuta mengi. Kwa vyovyote, paka kikolezo kilicho na ladha ya moshi kwenye nyama yote. Tumia kijiko kimoja kikubwa cha kikolezo hicho kwa kila nusu kilogramu ya nyama. Kikolezo hicho kitafanya nyama iwe na ladha na harufu ya m̀oshi.

Ukiweza kupata majani ya ti, funga nyama kwa majani hayo. Weka nyama katika kifaa cha kupikia cha umeme kinachopika polepole, kwa kuwa kifaa hicho kina mvuke na moto sawa na joko la imu. Ikiwa huna kifaa hicho, unaweza kutumia joko lako la kawaida. Ili kuhifadhi unyevu kwa kadiri iwezekanavyo, funika nyama kwa karatasi ya alumini baada ya kuifunga kwa majani ya ti. Joto ndani ya joko linapaswa kuwa nyuzi 160 Selsiasi (nyuzi 325 Farenhaiti), na nyama inapaswa kupikwa vizuri kabisa. Nyama inapaswa kutoka kwenye mifupa kwa urahisi. Kata nyama vipande vidogo-vidogo na uinyunyizie umajimaji uliotoka katika nyama wakati ilipopikwa ili kuongeza unyevu. Sasa nguruwe wako wa kalua yuko tayari kwa ajili ya karamu yako ya luau.

Baada ya kuonja chakula hicho cha Hawaii, huenda ukashawishiwa kusafiri hadi Hawaii ili ufurahie nguruwe wa kalua aliyepikwa katika joko la chini ya ardhi.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ua la “Red hibiscus”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Vyakula kama vile majimbi, viazi vitamu, na samaki aina ya samoni vinapendwa kisiwani

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mchezo wa “hula”

[Hisani]

Ron Dahlquist/SuperStock

[Picha katika ukurasa wa 25]

Wageni hukaribishwa kwa kupewa shada la maua

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nguruwe wa “kalua” anaondolewa katika joko