Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hasara Zinazosababishwa na Mabwawa

Hasara Zinazosababishwa na Mabwawa

Hasara Zinazosababishwa na Mabwawa

IJAPOKUWA HAPO MBELENI mabwawa yalionwa kuwa njia bora ya kutokeza umeme na kuhifadhi maji, sasa, hayapendwi katika nchi nyingi. Gazeti la World Watch linasema hivi: “Mabwawa hayaonwi tena kuwa yenye faida kubwa. Utafiti unaonyesha kwamba hasara zinazotokezwa na yale mabwawa 45,000 makubwa yaliyopo duniani (yenye kuta zenye kimo cha zaidi ya meta 15), ni nyingi kuliko ilivyodhaniwa mbeleni.” Baadhi ya hasara hizo ni zipi?

Hasara moja kubwa ni uharibifu wa asilimia 60 ya mito mikubwa duniani. Gazeti la World Watch linasema hivi: “Mazingira ya viumbe wanaoishi katika mito yanaharibiwa kotekote duniani, kwa kuwa mito hiyo inakaushwa na kuchafuliwa, mikondo yake inageuzwa, na maji yake yanazuiwa ili kutengeneza mabwawa. Kuna angalau bwawa moja kubwa katika zaidi ya nusu ya idadi ya mito yote duniani . . . , kwa hiyo, uharibifu wa mazingira ya mimea na viumbe wa mtoni umesababishwa kwa kadiri kubwa na mabwawa. Kwa mfano, angalau asilimia 20 ya samaki wanaoishi katika maji yasiyo na chumvi kotekote ulimwenguni wamo hatarini au tayari wameangamia.” Samaki wanaoishi baharini kama vile samoni wameathiriwa pia kwa kuwa wanazuiwa na mabwawa wasiweze kufika mahali pao pa kutagia mayai mitoni.

Hata maoni ya watu wengi kwamba umeme unaotokezwa kwa maji hauharibu mazingira yanatiliwa shaka sasa. Kwa nini? Kwa kuwa mimea na mizoga inayooza hupelekwa na maji hadi kwenye mabwawa hayo nayo hutokeza gesi zinazoongeza joto ulimwenguni. Watu huumia pia. Watu milioni 40 hadi milioni 80 wamelazimishwa kuhama hasa kutoka maeneo ambayo ni yenye rutuba zaidi duniani. Hao ni watu wengi kuliko wakazi wa nchi nyingi.

Watu wengi wameanza kutambua hasara ya mabwawa. Kwa mfano, kotekote katika mito ya Marekani kuna mabwawa 75,000 yenye ukubwa mbalimbali. Sasa, Marekani ni nchi inayoongoza katika kubomoa mabwawa. Hata Benki ya Dunia imepunguza misaada inayotoa kwa ujenzi wa mabwawa.

Hata hivyo, mabwawa yana faida kadhaa. Lakini, kama ilivyo na jitihada nyingine nyingi za wanadamu, ujenzi wa mabwawa mengi sana umeonyesha ukosefu wa hekima na busara. Maneno haya ya nabii Yeremia yamethibitika kuwa kweli: “Kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”—Yeremia 10:23.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

PICHA: MOURA