Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ukweli Ulifichwa kwa Miaka 50—Mbona?

Ukweli Ulifichwa kwa Miaka 50—Mbona?

Ukweli Ulifichwa kwa Miaka 50—Mbona?

Rum ni kisiwa kidogo katika Inner Hebrides, karibu na pwani ya magharibi ya Scotland. Miaka 70 iliyopita, mmiliki wa kisiwa hicho alimruhusu mtaalamu wa mimea John Heslop Harrison, profesa wa chuo kikuu na mwanachama wa shirika maarufu la Uingereza la Royal Society, achunguze mimea ya kisiwa hicho.

Katika miaka iliyofuata, Harrison aliripoti kwamba aligundua jamii adimu za mimea kisiwani, mimea ambayo iliwahi kuonekana ikikua mamia ya kilometa upande wa kusini tu. Harrison alipokea sifa maridhawa, ugunduzi wake ulimletea sifa kenyekenye. Lakini kadiri orodha yake ilivyoongezeka, iliamsha shuku ya wataalamu wengine wa mimea.

Mnamo 1948, John Raven, profesa wa fasihi katika Cambridge na mtaalamu makini wa mimea mwenye ujuzi wa kadiri, alikubali kufanya uchunguzi. Lakini ripoti yake haikuwahi kuchapishwa. Badala yake ilifichwa kabisa, na ilifunuliwa mwaka wa 1999 tu. Mbona? Kwa sababu Raven alithibitisha kwamba Harrison alikuwa mlaghai. Gazeti New Scientist liliripoti kwamba mimea hiyo ilikuwa imekuzwa sehemu nyingine na kuhamishwa kisirisiri hadi Rum.

Raven alikuwa na ustadi wa ajabu wa ukuzi wa mimea kwenye mazingira yake na hivyo upesi akagundua kwamba miongoni mwa mizizi ya “uvumbuzi” kadhaa wa Harrison kulikuwemo magugu ambayo yalikuwa ya kawaida huko Uingereza lakini adimu katika Rum. Mimea mingine ilishambuliwa na mdudu fulani ambaye alikuwa ameonekana katika sehemu mbili pekee huko Uingereza—moja ikiwa ni shamba la Harrison katika Uingereza. Uthibitisho zaidi ulitokana na mizizi ya mmea fulani, iliyokuwa na chembe za jiwe la kwatzi—jiwe ambalo halipatikani kiasili popote katika Rum.

Kulikuwa na mengi zaidi. Maelezo ya Harrison kuhusu vipepeo na mbawakavu wa kisiwa hicho yalijulikana kuwa ya uwongo. Gazeti The Sunday Telegraph lilisema kwamba mkazi mmoja wa Rum alisema hivi: “Profesa alificha kitu fulani—ama kipepeo au mmea—wa kuvumbuliwa kila mwaka.” Kwa nini Harrison hakuchukuliwa hatua?

Mtafiti Karl Sabbagh akata kauli kwamba uamuzi wa kutochukua hatua ulikuwa fadhili ya kuilinda familia ya Harrison, lakini uhakika wa kwamba Harrison alikuwa mtu mashuhuri, na ikawa hatari kumpinga, huenda ulichangia pia. Sabbagh pia asema kwamba kufichua ulaghai wake “kungeziharibia sifa nyanja zote za utaalamu wa mimea.”