NOVEMBA 21, 2025
UKRAINIA

Ndugu Vitalii Kryushenko pamoja na mke wake, Olha, baada ya Vitalii kuachiliwa kutoka gerezani

Ukrainia Yamwachilia Ndugu Mmoja na Kuwafunga Wengine Watano Kwa Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Ukrainia Yamwachilia Ndugu Mmoja na Kuwafunga Wengine Watano Kwa Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Oktoba 27, 2025, Mahakama Kuu ya Ukrainia ilitoa uamuzi wa kumwachilia huru Ndugu Vitalii Kryushenko kutoka gerezani. Tangu Januari 2025, Vitalii amekuwa akitumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kuwa alikataa kutumikia jeshini kwa sababu ya dhamiri. Katika uamuzi huo uliotolewa na mahakama, mahakimu wote saba waliosikiliza kesi hiyo walikataa kumwondolea Vitalii hukumu ya hatia lakini walikubali kumpunguzia kifungo chake na kumwachilia. Hata hivyo, atakuwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja. Kwa sababu hiyo, Vitalii aliachiliwa na akaungana tena na mke wake, Olha. Vitalii alisema hivi baada ya kuachiliwa: “Mimi na Olha tumejionea mkono wa Yehova katika kipindi hiki kigumu. Nina uhakika kabisa kwamba Yehova atatenda na kulitukuza jina lake.”

Ndugu Andrii Kliuka anatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani

Kwa upande mwingine, ndugu watano kutoka sehemu mbalimbali za Ukrainia wamefungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Julai 16, 2025, Mahakama ya Wilaya ya Kamianets-Podilskyi ilimhukumu Ndugu Andrii Kliuka, mwenye umri wa miaka 40, kifungo cha miaka mitano gerezani. Hicho ndicho kifungo kirefu zaidi ambacho ndugu zetu wamepata tangu vita vilipoanza nchini Ukrainia. Mahakama iliamua kwamba Andrii ataendelea kukaa kizuizini hata ingawa amekata rufaa.

Isitoshe, katika mwezi wa Septemba na Oktoba 2025, mahakama mbalimbali ziliwaweka kizuizini Ndugu Yurii Hordynskyi, Ndugu Mykola Ivanskyi, Ndugu Vitalii Nedzelenko, na Ndugu Oleksii Rudov. Wamezuiliwa kwa kipindi kisichopungua miezi miwili kila mmoja wakisubiri kesi zao zisikilizwe. Katika visa fulani, ndugu hao walikamatwa ghafla na kuzuiliwa kwa lazima na maofisa wa polisi. Wote wanne walikamatwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kushoto kwenda kulia: Ndugu Yurii Hordynskyi, Ndugu Mykola Ivanskyi, Ndugu Vitalii Nedzelenko, na Ndugu Oleksii Rudov wamezuiliwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na wanasubiri kesi zao zisikilizwe

Tunafurahi kwamba Ndugu Vitalii Kryushenko ameungana tena na familia yake. Hata hivyo, bado ndugu zetu nchini Ukrainia wanakabili majaribu ya utimilifu wao. Licha ya mambo hayo, tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwapa nguvu wanazohitaji ili kuvumilia.​—1 Wakorintho 10:13.