Hamia kwenye habari

OKTOBA 9, 2013
UJERUMANI

Mnara kwa Ajili ya Shahidi Aliyeokoka Yale Maangamizi Makubwa Nchini Ujerumani

Mnara kwa Ajili ya Shahidi Aliyeokoka Yale Maangamizi Makubwa Nchini Ujerumani

SELTERS, Ujerumani—Juni 21, 2013, mnara uliwekwa wakfu kule Lautertal-Reichenbach kwa ajili ya Max Liebster, Shahidi wa Yehova aliyefungwa katika kambi za mateso za Nazi kwa miaka mitano. Meya na maofisa wengine wa jiji waliuweka wakfu mnara huo katika sherehe iliyohudhuriwa na wakaaji wa jiji hilo pamoja na mjane wa Bw. Liebster, Simone Liebster, ambaye pia ni Shahidi wa Yehova.

Bw. Liebster alikamatwa na Gestapo katika mwaka wa 1939 kwa sababu alikuwa Myahudi anayeishi nchini Ujerumani wakati wa utawala wa Nazi wa Hitler, na akafungwa katika kambi tano za mateso: Kambi za Sachsenhausen, Neuengamme, Auschwitz, Buna, na Buchenwald. Washiriki wanane wa familia yake walikufa katika kambi hizo. Mmoja kati ya waliokufa alikuwa baba yake, naye Bw. Liebster alilazimika kuubeba mwili wake hadi kwenye sehemu ya kuteketezea maiti ya Sachsenhausen.

Bw. Liebster alianza kushirikiana na wafungwa wenzake ambao ni Mashahidi wa Yehova katika kambi hizo za mateso. Alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova baada ya kufunguliwa mnamo 1945. Bamba moja la shaba ambalo lilipachikwa kwenye mnara wake linasema kwamba imani ya Bw. Liebster “ilimpa nguvu na utayari wa kuendelea kuishi.” Alikufa katika mwaka wa 2008 akiwa na umri wa miaka 93.

Kadi ya kuwakaribisha watu kwenye sherehe hiyo ya kuweka wakfu mnara huo inasema kwamba Bw. Liebster “alikuwa amesadikishwa kabisa kwamba viwango vya Kikristo vina uwezo wa kuwafanya watu watende kwa njia bora zaidi.” Wolfram Slupina, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Ujerumani, alitoa maelezo haya: “Tunafurahi sana kwamba ujasiri wa mmoja kati ya waumini wenzetu walioendelea kushikilia msimamo wao licha ya upinzani wa kidini umetambuliwa. Mnara huu ni wonyesho wa wazi kwamba ujumbe wa Biblia kuhusu amani na umoja ambao Mashahidi wa Yehova hujitahidi kuendeleza, una nguvu kwelikweli.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Ujerumani: Wolfram Slupina, simu +49 6483 41 3110