Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 29, 2020
AZERBAIJAN

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Maamuzi Mawili Kuunga Mkono Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Maamuzi Mawili Kuunga Mkono Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan

Septemba 24, 2020, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa maamuzi mawili muhimu kuunga mkono Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan. Uamuzi wa kwanza ulihusu kesi ya Valiyev and Others v. Azerbaijan (Valiyev na Wengine dhidi ya Azerbaijan), na uamuzi wa pili ulihusu kesi ya Religious Community of Jehovah’s Witnesses v. Azerbaijan (Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova dhidi ya Azerbaijan). Maamuzi hayo yanasaidia kulinda haki ya kisheria ya ndugu zetu kuendelea na utendaji wao wa kidini kwa uhuru.

Katika kesi zote mbili, serikali ya Azerbaijan ilitoa tangazo la kukubali kwamba ilikiuka haki za kisheria za ndugu zetu. Pia, serikali ilikubali kuwalipa ndugu zetu fidia ya jumla ya euro 19,000 (dola 22,146 za Marekani). Maamuzi ya ECHR yanaonyesha kwamba mahakama hiyo ilikubali tangazo hilo la Azerbaijan.

Ndugu Valiyev akiongoza mkutano katika nyumba ya kibinafs

Kesi ya Valiyev and Others v. Azerbaijan, iliyofikishwa mbele ya ECHR katika mwaka wa 2011, iliwahusu ndugu zetu katika jiji la Ganja. Kwa miaka mingi, wenye mamlaka katika jiji la Ganja walizuia tengenezo letu lisiandikishwe kisheria. Kwa sababu hiyo, maofisa wa polisi walikuwa na kawaida ya kuvuruga mikutano yetu ya kidini yenye amani, kuwakamata wote waliohudhuria, na kuwatoza faini kubwa baadhi ya wahudhuriaji. Ndugu mmoja alihukumiwa na kutozwa faini mara nyingi, hivi kwamba hatimaye alikuwa amelipa jumla ya Manat 9,450 za Azerbaijan (wakati huo zilikuwa dola 11,375 za Marekani). Baadhi ya ndugu na dada walikamatwa kwa sababu hawakuweza kulipa faini hizo kubwa.

Mnamo 2013, akina ndugu walifikisha kesi ya pili mbele ya ECHR, yaani, Religious Community of Jehovah’s Witnesses v. Azerbaijan kwa sababu serikali ya Azerbaijan ilidhibiti kiwango cha machapisho ambayo wangeweza kuingiza nchini.

Ingawa bado serikali haijaandikisha tengenezo letu kisheria katika jiji la Ganja, hali ni nzuri zaidi. Katika miaka ya karibuni, ndugu zetu wamefanya mikutano wakiwa vikundi vidogo katika nyumba za kibinafsi bila kuvurugwa na polisi. Isitoshe, ingawa machapisho yetu lazima yachunguzwe na serikali kabla ya kuingizwa nchini, serikali imewaruhusu ndugu zetu kuingiza kiasi kinachotosha cha machapisho.

Ndugu Kiril Stepanov, anayefanya kazi katika Dawati la Habari za Umma la Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan, anasema: “Tunatumaini kwamba uamuzi huu muhimu wa ECHR utaharakisha mchakato wa kuandikisha tengenezo letu kisheria katika jiji la Ganja na majiji mengine nchini Azerbaijan. Ni matumaini yetu kwamba baada ya muda serikali itaacha kuchunguza machapisho yetu kabla ya kuyaruhusu yaingizwe nchini.”

Tunamshukuru Yehova kwa utegemezo wake. Ushindi huo wa kisheria ni uthibitisho zaidi kwamba “hakuna silaha yoyote itakayotokezwa dhidi yako itakayofanikiwa.”—Isaya 54:17.