Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mnamo 2006, “waandishi 167 wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari,” kama vile madereva na watafsiri, “walikufa wakijaribu kuripoti habari.” Wengi walikuwa wakiripoti kuhusu uhalifu, ufisadi, au mapambano ya wenyewe kwa wenyewe. Wengine 133 waliuawa.—TAASISI YA KIMATAIFA YA USALAMA WA MASHIRIKA YA HABARI, UBELGIJI.

Kila mwaka, risasi zinazotosha kufyatuliwa mara bilioni 10 hadi 14 hutengenezwa. “Risasi [hizo] zinatosha kuua watu wote ulimwenguni mara mbili.”—TAASISI YA TEKNOLOJIA YA ROYAL HUKO MELBOURNE, AUSTRALIA.

Je, Matetemeko ya Nchi Yanaweza Kusababishwa na Wanadamu?

Tangu karne ya 19, shughuli za wanadamu zimesababisha zaidi ya matetemeko makubwa 200 ya nchi, inasema ripoti katika gazeti la Ujerumani Die Zeit. Uchimbaji-migodi ulisababisha nusu ya matetemeko hayo. Visababishi vingine huenda vikawa kuchimbuliwa kwa gesi, mafuta, au maji; kuingizwa kwa umaji-maji katika visima virefu; na kuchimbwa kwa mabwawa. Tetemeko la nchi lililotukia mnamo 1989 huko Newcastle, Australia, ambalo wanasayansi wanasema lilisababishwa na uchimbaji wa mgodi wa makaa ya mawe chini ya ardhi, lilisababisha vifo vya watu 13, majeruhi 165, na uharibifu wa mali unaokadiriwa kuwa dola bilioni 3.5. Inakadiriwa kwamba hasara iliyosababishwa na tetemeko hilo ilizidi jumla ya pesa zote zilizopatikana kwa kuchimba makaa ya mawe huko Newcastle tangu uchimbaji huo uanze karne mbili zilizopita.

Hali ya Wakatoliki wa Ufaransa

Mnamo 1994, asilimia 67 ya watu huko Ufaransa walidai kuwa Wakatoliki. Leo, ni asilimia 51 tu wanaodai hivyo, linasema gazeti Le Monde des Religions. Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kwamba nusu ya Wakatoliki wa Ufaransa hawaendi kanisani isipokuwa tu wakati wa matukio ya pekee, kama vile arusi. Ingawa asilimia 88 wanadai kujua sala ya Baba Yetu, asilimia 30 hawasali hata kidogo. Karibu nusu ya Wakatoliki wana Biblia nyumbani, lakini hilo halimaanishi kwamba wao huisoma.

Watoto Walio na Matatizo ya Usemi

“Watoto wengi zaidi wanaanza kuzungumza wakiwa wamechelewa mno na wanajifunza maneno machache tu . . . kwa sababu watu wazima hawazungumzi nao,” linasema gazeti la Poland Wprost. Kwa wastani, akina mama hutumia dakika 30 hivi kwa siku pamoja na watoto wao, nao akina baba hutumia “dakika saba tu.” Kwa sababu hiyo, mtoto 1 hivi kati ya kila watoto 5 “ana tatizo fulani la usemi linalosababishwa hasa na kupuuzwa na wazazi wake.” Michał Bitniok, mtaalamu wa usemi na lugha katika Chuo Kikuu cha Silesia, anaonya hivi: “Ikiwa watoto kama hao hawatibiwi mapema na wanaendelea kupuuzwa, matatizo hayo ya usemi yanaweza kuwafanya wapate matatizo shuleni na wanapokuwa watu wazima.”

Kutumia Ushirikina Nchini Japani

Kutupa takataka kwenye maeneo ya manispaa ni jambo linalowahangaisha sana wenye mamlaka nchini Japani. Tatizo hilo limeendelea licha ya kuwa na walinzi wa mchana kwa kuwa watu hutupa takataka zao usiku. Sasa, wenye mamlaka wanatumia ushirikina kukabiliana na tatizo hilo kwa kujenga torii, yaani, malango mekundu ya mbao yaliyotengenezwa kama malango ya kuingia kwenye vihekalu vya Shinto. “Mbinu hiyo ni rahisi,” linasema gazeti IHT Asahi Shimbun. “Kwa kawaida, watu huona torii kuwa mahali patakatifu, hivyo kutupa takataka karibu na mahali hapo kunaweza kuleta bahati mbaya.” Kwa kweli, sasa watu hawatupi tena takataka karibu na torii hizo. “Lakini hatua chache tu kutoka hapo takataka zimerundamana,” linasema gazeti hilo.