Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Nyumba za Wamarekani wengi sasa zina televisheni nyingi kuliko watu wanaoishi humo, nusu ya nyumba hizo zina televisheni tatu au zaidi.”—ASSOCIATED PRESS, MAREKANI.

Kila siku katika mahakama za Afrika Kusini, watoto 82 wanafunguliwa mashtaka ya “kubaka au kuwashika-shika watoto wenzao sehemu za siri.” Kulingana na utafiti uliofanywa na mahakama fulani, wengi wa washtakiwa wanadai kwamba walifanya hivyo baadaya “kutazama vitendo hivyo kwenye televisheni.”—THE STAR, AFRIKA KUSINI.

Kutolala vya Kutosha Kunapunguza Uwezo wa Kufanya Kazi Vizuri

Mazoea ya kulala ya Wahispania fulani yanapunguza uwezo wao wa kufanya kazi vizuri. Dakt. Eduard Estivill ambaye ni msimamizi wa kliniki fulani inayoshughulikia mambo ya usingizi huko Barcelona, anasema kwamba wakilinganishwa na watu wengine katika Bara la Ulaya, Wahispania huamka mapema zaidi, wanafanya kazi saa nyingi zaidi, wanakula chakula usiku sana, na kwa wastani saa zao za kulala hupungua kwa dakika 40. Hata hivyo, kutolala vya kutosha kunaweza kumfanya mtu akasirike haraka, apoteze kumbukumbu, awe na wasiwasi, na ashuke moyo. Kwa hiyo, “mtaalamu yeyote ambaye hufanya kazi inayohitaji kutumia akili au utendaji mwingine unaohitaji mtu kuwa makini, anapaswa kulala kati ya saa saba na nane kila siku,” anaonya Dakt. Estivill.

Je, Ngano Itumiwe Kama Makaa?

Je, inafaa kutumia ngano kupasha nyumba joto? Gazeti la Ujerumani, Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung, linaeleza kwamba kwa kuwa bei ya nafaka inapungua na bei ya mafuta inapanda, ni rahisi zaidi kwa mkulima kuichoma ngano ili kupata joto badala ya kuiuza ili anunue mafuta. Mkulima anatumia senti 20 kuzalisha kilo 2.5 za ngano, lakini akiichoma itatoa kiasi cha joto kilicho sawa na kile ambacho kingetolewa na mafuta ya lita moja ambayo yanagharimu senti 60. Kwa hiyo wakulima wanakabili uamuzi huu mgumu ambao ulitajwa na gazeti hilo: Je, unaweza “kuchoma nafaka huku watu wengine wakifa njaa”?

Ziara ya Papa Yatumiwa Kufanya Biashara

Papa alipozuru Ujerumani mwaka wa 2006, watengeneza bidhaa, wachuuzi, na wanaofanya biashara ya utalii walijitayarisha vilivyo ili wafaidike na ziara yake. Kanisa pia lilichagua shirika fulani la kuwauzia bidhaa mbalimbali. Bidhaa zilizokuwa zikiuzwa zilitia ndani rosari, mishumaa, chupa za maji matakatifu, vikombe, kofia, fulana, vitu vya kushikilia funguo, na bendera za Vatikani. Gazeti Der Spiegel lilisema hivi: “Kanisa Katoliki limejihusisha sana kujitafutia pesa, kana kwamba Yesu Kristo . . . hakuwafukuza wafanyabiashara kutoka hekaluni.”

Michezo ya Video Yafanya Dhamiri Ife Ganzi

Wanasaikolojia watafiti wa Chuo Kikuu cha Iowa, Marekani, wanasema hivi: “Kucheza michezo ya jeuri kunaweza kufanya dhamiri ya mtu ife ganzi kuelekea jeuri.” Uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba kucheza michezo hiyo husababisha mtu “awe na chuki, hasira, huongeza mapigo ya moyo na matendo ya jeuri.” Uchunguzi huo ulipima mapigo ya moyo ya watu na jinsi walivyoitikia walipoonyeshwa sinema ya vitendo halisi vya jeuri baada ya kucheza michezo ya video inayoonyesha jeuri. Matokeo yalionyesha kwamba wale “waliocheza michezo ya video yenye jeuri wanazoea jeuri na mwishowe dhamiri zao hufa ganzi.”