Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ng’ombe Waendapo Likizo!

Ng’ombe Waendapo Likizo!

Ng’ombe Waendapo Likizo!

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA USWISI

JE, ULIPATA kujua kwamba maelfu ya ng’ombe katika Uswisi huenda likizo kila mwaka? Laiti ungejua jinsi wao huifurahia!

Wakati wa miezi ya baridi na barafu ya kipupwe ya Uswisi, ng’ombe wa maziwa huwekwa kwenye mazizi. Inaburudisha kama nini masika yafikapo na ng’ombe wanaweza kwenda nje na kulisha katika malisho ya majani. Kurukaruka kwao mara kwa mara hewani huonyesha shangwe yao ya badiliko la mandhari na majira.

Kufikia Mei au mapema mwezi wa Juni, mahali pa ziada pa malisho hupatikana wakati theluji inapoyeyuka na kutokeza malisho kwenye milima. Ni wakati wa ng’ombe kuwa katika kiangazi milimani.

Nchi Yenye Malisho Yaliyo na Maji Vizuri

Huko Uswisi kuna viwanja vya malisho karibu 10,000 kwenye milima, vyenye urefu wa kilometa za mraba 4,000 hivi. Hiyo yajumlika kuwa robo moja ya eneo la nchi hiyo. Kwa hiyo, utunzi mkubwa wahusika katika kulinda mali hiyo.

Mwanadamu na mnyama wanafanya kazi pamoja ili kuendeleza malisho hayo yabaki bila vichaka. Kwa madhumuni haya, wakulima huwapa wachungaji wa mifugo wa kulipwa ng’ombe wapatao 500,000. Ng’ombe wa maziwa, pamoja na ng’ombe ambao bado hawajazaa, husafirishwa kwa lori au garimoshi kwa ajili ya likizo ya kiangazi ya kulisha milimani.

Kwa kuwa barabara na reli hazifiki juu kabisa, sehemu ya mwisho ya safari lazima imalizwe kwa miguu. Kundi hilo la wanyama huendelea kupanda juu kiangazi kisongapo. Huko, nyakati nyingine kwenye malisho yapatayo meta 2,000 na 2,200 juu ya usawa wa bahari, ng’ombe hupata nyasi tamu aina ya alpine na maua yenye rangi mbalimbali. Chemichemi za mlimani ni nyingi, kwa hiyo hakuna shida ya maji ya kunywa.

Maziwa mazuri yanayotoka kwa ng’ombe hao nyakati nyingine husafirishwa kutoka mlimani kwa matumizi na utengenezaji wa bidhaa nyingine. Lakini mara nyingi hutengezwa kuwa siagi au jibini hukohuko mlimani. Siku za kiangazi zinapopungua, kundi hilo la wanyama huelekezwa kwenye malisho ya chini. Hatimaye siku inafika—ikitegemea hali ya hewa, kawaida huwa mwisho wa Septemba—ambapo mifugo hurudi kwenye makao yao ya majira ya kipupwe. Naam, likizo yao ya kiangazi inakaribia kumalizika! Lakini kwanza gwaride ya pekee hufanywa.

Siku Kuu!

Rekodi za uzalishaji zimewekwa, nao ng’ombe mashuhuri wanapambwa kulingana na kiwango cha maziwa walichotokeza. Yule aliyetoa maziwa mengi zaidi ndiye anayeongoza mifugo wenzake kwenye msafara huo kwenda nyumbani. Vichwa vya ng’ombe vinapambwa kwa maua ya karatasi yenye kupendeza, tepe, na matawi ya miti midogo ya misonobari. Wengi hubeba kengele ya chuma shingoni, wakitangaza kufika kwao tokea mbali.

Katika kipindi hiki cha pekee, wachungaji hao wa mifugo huvalia shati nyeupe na makoti meusi ya mahameli yaliyotiwa almaria. Wakati uleule, kule chini bondeni, idadi ya watu wenye mashamba wanakusanyika kandokando ya barabara kupokea msafara huo kwa makofi ya shangwe.

Wanapofika kwenye nyanda za chini, ng’ombe hao huelekezwa kwa wenyewe wakakae huko kwenye kipupwe kingine. Hata hivyo, hautakuwa muda mrefu kabla ya wakati mwingine wa likizo milimani! Ni maisha yenye kufurahisha kama nini!

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 18]