Ona video zinazopatikana

Ona habari zilizo ndani

KUUTAZAMA ULIMWENGU

KUUTAZAMA ULIMWENGU

Israel

Watu “waliozaliwa na kasoro ambazo zingeweza kugunduliwa mama alipokuwa mja-mzito” hawawezi tena kuwashtaki madaktari kwa sababu ya “kuwaruhusu wazaliwe,” inaripoti Tovuti ya Haaretz.com. Hata hivyo, wazazi wanaweza kuwashtaki madaktari ili walipwe “gharama za ziada za kumlea mtoto mlemavu na za kumtimizia mahitaji yake muda wote wa maisha yake.”

Australia

Nchini Australia, wenzi 8 kati ya 10 huishi pamoja kabla ya kufunga ndoa.

Ugiriki

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Ugiriki zilionyesha kwamba kulikuwa na ongezeko la asilimia 40 la visa vya kujiua katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka wa 2011, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa 2010. Ongezeko hilo lilitokea wakati uleule ambapo matatizo ya kiuchumi yalianza.

Marekani

Baraza la Kuhifadhi Mali za Asili la Marekani linasema kwamba asilimia 40 hivi ya chakula chote nchini humo hakitumiwi. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba asilimia 7 ya mazao yote hayavunwi, kwamba asilimia 17 ya vyakula vya mikahawani haviliwi, na kwamba familia hutupa asilimia 25 hivi ya vyakula wanavyonunua.

Madagaska

Kinyonga mdogo zaidi ulimwenguni aligunduliwa nchini Madagaska hivi karibuni. Kinyonga huyo mwenye rangi ya kahawia anaweza kufikia urefu wa milimita 29, na baadhi yao wanatoshana na ukucha wa mwanadamu. Kwa sababu ya kuharibiwa kwa mazingira anayoishi, mnyama huyo yuko katika hatari ya kutoweka.