Programu ya JW Library Inavyotumia Taarifa Zako
Ili uweze kutumia programu ya JW Library, taarifa fulani muhimu zinahitaji kupitishwa kutoka kwetu hadi kwenye kifaa chako na kutoka kwenye kifaa chako kuja kwetu. Taarifa hizo hazitauzwa kamwe au kutumiwa kibiashara. Programu hiyo pia inahifadhi taarifa kwenye kifaa chako ambazo zinakusanywa unapoitumia. Ili kufafanua hilo vizuri zaidi, ona mbinu tatu zifuatazo tunazotumia:
Taarifa Zinazotoka Kwenye Tovuti Yetu
JW Library hupakua taarifa kutoka kwenye tovuti ya jw.org. Taarifa hizo hutia ndani katalogi zenye orodha za rekodi na pia rekodi zenyewe. Kwa njia hii, unaweza kupata habari za karibuni zaidi kila wakati. Programu hii haitumii taarifa zozote kukuhusu au kuhusu kifaa chako inapopakua taarifa kutoka kwenye tovuti.
Kama tu inavyokuwa unapopakua kitu mtandaoni, tovuti yetu pia ina uwezo wa kupata anwani yako ya IP, programu ya Jw Library inapopakua habari kutoka kwenye jw.org. Anwani hiyo ya IP haitumiwi kumtambua mtu mmoja mmoja bali inatumiwa kulinda usalama wa programu hiyo na wa tovuti yetu pia. Habari zaidi kuhusu jinsi jw.org inavyotumia taarifa zinapatikana kwenye Sera ya Faragha ya tovuti hiyo.
Ikiwa unataka programu hiyo isipakue chochote kwenye jw.org, unaweza kuchagua mpangilio wa “nje ya mtandao.” Hata hivyo, kufanya hivyo kutapunguza sana uwezo wa programu hiyo.
Mapendezi Yako ya Kibinafsi na Taarifa
Programu ya JW Library inakuruhusu kubadili na kuhifadhi mapendezi yako ya kibinafsi na taarifa. Kwa mfano, unaweza kutia alama kwenye maandishi, kuandika maelezo yako, kutayarisha orodha ya video za kucheza, kuchagua Biblia utakayotumia, na kuweka machapisho kwenye sehemu ya vipendwa. Taarifa hizo zote zinahifadhiwa kwenye programu yako pekee, hazitumwi kwetu. Unaweza kuamua kuhifadhi taarifa hizo kwingineko ili uzipate tena iwapo zitapotea kwa sababu yoyote ile.
Programu hiyo pia inahifadhi baadhi ya mapendezi na mipangilio yako kwa kutegemea habari unazotafuta na mipangilio unayopendelea. Kwa mfano, inaweka kumbukumbu ya machapisho uliyotumia hivi karibuni, video, lugha, rangi uliyotumia kutia alama maandishi, maneno uliyotafuta, na ubora wa video uliochagua ulipotazama video mtandaoni. Mambo hayo yanaiwezesha programu hiyo kumpa mtumiaji huduma anazohitaji.
Uchanganuzi na Taarifa ya Utumiaji
Kwa kuongezea, programu hiyo inakupa fursa ya kututumia baadhi ya habari za uchanganuzi na taarifa za utumiaji. Taarifa hizo zinatusaidia kuboresha programu ili ifanye kazi vizuri. Hatuuzi kamwe taarifa hizo au kuzitumia kibiashara. Unaweza kuchagua ikiwa unataka tupokee habari hizo au la katika ukurasa wa mipangilio ulio katika programu hiyo.
Tunapopokea habari za uchanganuzi na taarifa za utumiaji, zinakuja na kitambulisho cha pekee cha kusakinisha. Kitambulisho hicho hakina uhusiano na kifaa chako, hata hatuna uwezo wa kutambua mtu binafsi aliyetuma habari hizo. Unaweza kuondoa kitambulisho hicho wakati wowote kwa kufuta programu na kisha kuipakua tena kwenye kifaa chako.

