Hamia kwenye habari

Mashahidi wa Yehova

Chagua lugha Kiswahili

Awamu ya 1 ya Picha za Ujenzi, Uingereza (Januari Hadi Agosti 2015)

Awamu ya 1 ya Picha za Ujenzi, Uingereza (Januari Hadi Agosti 2015)

Mashahidi wa Yehova wanahamisha ofisi yao ya tawi kutoka Mill Hill, London, kwenda eneo lililopo kilometa 70 hivi kuelekea mashariki, karibu na jiji la Chelmsford, Essex. Kati ya mwezi wa Januari na Agosti 2015, wajenzi waliandaa makazi ya muda ili kuwa tayari kuanza kazi ya kujenga.

Januari 23, 2015​—Eneo la ujenzi la ofisi ya tawi

Wakiwa na kibali kutoka kwenye mamlaka za eneo hilo, wafanyakazi walikata miti kwa ajili ya kuanza ujenzi. Walijitahidi kufanya hivyo kwa bidii ili wamalize mapema kabla kipindi cha ndege kutengeneza viota na kutaga mayai kuanza. Mabaki ya mbao yanatumika kutengenezea njia salama za wanaotembea kwa miguu, na mbao zinahifadhiwa kwa ajili ya kutumiwa katika ujenzi.

Januari 30, 2015​—Chumba cha muda cha kulia chakula

Fundi wa umeme akiweka soketi kwa ajili ya skrini za video kwenye jengo lililokuwa hoteli zamani. Sasa jengo hilo litatumiwa kupikia na kulia chakula. Skrini hizo zitatumiwa kutazama programu za kiroho kama vile ibada ya asubuhi na Funzo la Mnara wa Mlinzi la familia ya Betheli.

Februari 23, 2015​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Wafanyakazi wakizungushia ua eneo kubwa la ujenzi. Kwa kuwa eneo liko nje ya mji, hatua zinachukuliwa ili kuhakikisha kwamba ujenzi huo hauathiri sana wanyama wanaoishi eneo hilo. Kwa mfano, upande wa chini ya ua, nafasi yenye urefu wa sentimeta 20 imeachwa kuruhusu melesi wanaotafuta chakula usiku kuendelea na shughuli zao.

Februari 23, 2015​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Wafanyakazi wakijenga barabara ya muda inayounganisha eneo la makazi ya muda na eneo maalumu la ujenzi.

Machi 5, 2015​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Mwonekano wa barabara ya muda iliyokamilika, kutoka upande wa mashariki. Kama inavyoonekana upande wa juu kulia, barabara hiyo inatoka kwenye makazi ya muda hadi kwenye eneo maalumu la ujenzi. Majengo yanayoonekana upande wa chini kushoto sasa yanatumika kama nyumba za wajenzi. Mjengo ya makazi ya muda yatawekwa kwenye maeneo yaliyo karibu na majengo hayo.

Aprili 20, 2015​—Eneo la makazi ya muda

Mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova na mwakilishi mwingine wa makao makuu walikitembelea kikosi cha ujenzi. Baadaye katika juma hilo, mkutano wa pekee ulifanywa na Majumba yote ya Ufalme nchini Uingereza na Ireland yaliunganishwa kupitia intaneti kwa ajili ya programu hiyo. Ikatangazwa kuwa katika jioni iliyotangulia, Halmashauri ya Jiji la Chelmsford ilitoa kibali cha awali cha kuendelea na ujenzi.

Mei 13, 2015​—Eneo la kutegemeza ujenzi

Wafanya kazi wakiweka vifaa vya kuilinda mizizi katikati ya mialoni miwili. Njia hii inaunganisha eneo maalumu la makazi ya muda na eneo maalumu la ujenzi, hivyo vifaa hivyo vinaweza kusaidia kulinda mizizi isiharibiwe vyombo vizito vinapopita.

Mei 21, 2015​—Eneo la makazi ya muda

Wafanyakazi wakichimba mitaro kwa ajili ya kupitisha mabomba na nyaya za makazi ya muda. Nyuma kuna majengo 50 yaliyokamilika watakayokuwa wakiishi wafanyakazi katika kipindi cha ujenzi.

Juni 16, 2015​— Eneo la makazi ya muda

Fundi wa mabomba akiweka mabomba ya maji kwenye majengo ya makazi ya muda.

Juni 16, 2015​—Eneo la makazi ya muda

Mwonekano wa nyumba za muda kutoka upande wa mashariki. Mbele ni maeneo yanayoandaliwa kwa ajili ya kuweka nyumba zaidi. Upande wa kushoto kuna majengo mengine yanayotia ndani chumba cha kulia chakula. Ofisi ya tawi itajengwa katika eneo linaloonekana katikati ya picha kwa nyuma.

Juni 16, 2015​—Eneo la makazi ya muda

Mtaalamu akiunganisha nyaya katika chumba cha vyombo vya mawasiliano. Mfumo wa kompyuta na Intaneti ilihitajika mapema katika mradi huo ili kushughulikia shughuli zote za ujenzi, kuwasiliana na ofisi za tawi nyingine, na kuwasiliana na makao makuu ya ulimwenguni pote.

Julai 6, 2015​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Mwanakandarasi akipima maeneo yenye mashimo ya kufanyia uchunguzi kwa kutumia kifaa cha kupokea habari kutoka kwenye setilaiti (GPS). Mashimo hayo yanawasaidia wanaakiolojia kutathmini eneo kabla ya ujenzi kuanza. Ingawa Waroma waliishi eneo la karibu la Chelmsford, katika mashimo 107 yaliyochimbwa kwenye awamu ya kwanza ya tathmini hizo hakuna vitu vyenye thamani vya kale vilivyovumbuliwa.

Julai 6, 2015​—Eneo la kutegemeza ujenzi

Mfanyakazi akikata fremu ya mlango katika urefu unaofaa. Baadhi ya majengo katika eneo la kutegemeza ujenzi yalirekebishwa ili yawe karakana. Ofisi za muda na utendaji mwingine wa kutegemeza kazi utapatikana hapo.

Julai 6, 2015​—Eneo maalumu la makazi ya muda

Mfanya kazi akijaza udongo kwenye lori ili kujaza maeneo yaliyo na mashimo.

Julai 7, 2015​—Eneo la ujenzi la ofisi ya tawi

Mandhari kutoka upande wa kusini wa eneo la ujenzi lenye ekari 34 inayoonyesha mashamba ya jirani. Barabara kuu iliyo jirani (haijaonyeshwa) inafika kwenye bandari, viwanja vya ndege, na kwenye jiji la London.

Julai 23, 2015​—Eneo la ujenzi la ofisi ya tawi

Wanakandarasi wakibomoa majengo yaliyokuwapo kwenye eneo linalotarajiwa kujengwa ofisi ya tawi mpya.

Agosti 20, 2015​—Eneo la kutegemeza ujenzi

Kreni yenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 60 ikiweka sehemu ya chini ya kibanda kwenye mahali pake. Sehemu ya mbele ya picha, inaonyesha misingi kwa ajili ya kuweka vibanda vingine. Vibanda hivi ni kwa ajili ya ofisi za kuratibu mradi wa ujenzi.