Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Makao Makuu ya Mashahidi Kuhamishwa

Makao Makuu ya Mashahidi Kuhamishwa

Mnamo Julai 2009, Mashahidi wa Yehova walinunua kiwanja kaskazini mwa New York wakiwa na lengo la kuhamisha makao yao makuu. Kiwanja hicho chenye ukubwa wa ekari 253 kiko kilomita 80 (maili 50) hivi kaskazini magharibi mwa makao makuu ya sasa yaliyo Brooklyn, New York, ambayo yamekuwa yakitumika tangu mwaka wa 1909.

Mashahidi wapatao 800 wataishi na kufanya kazi katika makao hayo mapya, yatakayotia ndani jengo la ofisi mbalimbali, jengo la huduma mbalimbali, na majengo manne ya makazi. Pia kutakuwa na chumba cha makumbusho chenye historia ya Mashahidi wa Yehova wa leo.

Majengo hayo yatajengwa kwenye eneo la ekari 45 za kiwanja hicho kilichonunuliwa, na kuacha msitu unaozunguka na maeneo yenye maji kama yalivyo. Bustani haitakuwa na maeneo makubwa yenye nyasi. Badala yake, mazingira ya asili ya eneo hilo yatadumishwa.

Wasanifu-majengo wamechora ramani za majengo yatakayohifadhi nishati na kupunguza gharama, na hivyo, kuepuka kuharibu mazingira isivyo lazima. Kwa mfano, juu ya paa za majengo kutakuwa na uoto mbalimbali ili kupunguza kuchuruzika kwa maji ya mvua na vilevile kusawazisha joto ndani ya majengo hayo. Ofisi zitajengwa kwa njia ambayo mwanga wa asili unaweza kutumika kwa kiasi kikubwa. Uhifadhi wa maji pia utazingatiwa.

Sababu ya kuhama ni nini? Ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova katika sehemu nyinginezo ulimwenguni sasa zinashiriki katika kazi ya kuchapisha Biblia na machapisho mengine yanayozungumzia Biblia, kazi ambayo awali ilikuwa ikifanywa Brooklyn peke yake. Mnamo 2004, kazi ya kuchapisha na kusafirisha nchini Marekani ilihamishiwa Wallkill, New York, kilomita 145 hivi (maili 90) kaskazini-magharibi mwa Brooklyn.

Sababu nyingine ni gharama. Kuendesha na kudumisha majengo yaliyo Brooklyn ni gharama kubwa. Kuhamia mahali pamoja kutapunguza gharama na hivyo kutegemeza kazi ya elimu ya Biblia vizuri zaidi.

Uchanganuzi wa mazingira unahitajika kabla ya vibali vya mwisho kutolewa. Mambo yakiwa shwari, ujenzi utaanza 2013 na kukamilika baada ya miaka minne.

Mbali na kiwanda cha uchapishaji kilicho Wallkill, New York, Mashahidi wa Yehova wana kituo cha elimu kilicho Patterson, New York. Pia tuna ofisi za tawi katika nchi nyingi. Ulimwenguni pote kuna Mashahidi zaidi ya milioni saba na nusu.