Mashahidi wa Yehova nchini Uingereza wameanza kujenga ofisi yao mpya ya tawi karibu na Chelmsford, katika mkoa wa Essex. Eneo hilo maridadi lina jamii kadhaa za wanyama-mwitu ambao wamelindwa nchini Uingereza chini ya Sheria ya Wanyama-mwitu na Maeneo ya Vijijini ya 1981. Mashahidi wa Yehova wanafanya nini wakati wa ujenzi ili kutenda kupatana na Sheria hiyo na kuwalinda wanyama hao?

Kujenga daraja la panya aina ya dormouse

Mashahidi walitumia mbao kutoka kwenye miti ya eneo hilo kutengeneza visanduku vidogo kwa ajili ya kuwaelekeza panya aina hazel dormice wasifike kwenye eneo la ujenzi. Pia walijenga daraja la pekee kwa ajili ya panya hao linalopita juu ya mwingilio mpya wa ofisi ya tawi ili kuhakikisha kwamba panya hao wanaweza kuvuka barabara bila kutenganishwa na miti na vichaka walivyozoea. Isitoshe, Mashahidi wana ratiba ya kudumisha visehemu mbalimbali vilivyotenganishwa kwa uzio wa vichaka ili kumnufaisha panya huyo. Wakati wa msimu wa baridi kali panya hao wanapolala, sehemu moja itakuwa ikikatwa kisha msimu unaofuata sehemu nyingine ishughulikiwe. Udumishaji huo unamfanya panya huyo asiathiriwe sana, unalinda mazingira yao na kuhakikisha kwamba nyakati zote wana chakula cha kutosha.

Kutundika visanduku kwa ajili ya panya aina ya dormouse

Mashahidi pia wanalinda mazingira ya nyoka na aina mbalimbali za mijusi. Wataalamu wa elimu ya uhusiano wa wanyama na mazingira waliwakusanya chini ya vigae vilivyowekwa sehemu fulani kwa muda kisha wakawahamisha hadi kwenye eneo salama mbali na eneo la ujenzi. Eneo hilo jipya kwa ajili ya nyoka na mijusi lina maeneo ya kujificha wakati wa majira ya baridi kali na uzio wa pekee wa kuwatenga na watu. Mashahidi hukagua uzio huo kwa ukawaida ili kuhakikisha wanyama hao hawarudi tena kwenye maeneo ya ujenzi ili wasiumie.

Hazel dormouse

Ili kuepuka kuvuruga utendaji wa popo, eneo la ujenzi linatumia taa ya aina ya pekee inayodhibiti kuenea kwa mwanga. Taa hizo zinamulika tu zinapotambua gari linakaribia, na hivyo kudumisha giza kwa kadiri iwezekanavyo kwa ajili ya popo. Kwa kuwa popo hutafuta chakula katika visehemu hivyo vyenye uzio wa vichaka katika eneo la ujenzi, visehemu vingi vitadumishwa na vichaka vingine vitapandwa vyenye urefu wa kilomita mbili na nusu. Kwa kuwa lazima miti fulani ikatwe katika eneo la ujenzi, wafanyakazi walitundika visanduku vya aina fulani kwa ajili ya popo wowote wanaopoteza makao yao.

Kutundika visanduku kwa ajili ya popo

Mashahidi wanajitahidi kuhifadhi miti kadhaa muhimu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu sana, kwa kuhakikisha kwamba magari na watu hawapiti karibu na eneo ambapo mizizi ya miti hiyo inamea. Miti hiyo ni makao ya wadudu wengi, popo, na ndege. Katika njia hizi zote, Mashahidi wameazimia kuendelea kulinda wanyama-mwitu katika eneo la Chelmsford.