Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Jumba Jipya la Kusanyiko Katikati ya Msitu wa Amazon

Katikati ya msitu mkubwa wa Amazon Jumba la Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova maridadi limesimamishwa. Sehemu kubwa ya eneo hilo la ekari 128, lililo kaskazini mwa jiji la Manaus, Brazili, ni msitu. Aina ya ndege kama vile kasuku, tokani, na ndege wengine wenye rangi za kupendeza, wanalia kwa sauti kwenye miti mbalimbali yenye kupendeza. Kwa nini Jumba la Kusanyiko lijengwe mahali kama hapa?

Jiji la Manaus—lililo kilomita 1,450 kutoka kwenye mlango wa Mto Amazon—lina karibu watu milioni mbili. Jumba hilo jipya litatumiwa na Mashahidi 7,000 hivi kutoka Manaus na miji iliyo karibu, kutia ndani vijiji vilivyo karibu na Mto Amazon na vijito vyake. Mji ulio mbali zaidi, São Gabriel da Cachoeira, upo zaidi ya kilomita 800 magharibi mwa Manaus. Ili kuhudhuria kusanyiko kwenye Jumba la Kusanyiko, baadhi ya Mashahidi husafiri kwa mashua kwa siku tatu!

Ilikuwa kazi kubwa kujenga Jumba la Kusanyiko katikati ya eneo la Amazon. Ilitia ndani kusafirisha kontena 13 hivi zenye vifaa vya ujenzi kutoka katika bandari iliyoko jiji la Santos, São Paulo; kuzisafirisha kwenye pwani ya Brazili; kisha kusafiri dhidi ya mkondo wa Mto Amazon ili kufika kwenye eneo la ujenzi.

Jumba hilo jipya ni Jumba la Kusanyiko la 27 kujengwa nchini Brazili, na watu 1,956 walihudhuria programu ya kuliweka wakfu iliyofanywa Jumapili, Mei 4, 2014. Wengi walisisimka kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kwao kuhudhuria mkutano katika Jumba la Kusanyiko.

Wasikilizaji waliweza kumsikia na kumwona msemaji. Hilo lilikuwa tofauti na zamani, wakati ambapo makusanyiko yalifanyiwa katika maeneo ya umma na wengi hawangeweza kuona jukwaa wala msemaji. Shahidi mmoja alisema, “Nimehudhuria makusanyiko kwa miaka mingi, lakini sikuwahi kufaulu kutazama drama ya Biblia; niliisikiliza tu.” Sasa kila mtu anaweza kuona jukwaa.