Hamia kwenye habari

Kutokeza Video Katika Mamia ya Lugha

Mashahidi wa Yehova wanajulikana sana kwa kazi yao ya kutafsiri. Kufikia Novemba 2014, tulikuwa tumetafsiri Biblia katika lugha 125 na machapisho yanayotegemea Biblia katika lugha 742. Kazi yetu ya kutafsiri inatia ndani pia video. Kufikia Januari 2015, video Ni Nini Hutendeka Katika Jumba la Ufalme? ilikuwa inapatikana katika lugha 398, na video Kwa Nini Ujifunze Biblia? katika lugha 569. Kwa nini tulifanya kazi hiyo, na ilitimizwaje?

Katika Machi 2014, Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova liliagiza ofisi za tawi ulimwenguni pote zirekodi sauti kwa ajili ya video katika lugha nyingi iwezekanavyo ili kuwachochea watu wajifunze Biblia.

Kutafsiri video kunachukua hatua kadhaa. Kwanza, kikundi cha watafsiri wenyeji hutafsiri hati ya video. Kisha, wenyeji wanachaguliwa kwa ajili ya kila sauti katika video. Halafu, mafundi wa mitambo hurekodi sauti katika lugha iliyotafsiriwa, wanahariri rekodi hizo, na kuingiza maandishi yanayoonekana kwenye video. Mwishowe, sauti, maandishi, na video huunganishwa ili kutokeza faili iliyokamilika ambayo inaweza kupakiwa kwenye Tovuti.

Baadhi ya ofisi za tawi zina studio za kurekodi na watu waliozoezwa kufanya kazi hiyo. Namna gani lugha zinazozungumzwa na kutafsiriwa katika maeneo ya mbali?

Ulimwenguni pote, mafundi wa mitambo walisafiri kwenda sehemu za mbali wakiwa na mifumo ya kurekodia inayoweza kubebeka. Kwa kutumia maikrofoni na kompyuta ndogo iliyo na programu ya kurekodi, walisimamisha studio ya muda ya kurekodi ndani ya ofisi, Jumba la Ufalme, au hata ndani ya nyumba ya mtu binafsi. Watu waliozungumza lugha inayorekodiwa walitumiwa kuwa wasomaji, wasimamizi, na wasahihishaji. Kazi ya kurekodi ilipokwisha na rekodi ikaidhinishwa, fundi wa mitambo angechukua vifaa vyake na kuhamia eneo lingine.

Kwa njia hii, video zilitokezwa katika lugha zaidi ya mara tatu ya zile zilizokuwa zikitokezwa hapo awali.

Itikio limekuwa la kupendeza sana. Video zetu ndizo video za kwanza ambazo watu wengi wametazama katika lugha yao.

Pitjantjatjara ni moja ya lugha zilizorekodiwa, inayozungumzwa na zaidi ya watu 2,500 nchini Australia. Lugha hiyo ilirekodiwa katika Alice Springs, Eneo la Kaskazini. Callan Thomas, aliyesaidia kutokeza rekodi hizo, anasema hivi: “Video hizo zilipokelewa vizuri sana. Wenyeji walikaza macho yao kwenye kompyuta ndogo na kuuliza tena na tena wangepata wapi video zaidi kama hizo. Machapisho yanayopatikana katika lugha hiyo ni machache sana. Lakini wanapoisikia lugha hiyo​—na hasa wanapoitazama​—wanashangaa sana.”

Mashahidi wawili nchini Kamerun walikuwa wakisafiri ndani ya mtumbwi kwenye mto. Walitua kwenye kijiji kimoja cha Mbilikimo na kuzungumza na chifu, ambaye alikuwa mwalimu kwenye shule moja katika eneo hilo. Baada ya kujua kwamba chifu huyo alizungumza lugha ya Bassa, ndugu hao walitumia kompyuta ndogo kumwonyesha video Kwa Nini Ujifunze Biblia? katika lugha yake. Chifu huyo alifurahi sana na akaomba machapisho.

Katika kijiji kimoja nchini Indonesia, kiongozi wa kidini katika eneo hilo aliwapinga Mashahidi wa Yehova, na alichoma machapisho yote ambayo Mashahidi walikuwa wamegawanya katika eneo hilo. Wengine katika eneo hilo walitishia kuteketeza Jumba la Ufalme. Baadaye, polisi wanne walienda kwenye nyumba ya Shahidi mmoja na kumhoji yeye na familia yake. Walitaka kujua nini hutendeka ndani ya Jumba la Ufalme, hivyo akawaonyesha video Ni Nini Hutendeka Katika Jumba la Ufalme? katika Kiindonesia.

Baada ya kuitazama, polisi mmoja alisema hivi: “Sasa nimeona kwamba watu hawawaelewi wala hawawafahamu kikweli.” Polisi mwingine aliuliza hivi: “Ninaweza kupata video hii ili niwaonyeshe wengine? Video hii inatoa habari sahihi kuwahusu.” Sasa polisi wana maoni yanayofaa kuwahusu Mashahidi na wanaandaa ulinzi kwa ajili yao.

Ikiwa hujatazama video hizi, kwa nini usizitazame katika lugha yako mwenyewe?