Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Kutangaza JW.ORG Katika Maonyesho ya Vitabu ya Toronto

Novemba 13 hadi 16, 2014, Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu yalifanywa katika Ukumbi wa Metro jijini Toronto. Zaidi ya watu 20,000 walihudhuria maonyesho hayo ya siku nne, ambayo yalikuwa na vitabu vilivyochapishwa na vya kielektroni.

Mashahidi wa Yehova walisimamisha kibanda chenye kuvutia sana. Katika kibanda hicho kilichokuwa na kompyuta ndogo za mkononi (tablet) watu walionyeshwa jinsi ya kutumia jw.org.

Msimamizi mmoja alisema hivi: “Tovuti yenu ni ya kisasa sana. Nafikiri mashirika mengine yanapaswa kujifunza kutoka kwenu.” Wageni walisema kwamba tovuti hiyo imepangwa kitaalamu na ni rahisi kuitumia na ina majibu ya maswali muhimu. Pia walivutiwa kuona kwamba tovuti hiyo inaweza kuwasaidia watu kukabiliana na matatizo yao.

Mashahidi waliokuwa wakishughulikia kibanda hicho walipozungumza na watu waliopitia hapo waligundua kwamba wengi wao hawakuwa wamewahi kusikia kuhusu tovuti ya jw.org kabla ya hapo. Wageni wote walichukua kadi ya mawasiliano au trakti yenye kichwa Tutapata Wapi Majibu ya Maswali Muhimu Maishani? Wengi wao walisema kwamba watatembelea tovuti hiyo tena na baadhi yao wakaomba Mashahidi wa Yehova wawatembelee nyumbani.

Ijumaa ilikuwa “Siku ya Watoto” na hivyo video za vibonzo kwenye ubao zilionyeshwa kutoka kwenye jw.org. Watoto wa shule na walimu wao walisimama kwenye kibanda hicho ili kutazama video hizo.

Mwanamume fulani kutoka Chicago anayefanya kazi katika kampuni inayochapisha Biblia alishukuru kwa ubora wa Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya iliyokuwepo kwenye kibanda hicho. Alitaka kuwasiliana na wachapishaji wa Biblia hiyo, hivyo akapewa kadi ya mawasiliano.

Tovuti hiyo ina lugha zaidi ya 700, lakini wageni walitazama tovuti hiyo katika lugha 16—Kiamhara, Kibengali, Kichina, Kifaransa, Kigiriki, Kigujarati, Kihindi, Kihispania, Kiingereza, Kikorea, Kireno, Kiswedi, Kitamili, Kitigrinya, Kiurdu, na Kivietnam.

Shahidi mmoja aliyewakaribisha watu kwenye kibanda hicho alisema kwamba kuna tofauti kubwa kati ya kuwaambia watu kuhusu tovuti yetu na kuwaonyesha tovuti hiyo. Alisema, “Hiyo ilikuwa nafasi nzuri sana kwetu kuwaonyesha watu tovuti hiyo.”