Hamia kwenye habari

Hamia kwenye menyu ya pili

Mashahidi wa Yehova

Kiswahili

Wakati wa Kuondoka Hoteli ya Bossert

Wakati wa Kuondoka Hoteli ya Bossert

Katika mwezi wa Novemba 2012, Mashahidi wa Yehova waliuza hoteli ya Bossert. Funguo za jengo hilo zilikabidhiwa mmiliki mpya, na kama ilivyokuwa kwa wageni wengi, Mashahidi waliondoka kwenye hoteli hiyo. Pesa zilizopatikana baada ya uuzaji huo zitatumika kuendeleza kazi ya ulimwenguni pote ya elimu ya Biblia inayofanywa na Mashahidi wa Yehova.

Mashahidi waliuza jengo hilo lenye orofa 14 lililojengwa kwa mtindo wa ujenzi uliotumika huko Italia kati ya karne ya 14 na 16 kwa sababu watahamisha makao yao makuu kutoka Brooklyn, New York, hadi kwenye majengo mapya yatakayojengwa huko Warwick, New York. Mpango huo wa kuhama unatazamiwa kuchukua miaka kadhaa.

Historia ya Miaka Mia Moja

Louis Bossert, mfanyabiashara wa mbao wa New York, alijenga Hotel Bossert katika mwaka wa 1909. Ilikusudiwa kuwa na vyumba vya hoteli na vyumba vya kupanga kwa ajili ya wageni wa muda na wakaaji wa kudumu. Kwa kuwa hoteli hiyo ilijaa haraka, katika mwaka wa 1914 mfanyabiashara huyo alijenga jengo la ziada lililokuwa na ukubwa karibu mara mbili wa jengo la awali. Mkahawa uliokuwa darini ulioitwa Marine Roof uliongezwa katika mwaka wa 1916.

Katika miaka ya 1980, Mashahidi wa Yehova walinunua jengo hilo na kulikarabati ili liwe makao ya Mashahidi waliofanya kazi katika makao yao makuu. Mafundi walibadili vyumba vya kuchezea dansi kuwa vyumba vya kulia chakula na mkahawa uliokuwa darini kuwa sebule ya kupumzikia kwa wakazi na wageni wao.

Tangu mwaka wa 2010, jengo hilo limepokea Mashahidi wa Yehova kutoka ulimwenguni pote ambao walikuja kutembelea makao makuu.

Mmiliki mpya anapanga kulikarabati jengo hilo na kulifanya kuwa hoteli. Kazi ya kubadili Bossert kutoka kuwa jengo la makazi ya chumba kimoja au viwili na kuwa hoteli ya kifahari haitakuwa ngumu kwa sababu jengo hilo lilitunzwa vizuri sana.

Kurudisha Fahari Yake

Kabla ya Mashahidi kuhamia Bossert, jengo hilo lilikuwa limeachwa likachakaa kwa miaka mingi. Kuta zake nyeupe za nje zilikuwa chafu, utepe wenye nakshi uliotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi uliozungushwa kwenye paa la jengo ulikuwa umevunjika na kulegea. Madirisha yalikuwa yamezeeka na kulegea. Ni njiwa tu waliokuwa wakiishi kwenye dari la mkahawa wa Marine roof. Kwa hiyo, mradi mkubwa wa ukarabati ukaanza. Mashahidi wa Yehova kutoka maeneo mbalimbali ya Marekani walitumia wakati na stadi zao wakijitolea katika mradi huo, ambao ulikamilika mwaka wa 1991.

Wakati wa ukarabati, Mashahidi walisafisha na kurekebisha mawe ya chokaa na matale yaliyo upande wa nje wa jengo. Waliondoa ule utepe wenye nakshi uliofinyangwa kwa udongo na kuweka mwingine unaofanana kabisa na huo uliotengenezwa kwa nyuzinyuzi za kioo. Waliweka madirisha mapya ya mkangazi.

Pia walikarabati sehemu ya ndani ya jengo, wakikazia uangalifu ukumbi ambao hapo zamani ulikuwa maridadi sana. Ili kurekebisha kuta za marumaru zilizoharibika, walileta mawe kutoka kwenye machimbo yake ya asili yaliyo nchini Italia. Pia wafanyakazi walirekebisha mapambo ya darini yaliyotengenezwa kwa ustadi kwa kutumia plasta ambayo yalikuwa yameharibiwa na maji.

Ilikuwa kazi ngumu sana kukarabati nguzo kubwa za chuma zilizo ukumbini. Awali nguzo hizo zilinakshiwa kwa scagliola, mbinu ya Italia ya kupiga plasta ambayo ilifanana kabisa na marumaru. Hata hivyo, nguzo hizo zilikuwa zimepakwa rangi mara nyingi na wamiliki waliotangulia. Hakuna mfanyakazi yeyote kati ya waliojitolea kurekebisha jengo hilo aliyejua mbinu ya kutumia scagliola. Maktaba ya chuo kikuu kilicho jirani ilikuwa na kitabu kilichokuwa na mwongozo wa jinsi ya kufanyiza marumaru hiyo bandia. Kwa msaada wa kitabu hicho, wafanyakazi hao walitumia majuma kadhaa kurudisha nakshi kwenye nguzo hizo mpaka zikakaribia kabisa kufanana na zilivyokuwa hapo awali.

Kazi ya kukarabati ilipokamilika katika mwaka wa 1991, jengo hilo lilikuwa maridadi na linaloweza kutumiwa. Kwa kutambua jitihada iliyofanywa, Bossert ilitunukiwa tuzo la Lucy G. Moses kwa kazi kubwa iliyofanywa ya kuhifadhi jengo hilo katika mtindo wake wa kale.