Kiswahili
Samweli​—Mvulana Aliyetangaza Ujumbe wa Yehova kwa Ujasiri
https://cms-imgp.jw-cdn.org/img/p/1102025921/univ/art/1102025921_univ_sqr_xl.jpg
wcg sura 21

21 SAMWELI

Mvulana Aliyetangaza Ujumbe wa Yehova kwa Ujasiri

Mvulana Aliyetangaza Ujumbe wa Yehova kwa Ujasiri

MAISHA ya Samweli, binti ya Yeftha, na Samsoni yalifanana katika njia fulani. Katika njia ipi? Mambo ambayo wazazi wao walifanya yaliathiri maisha yao kwa njia kubwa. Kama binti ya Yeftha, Samweli pia alikabidhiwa kwa Yehova ili amtumikie kwa njia ya pekee maisha yake yote. (1 Sam. 2:11) Kama Samsoni, Samweli alikuwa Mnadhiri maisha yake yote. (Amu. 13:7) Naye Samweli alihitaji kuwa jasiri, kama tu binti ya Yeftha na Samsoni.

Samweli alipoachishwa kunyonya, huenda akiwa na umri wa miaka mitatu hivi au zaidi, Hana mama yake, alimpeleka akamtumikie Yehova kwenye hema la mkutano lililokuwa Shilo, kama tu mama yake alivyokuwa amemwahidi Yehova. Lakini aliendelea kumtembelea mwana wake, na kila mwaka alimpelekea joho jipya. Samweli alilelewa huko chini ya utunzaji wa kuhani mkuu Eli aliyekuwa na umri mkubwa. Huenda baadhi ya wanawake waliokuwa kwenye hema la mkutano walisaidia kumtunza mvulana huyo.

Hata hivyo, ibada kwenye hema la mkutano ilikuwa ikichafuliwa, na Eli alikuwa na hatia kwa kadiri fulani. Watoto wake wawili, Hofni na Finehasi, walikuwa waovu. Walifanya uasherati na baadhi ya wanawake waliotumikia katika hema takatifu la Yehova. Mbali na hilo, walichafua ibada safi katika njia nyingine. Inaonekana kwamba watu walipoleta dhabihu kwenye hema la mkutano, Hofni na Finehasi waliwaamuru watumishi wa makuhani wawape sehemu bora za dhabihu kabla hazijatolewa kwa Yehova. Eli alijua mambo ambayo watoto wake walikuwa wakifanya. Hata hivyo, aliwaonya kwa upole tu, nao walimpuuza. Licha ya kwamba Samweli alizungukwa na uovu wote huo, aliendelea kukua na kupendwa na Mungu na wanadamu. Wakati wa Yehova wa kurekebisha matatizo huko Shilo ulipofika, alimchagua kijana Samweli kuwa msemaji wake.

Usiku mmoja, Samweli aliamka aliposikia sauti ikimwita. Samweli alifikiri kwamba Eli, ambaye alikuwa mzee na kipofu, ndiye aliyekuwa akimwita. Kwa hiyo, alikimbia na kumuuliza kuhani huyo mkuu alichotaka. Hata hivyo, Eli akamwambia arudi akalale kwa kuwa hakuwa amemwita. Jambo hilo lilitokea mara ya pili na ya tatu. Hapo ndipo Eli alipotambua kilichokuwa kikiendelea. Yehova ndiye aliyekuwa akimwita Samweli! Kwa hiyo, akamwambia Samweli arudi akalale, na ikiwa Yehova atamwita tena, Samweli aseme: “Sema, Yehova, kwa maana mtumishi wako anasikiliza.” Samweli akatii.

Yehova alimwita Samweli kwa mara ya nne: “Samweli, Samweli!” Mvulana huyo akajibu: “Sema, kwa maana mtumishi wako anasikiliza.” Kisha Yehova akazungumza naye. Alimwambia kwamba atarekebisha matatizo yaliyokuwepo huko Shilo na kwamba Eli angehukumiwa kwa kukosa kuwaadhibu wanawe. Nyumba yake yote ingeadhibiwa, kutia ndani wana hao wawili waovu. Samweli alipaswa kumwambia Eli mambo yote hayo!

Samweli akarudi kitandani. Asubuhi ilipofika akaenda kufungua milango ya ua wa hema la mkutano. Inaeleweka kwa nini ‘Samweli aliogopa kumwambia Eli maono hayo.’ Eli alimwita mvulana huyo na kumuuliza Mungu alikuwa amemwambia nini. Huenda alitambua kwamba Samweli alikuwa akiogopa, kwa hiyo akamwambia: “Tafadhali, usinifiche.”

Ingawa Samweli alikuwa mvulana tu, alipaswa kumtangazia Kuhani Mkuu Eli ujumbe wa Yehova wa hukumu

Bila shaka, lazima iwe ilikuwa vigumu kwa Samweli kuanza kuzungumza. Kwa nini? Huenda alimheshimu Eli kama tu ambavyo angemheshimu babu yake. Isitoshe, kwa kuwa Eli alikuwa kuhani mkuu, alistahili kuheshimiwa kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kiroho wa taifa la Israeli! Licha ya hayo, mvulana huyo alizungumza kwa ujasiri. Biblia inasema, “Samweli akamwambia kila jambo.” Kwa hiyo, Eli akagundua kwamba hivi karibuni angepatwa na msiba. Je, angewarekebisha wanawe waovu? Hakuna jambo lolote linalotuonyesha kwamba alifanya hivyo.

Yehova alimbariki sana Samweli kwa kuonyesha ujasiri. Tunasoma hivi: “Yehova mwenyewe alikuwa pamoja naye.” Mbali na hilo, Mungu alianza kumtumia kuwa msemaji wake, na Yehova ‘hakuruhusu neno lolote kati ya maneno yote ya Samweli likose kutimia.’ Maneno yote ambayo Samweli alisema kumhusu Eli na wanawe yalitimia. Katika kipindi hicho chote, Yehova aliendelea kumtumia Samweli kuwapa Waisraeli mwongozo wa kiroho. Kwa miaka mingi, Samweli alimtumikia Yehova kwa ushikamanifu akiwa nabii na mwamuzi wake. Alikuwa amejifunza kuonyesha ujasiri alipokuwa mtoto, na hadi alipozeeka aliendelea kumtumikia Yehova kwa ujasiri na kwa uaminifu.

Soma simulizi hili katika Biblia:

Jambo la kuzungumzia:

Samweli alionyesha ujasiri katika njia zipi?

Chimba Zaidi

  1. 1. Fafanua eneo la Shilo lilikuwaje, ambako hema la Yehova lilipatikana. (w92 11/1 8-9) A

    Todd Bolen/​BiblePlaces.com

    Picha A: Eneo la Shilo la kale

  2. 2. Samweli aliishi maisha ya aina gani kwenye hema la mkutano? (ia 60-62 ¶9-13) B

    Picha B

  3. 3. Ni katika maana gani “Samweli alikuwa bado hajamjua Yehova”? (1 Sam. 3:7; w02 12/15 8 ¶5-6)

  4. 4. Unabii kuhusu familia ya Eli ulitimiaje? (it “Eli, 1” ¶5–7)

Tafakari Masomo Tunayojifunza

  • Kijana anaweza kujifunza nini kutoka kwa Samweli kuhusu umuhimu wa . . .

  • Ni wakati gani ambapo kijana anahitaji kuzungumza kwa ujasiri, na mfano wa Samweli unaweza kumsaidiaje?

  • Unaweza kuiga ujasiri wa Samweli katika njia zipi nyingine?

Tafakari Kumhusu Yehova na Kusudi Lake

  • Simulizi hili linanifundisha nini kumhusu Yehova?

  • Simulizi hili linahusianaje na kusudi la Mungu kwa wanadamu?

  • Ningependa kumuuliza Samweli maswali gani atakapofufuliwa?

Jifunze Mengi Zaidi

Huenda ni wakati gani ambapo vijana na watu wazima wakahitaji kuwa jasiri ili kutetea kilicho sawa?

Jifunze Kutoka Kwao—Samweli (4:53)

Hata watu waliomzunguka walipomchukiza Mungu, kijana Samweli alifanya uamuzi unaofaa.

“Samweli Achagua Kumtumikia Yehova” (ijwis makala ya 15)