25 DAUDI
Daudi—Ujasiri Unaoongozwa na Dhamiri
DAUDI alikuwa akimkimbia Mfalme Sauli. Kwa kushangaza, pindi moja Sauli alimpenda na kumwamini sana Daudi. Wakati huo Daudi alimbebea Sauli silaha zake na alikuwa kiongozi wa jeshi lake. Hata hivyo, sasa Sauli alikuwa akijaribu kumuua Daudi. Ingawa Mungu alikuwa amemwahidi Daudi kwamba atakuwa mfalme, sasa alikuwa akijificha nyikani ili kujilinda pamoja na wanaume wake 600.
Sauli alikuwa amebadilika na kuwa mfalme mwovu. Alikuwa ameruhusu wivu umwongoze kutenda mambo maovu, na hata mara kadhaa alijaribu kumuua Daudi. Pindi fulani Daudi alipata fursa ya kumuua Sauli, lakini hakufanya hivyo. Hata hivyo, bado Sauli aliendelea kumwinda. Kwa hiyo, Daudi alienda kujificha karibu na jiji linaloitwa Zifu, lakini watu wa jiji hilo wakamsaliti Daudi. Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa watu wa jiji hilo kumsaliti. Kwa hiyo, Sauli akaenda kumtafuta Daudi.
Daudi angefanya nini? Kwanza, aliwatuma baadhi ya wanaume wake wakapeleleze Sauli alikuwa wapi. Hata ingawa jeshi la Sauli lilikuwa na wanaume 3,000, Daudi hakuwa na hofu. Aliandika maneno haya katika kipindi hicho: “Tazama! Mungu ni msaidizi wangu; Yehova yuko pamoja na wale wanaonitegemeza.” (Zab. 54:4; utangulizi) Hivyo, Daudi akaamua kuingia kwenye kambi ya Sauli usiku. Akaomba mtu ajitolee kuandamana naye.
Abishai akajitolea. Abishai alikuwa mpwa wa Daudi naye alikuwa shujaa mwenye ujasiri ingawa pindi fulani hakuwa mwenye rehema. Daudi na Abishai walipoingia kimyakimya katika kambi ya Sauli, waliona kwamba kila mtu alikuwa amelala usingizi. Kwa kweli, Yehova aliwafanya wanaume wote hao washikwe na usingizi mzito. Hatimaye, Daudi na Abishai wakamwona Mfalme Sauli! Yeye pia alikuwa amelala. Hakukuwa na mtu anayemlinda, na mkuki wake ulikuwa umedungwa ardhini karibu na kichwa chake.
Daudi angefanya nini? Ingekuwa rahisi sana kumuua Sauli. Ikiwa angemuua angeacha kukandamizwa na huenda hata angekuwa mfalme. Abishai hakuelewa kwa nini Daudi alikuwa akisitasita. Alimwambia hivi kwa sauti ya chini: “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Na sasa tafadhali, acha nimpigilie ardhini kwa mkuki mara moja tu, wala sitafanya hivyo mara mbili.”
Daudi alikumbuka mara ya mwisho alipokuwa katika hali kama hiyo. Alipokuwa katika nyika ya En-gedi, Sauli aliingia katika pango ambamo Daudi alikuwa akijificha. Kwa kuwa Sauli hakumwona, Daudi angeweza kumuua kwa urahisi. Lakini hakufanya hivyo; alikata tu sehemu ndogo ya vazi la Sauli. Hata hivyo, baadaye jambo hilo liliumiza dhamiri ya Daudi. Alijihisi kwamba ana hatia ya kumvunjia heshima mfalme mtiwa-mafuta wa Yehova.
Usiku huu, huenda haikuwa rahisi kwa Daudi kumzuia Abishai asimuue Sauli. Abishai alikuwa pia akiishi akiwa mkimbizi. Bila shaka, wanaume wote wa Daudi walitamani Sauli aache kuwatesa. Hata hivyo, bado Daudi alikataa kulipiza kisasi. Alimsahihisha Abishai ambaye alitamani sana kumuua Sauli, naye akamsihi awe na subira. Daudi alimhakikishia Abishai hivi: “Yehova mwenyewe atampiga [Sauli], au siku yake itafika naye atakufa, au ataenda vitani na kuuawa.” Kisha Daudi akaongezea kusema hivi kwa uthabiti: “Ni jambo nisiloweza kamwe kuwazia, kulingana na maoni ya Yehova, kwamba niinue mkono wangu dhidi ya mtiwa-mafuta wa Yehova!”
Daudi alitendaje aliposhinikizwa amuue adui mwenye nguvu?
Daudi alijua kwamba kwa wakati unaofaa Yehova angeshughulikia uovu wa Sauli. Katika zaburi iliyotajwa mapema, Daudi aliandikia hivi kumhusu Yehova: “Utawalipa maadui wangu uovu wao wenyewe.” (Zab. 54:5) Kwa hiyo, Daudi na Abishai wakaondoka katika kambi ya Sauli na kwenda juu ya mlima uliokuwa karibu. Daudi akamwita Sauli na wanajeshi wake kwa sauti. Akawakaripia wanaume hao kwa kushindwa kumlinda mfalme wao. Kisha akamkemea Sauli kwa kupoteza wakati wake akimkimbiza, kwa sababu Daudi alisema yeye ni kama “kiroboto mmoja” tu ambaye hawezi kumdhuru mfalme. Sauli aliaibika sana. Akakiri hivi: “Nimetenda kipumbavu, nami nimekosea sana.”
Je, Sauli aliacha kumkimbiza Daudi? Hapana. Daudi alijua kwamba Sauli hakuwa amebadilika. Lakini hakujuta kamwe kwamba alionyesha ujasiri kwa kusikiliza dhamiri yake iliyoongozwa na kanuni za Mungu. Naye Yehova alimbariki huyo mtumishi wake jasiri na mshikamanifu katika njia ambazo hakuwa amewahi kuwazia.
Soma simulizi hili katika Biblia:
Jambo la kuzungumzia:
Daudi alionyesha ujasiri katika njia zipi?
Chimba Zaidi
-
1. Ingawa mara nyingi Abishai alitenda bila rehema na bila kufikiri, aliwateteaje watu wa Yehova kwa ujasiri, na alimteteaje Daudi? (it “Abishai” ¶3-5)
-
2. Kwa nini Daudi alijilinganisha na “kware milimani”? (1 Sam. 26:20; it “Kware” ¶4) A
Ekaterina Kolomeets/stock.adobe.com
Picha A
-
3. Kwa nini Daudi alihitaji kuwa na subira? (w17.08 6 ¶14-15)
-
4. Daudi aliendeleaje kuheshimu mamlaka ya Yehova miaka mingi baada ya matukio yanayotajwa katika simulizi hili? (w21.09 10 ¶8) B
Picha B
Tafakari Masomo Tunayojifunza
-
Ingawa Sauli alifanya makosa mengi, Daudi aliheshimu mamlaka yake. Tunaweza kumwigaje Daudi tunaposhughulika na:
-
wazazi wetu? C
Picha C
-
mamlaka za serikali? D
Picha D
-
wazee wa kutaniko? E
Picha E
-
-
Kwa ujasiri, Daudi alisikiliza dhamiri yake iliyoongozwa na kanuni za Mungu. Ni katika hali zipi tunahitaji kuonyesha ujasiri na kusikiliza dhamiri yetu?
-
Ni katika njia zipi nyingine unaweza kuiga ujasiri ambao Daudi alionyesha katika simulizi hili?
Tafakari Kumhusu Yehova na Kusudi Lake
-
Simulizi hili linanifundisha nini kumhusu Yehova?
-
Simulizi hili linahusianaje na kusudi la Mungu kwa wanadamu?
-
Ningependa kumuuliza Daudi maswali gani atakapofufuliwa?
Jifunze Mengi Zaidi
Ona video inayoonyesha matukio ya simulizi hili.
Watoto wanaweza kujifunza nini kutoka kwa Sauli, ambaye awali alikuwa mnyenyekevu na mwenye kiasi lakini baadaye akaja kuwa mkaidi?

