45 PETRO
“Mimi Ni Mtu Mwenye Dhambi”
PETRO alikuwa mvuvi mwenye bidii na alifanya biashara hiyo pamoja na watu wengine wa familia yake. Alikuwa jasiri na hodari. Mara nyingi alisema kilichokuwa akilini na alitenda upesi alipoona uhitaji. Siku moja, Andrea ndugu yake alimwambia hivi kwa msisimko: “Tumempata Masihi.” Mara moja Petro akawa mfuasi wa Yesu.
Miezi michache baadaye, Yesu alienda Kapernaumu, ambako Petro aliishi. Yesu alipomwona Petro aliona kwamba alikuwa amechoka. Usiku mzima alikuwa amejaribu kuvua samaki lakini hakupata chochote. Yesu alipanda kwenye mashua ya Petro. Baada ya muda, akamwambia aipeleke mashua hiyo mahali penye kina, kisha ashushe nyavu zake tena. Petro hakuamini kwamba anaweza kupata samaki. Kwa kawaida, huwezi kuvua samaki mchana! Kwa hiyo, akamwambia Yesu hivi: “Tumejitahidi kuvua samaki usiku wote na hatukupata chochote.” Lakini Petro akatii na kushusha nyavu zake. Punde si punde, nyavu zilijaa samaki, wakajaza mashua mbili hivi kwamba zikaanza kuzama! Petro akawa na hofu. Akaanguka magotini pa Yesu na kusema: “Bwana ondoka kwangu, kwa sababu mimi ni mtu mwenye dhambi.” Petro alihisi kwamba alikuwa mwenye dhambi nyingi sana hivi kwamba hakustahili kushirikiana na Mwana wa Mungu aliyekuwa na uwezo wa kufanya miujiza. Hata hivyo, Yesu akamhakikishia hivi: “Acha kuogopa. Kuanzia sasa utakuwa ukiwavua watu wakiwa hai.”
Yesu aliona sifa nzuri za Petro, na baadaye akamchagua kuwa mmoja wa mitume wake 12. Petro alionyesha ujasiri katika njia nyingi. Kwa mfano, Yesu aliposema jambo ambalo wanafunzi wake hawakuelewa, wanafunzi wengine waliogopa kumwomba Yesu afafanue jambo hilo, hata hivyo, Petro hakuogopa kuuliza ili apate ujuzi zaidi. Pia, wakati ambapo Yesu alitembea juu ya maji, Petro alikuwa na ujasiri wa kumwomba Yesu ajiunge naye katika muujiza huo.
Mara nyingi Petro alizungumza bila kutafakari, kwa hiyo alihitaji ujasiri ili kukubali kurekebishwa na kufanya mabadiliko
Petro alionyesha aina nyingine ya ujasiri. Mtu anaporekebishwa anahitaji ujasiri kujichunguza kwa unyoofu na unyenyekevu, kutambua udhaifu wake, na kufanya mabadiliko yanayohitajika. Petro alionyesha ujasiri huo tena na tena. Kwa mfano, Yesu alipotabiri kifo chake, Petro alimkemea Yesu kimakosa kwa kumwambia: “Bwana jihurumie.” Yesu alimrekebisha kwa uthabiti kwa sababu alizungumza kama Shetani, yaani, kwa njia iliyoonyesha anapinga mapenzi ya Mungu. Kwa unyenyekevu, Petro alikubali kurekebishwa.
Usiku kabla ya kifo chake, Yesu alitaka kuwafundisha mitume wake somo kuhusu unyenyekevu, kwa hiyo akaanza kuosha miguu yao kama ambavyo mtumishi wa hali ya chini angefanya. Petro akajaribu kumzuia kwa kusema: “Hutaosha kamwe miguu yangu.” Yesu akamrekebisha kwa uthabiti. Kwa hiyo, Petro akasema kitu tofauti kabisa na alichokuwa amesema kwa kumwambia Yesu asimwoshe tu miguu, bali pia amwoshe mikono na kichwa chake. Kwa mara nyingine, Yesu akamrekebisha. Baadaye, Yesu akatabiri kwamba mitume wake wote wangemwacha. Hata hivyo, Petro akasisitiza kwamba hata ikiwa wengine wote wangemwacha Yesu, yeye asingemwacha kamwe! Yesu akamwambia Petro kwamba usiku huo angemkana mara tatu.
Saa chache tu baadaye, askari walikuja na kumkamata Yesu. Kwa ujasiri, Petro alimfuata Yesu kwa umbali. Petro alikuwa kwenye ua wa nyumba ya kuhani mkuu huku Yesu akitendewa vibaya, kudhihakiwa, na kuhukumiwa isivyo haki ndani ya nyumba hiyo. Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwepo wakamtambua Petro kwamba alikuwa mfuasi wa Yesu. Kama Yesu alivyotabiri, Petro akakana mara tatu kwamba hata hakumjua Yesu.
Mara tu baada ya hapo, Yesu akatolewa nje ya nyumba hiyo na kumtazama Petro moja kwa moja. Petro akahuzunika sana. “Akaenda nje akalia kwa uchungu.” Saa chache baadaye, Bwana wake akauawa kikatili. Lazima Petro awe alihisi vibaya kuliko ambavyo amewahi kuhisi maishani. Lakini hakuruhusu kosa lake limvunje moyo. Aliazimia kuvumilia. Alifanya nini baada ya hapo? Badala ya kujitenga, alikutana na mitume wenzake. Baada ya siku kadhaa, akawaambia jambo lenye kustaajabisha: Yesu alikuwa amemtokea! Biblia haisemi Kristo aliyefufuliwa alimwambia nini, lakini ni wazi kwamba Petro aliimarishwa na kufarijika.
Majuma kadhaa baadaye, Yesu alikutana na mitume wake kwenye Bahari ya Galilaya na akampa Petro zawadi iliyoonyesha anampenda sana. Kama tu Petro alivyomkana mara tatu, Yesu alimpa nafasi tatu za kuthibitisha kwamba anampenda Bwana wake. Kisha Yesu akampa Petro mgawo muhimu sana: “Lisha kondoo wangu wadogo.” Katika Sura ya 49, tutajifunza jinsi Petro alivyomtii Yesu na kuonyesha ujasiri wenye kustaajabisha maisha yake yote.
Soma simulizi hili katika Biblia:
Jambo la kuzungumzia:
Petro alionyesha ujasiri katika njia zipi katika kipindi hiki cha maisha yake?
Chimba Zaidi
-
1. Kazi ya uvuvi ya Petro ilihusisha nini? (it “Kuwinda na Kuvua Samaki” ¶6-7) A
Picha A
-
2. Kwa nini Yesu alimpa Simoni jina Kefa (Petro)? (ia 181 ¶8)
-
3. Yesu alimaanisha nini alipowakaribisha Petro na Andrea kuwa “wavuvi wa watu”? (Mt. 4:18-20; w16.05 9 ¶3-4) B
Picha B
-
4. Muda mfupi kabla ya Yesu kupanda kwenda mbinguni, alimuuliza Petro: “Je, unanipenda kuliko hawa?” Huenda Yesu alikuwa akimaanisha nini? (w17.05 22 ¶2; ia 204 ¶26)
Tafakari Masomo Tunayojifunza
-
Unaweza kujifunza nini kutoka kwa Petro kuhusu jinsi ya kuendelea kumtumikia Yehova licha ya kufanya makosa mara kwa mara? C
Picha C
-
Unanufaikaje unapokumbuka jinsi Yehova na Yesu walivyomsamehe Petro kwa hiari?
-
Kulingana na simulizi hili, unaweza kuiga ujasiri wa Petro katika njia zipi nyingine?
Tafakari Kumhusu Yehova na Kusudi Lake
-
Simulizi hili linanifundisha nini kumhusu Yehova?
-
Simulizi hili linahusianaje na kusudi la Mungu kwa wanadamu?
-
Umejifunza mambo gani kumhusu Petro katika simulizi hili ambayo yamekufanya uwe na furaha kwamba alichaguliwa kutawala na Kristo mbinguni?
Jifunze Mengi Zaidi
Wazazi wanaweza kutumiaje mfano wa Petro kuwafundisha watoto wao kuhusu rehema za Yehova?
Chunguza jinsi Petro alivyoendelea kuwa mshikamanifu wengine walipomwacha Yesu.

