Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 27

Mfalme Mbaya Anatawala Misri

Mfalme Mbaya Anatawala Misri

WANAUME hawa wanalazimisha watu kufanya kazi. Mtazame yule mwanamume anayempiga mfanya kazi mmoja kwa fimbo! Wafanya kazi hao ni wa jamaa ya Yakobo, nao wanaitwa Waisraeli. Na wanaume hao wanaowalazimisha kufanya kazi ni Wamisri. Waisraeli wamekuwa watumwa wa Wamisri. Ilikuwa hivyo namna gani?

Kwa miaka mingi jamaa ya Yakobo ilikaa kwa amani huko Misri. Yusufu, aliyekuwa mkuu katika Misri na wa pili kwa mfalme Farao, aliwaangalia vizuri. Lakini Yusufu akafa. Farao mpya, ambaye hakuwapenda Waisraeli, akawa mfalme wa Misri.

Basi Farao huyo mbaya akawafanya Waisraeli kuwa watumwa. Naye akaweka wasimamizi juu yao, wanaume waliokuwa wakali na bila huruma. Wakawalazimisha Waisraeli kufanya kazi ngumu wakijenga miji ya Farao. Lakini Waisraeli waliendelea kuongezeka. Baada ya muda mfupi Wamisri waliogopa kwamba Waisraeli wangekuwa wengi mno na wenye nguvu mno.

Unajua Farao alifanya nini? Aliwaambia wanawake waliosaidia akina mama Waisraeli wakati wa kuzaa watoto wao, akasema: ‘Ueni kila mtoto wa kiume anayezaliwa.’ Lakini wanawake hao walikuwa wazuri, hawakuwaua watoto wachanga.

Basi Farao akaamuru watu wake hivi: ‘Waueni watoto wachanga Waisraeli. Acheni tu watoto wa kike waishi.’ Ilikuwa amri mbaya sana, sivyo? Na tuone namna mtoto mmoja wa kiume alivyookolewa.